SIMULIZI ZA MUZIKI: Uzinduzi wimbo wa Afcon kama tungelipia, tungedai kiingilio

Saturday April 20 2019

 

By Anko Kitime

Siku chache zilizopita nilipata kadi iliyonikaribisha kwenye hafla ya kukabidhi tuzo kwa mshindi wa wimbo bora wa Afcon U17 2019. Nilikuwa na shughuli nyingi asubuhi ya siku hiyo, lakini nilizifanya haraka haraka ili niwahi hafla hiyo iliyoandaliwa na Shirika la Utangazaji nchini (TBC).

Nilikuwa na hamu ya kujua nani mshindi na pia kuusikia na kuufurahia wimbo huo wa ushindi. Na ni kawaida katika hafla za namna hii lazima kuna burudani nyingi za muziki wa aina mbalimbali.

Saa 9.10 mchana nilifika na kukaribishwa na mmoja wa wasaidizi na kuonyeshwa mahali pa kukaa. Lakini hakika hapo ndipo nilipoanza kushangaa, kwa kawaida vituo vya redio vikiwa na shughuli za burudani za aina hii, umati huwa mkubwa sana.

Si ajabu kukuta shughuli zilizotayarishwa na kituo cha redio kujaza uwanja na kukosa hata sehemu ya kutema mate, lakini katika shughuli hii kulikuwa na watu wachache, jambo hili sikuwa nimeliona peke yangu kuna jirani zangu niliokuwa nimekaa nao niliwasikia wakiliongelea hili na kulikuwa na wazo kuwa uchache wa watu ni kutokana na kuwa siku ile ile kulikuwa na mechi kati ya Simba na TP Mazembe.

Lakini TBC walitakiwa kulipigia debe tukio lile ili kupata watu wengi zaidi kuliko waliokuweko siku ile na hasa kwa kuwa nia ya wimbo uliokuwa ukishindaniwa ilikuwa ni kuufanya wimbo wa kushangilia timu ya Afcon U17 Kitaifa.

Baada ya kupata kiti na kukaa nikagundua tatizo kubwa zaidi. Kituo chetu cha utanganzaji cha Taifa kilikuwa kimeleta spika mbovu kiasi kwamba ilikuwa ngumu kusikia vizuri kilichokuwa kikiendelea.

Kwa zama hizi ambapo karibu kila mtaa kuna watu wanakodisha vyombo vya muziki vyenye ubora, ilikuwa mshangao kuwa TBC waliweza kutayarisha shughuli ya wimbo wa Kitaifa kwa kutumia vyombo duni mno.

Pengine ilikuwa heri kuwa watu walikuwa wachache kwani wangekuwa wengi hali ya usikivu ingekuwa mbaya zaidi. Na kwa kuwa lengo lilikuwa kutangaza wimbo mpya, lengo hilo kwa kweli halikufanikiwa. Kundi lililoshinda, Baridi Band, lilipopanda jukwaani wasikilizaji hatukuweza kufaidi utamu wa wimbo wao, na hata wanamuziki wenyewe walionekana kushangaa kwa nini hawakuweza kuteka nyoyo za wasikilizaji.

Kifupi wimbo haukukaribishwa kwa shamra shamra iliyotegemewa. Baada ya washindani kupanda jukwaani walifuatia wasanii wengine lakini hakika usikivu ulikuwa hafifu sana kiasi cha kuwa asilimia kubwa ya tuliohudhuria, kama ilivyokuwa kwa wimbo ulioshinda, tulishindwa kupata ‘mzuka’ kutokana na kutosikia muziki vizuri.

Miaka michache iliyopita Wizara ya Viwanda na Biashara iliwahi kuandaa warsha kuhusu utengenezaji wa zana bora katika soko la ushindani. Watendaji wakuu wa viwanda mbalimbali walikuwepo.

Kulikuwa na mshiriki mmoja aliyeelezea tatizo alilokuwa akilipata katika kiwanda chake cha samani. Alisema alikuwa na mashine za kisasa, mbao nzuri lakini kila mara wafanyakazi walipotengeneza samani hawakuweka umakini katika umalizaji wa kazi, hivyo samani zikawa na mapungufu ambayo yalipunguza thamani za samani hizo sokoni, na kushindwa kupata soko la Kimataifa, hata alipowahakikishia wafanyakazi wake mgao wa asilimia fulani kutokana na mauzo ya samani hizo hakukuwa na mabadiliko, walikuwa wameridhika na mashahara wao wa kila mwezi.

Mjenzi mmoja wa majumba alisema tatizo hilo analipata pia kwa wafanya kazi wake, umalizaji wa mwisho wa kazi umekuwa tatizo, vitu kama ngazi kupishana urefu, au vitasa kutofungwa vizuri, tiles kutopangwa kwa mstari na kadhalika ni mambo ya kawaida kwa wafanyakazi wake na hawaoni kuwa ni tatizo kubwa. Je ni utamaduni wetu kutohangaika kupata kitu bora?

Hadithi ya kula ng’ombe na kubakiza mkia ni kawaida katika kazi nyingi na hakika ndicho nilichokiona kwenye hafla ile ya wimbo wa Afcon U17. TBC walieleza kuwa walipata nyimbo 300, majaji wakazichambua mpaka kupata wimbo bora, kazi ambayo si rahisi, mshindi akapata zawadi ya shilingi milioni kumi, sasa ilikuwaje TBC ikashindwa kumalizia ng’ombe huyu kwa kutayarisha onyesho zuri kwa kutafuta au kukodi vyombo vilivyostahili utoaji wa zawadi ya Kitaifa?

Mgeni rasmi wa shughuli ile alikuwa Waziri wa Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe, kwa kuwa TBC iko chini yake hakutendewa haki kabisa kwa uzembe ule.

Nia ya kuwa na wimbo wa Kitaifa wa kushangilia timu yetu ni nzuri sana lakini kwa ushauri wangu nadhani ingekuwa na manufaa zaidi wimbo kama huu uwahi zaidi kutafutwa, ili mechi zikianza watu wanakuwa wamekwisha ukariri, lakini pia ungekuwa shirikishi zaidi katika kuutafuta.

Katika zama hizi za ushindani, wimbo ambao kutafutwa na kutengenezwa kwake kunahusisha kituo kimoja tu cha utangazaji peke yake, inaweza kuwa sababu tosha ya wimbo huo kutokusikika katika vituo vingine vya redio.

Na kwa vile mashindano yenyewe yamekwishatuendea vibaya, tuchukue hili kama somo kwa kampeni nyingine za aina yake.

Advertisement