Vikundi kuwaokoa wafugaji kuku

Muktasari:

  • Kwa upande mwingine wapo wafugaji wanaopata ugumu kuyafikia masoko. Sababu za hali hii ni nyingi ikiwamo ya wafugaji kukosa ushirikiano baina yao.

Hamasa ya Watanzania kufuga kuku inaendelea kukua siku hadi siku.

Wapo waliofaidika hasa kutokana na kuwa na mipango bora ya ufugaji ikiwamo uhakika wa masoko.

Kwa upande mwingine wapo wafugaji wanaopata ugumu kuyafikia masoko. Sababu za hali hii ni nyingi ikiwamo ya wafugaji kukosa ushirikiano baina yao.

Changamoto ya maarifa sahihi

Wakati hamasa ya kufuga ikishika kasi, wengi wanaojiingiza katika sekta hiyo wanakosa maarifa sahihi ya ufugaji bora wa kuku. Haya ni yale maarifa yatakayo wawezesha kuzalisha kuku, vifaranga au mayai na bidhaa nyingine kwa kiwango kinachokubalika sokoni.

Ni maarifa hayohayo pia yanawafanya wakose mitaji itokanayo na mikopo inayotolewa na taasisi mbalimbali.

Mdau wa ufugaji kutoka shirika la Global Communities, Victor Antony anasema, kuna sababu za msingi zinazowafanya wakulima wengi kushindwa kukopeshwa.

”Tatizo lipo kwa wafugaji na watoaji wa mikopo pia, wengi wanapokwenda kuomba mikopo wanakuwa hawajiandaa, hawana mpango mkakati wa kazi wanazotaka kuzifanya hivyo inakuwa vigumu kwa watoaji mikopo kuwasaidia,’’ anaeleza.

Anaongeza: ‘’ Mimi nimeshakua ofisa mikopo wa benki, utakuta mtu anakuja anataka umpe mkopo wakati huohuo anakuuliza unafikiri utanipa kasi gani?

Antony anaungwa mkono na Julius Mcharo anayesema wafugaji wengi hawana mpango mkakati, hivyo inakuwa vigumu kwao kukopesheka.

“Ni kweli mwitikio ni mkubwa kwa wafugaji wanaohitaji kukopa fedha kwa ajili ya miradi yao, lakini tatizo kubwa tunalokumbana nalo tunapofanya ukaguzi ni kwamba wengi wao wanakua hawajajiandaa,” anasema.

Hata hivyo, Mcharo anayetoka katika taasisi ya ukopeshaji ya Victoria Finance Plc,anasema wafugaji hawana budi kujiunga kwenye vikundi ili iwe rahisi kwao kupata huduma za mikopo.

“Tunakopesha kwa wafugaji wenye kuku mia tano au zaidi lakini wakulima wengi wanafuga chini ya hapo” alifafanua.

Anasema ili kuhakikisha wafugaji wanakuwa na nguvu ya pamoja ni lazima wasajiliwe na wizara

‘’Tunapowatambua wafugaji ni rahisi kuwaongoza na kuwapatia huduma pale wanapohitajI. Mpaka sasa tumesajili vikundi vya wafugaji 21 wa kuku na 21 wa vifaranga pekee”.

Mwenyekiti msaidizi wa chama cha wafugaji wa kuku Kibaha mkoani Pwani anakiri kuwa umoja uliwasaidia katika kupambana na changamoto nyingi ikiwamo ya masoko. Anasema baada ya kuungana walifanikiwa kuwa na nguvu ya pamoja katika kuatafuta masoko

“Licha ya kupata masoko umoja wetu umetusaidia kuwa na ushirika na wadau muhimu katika biashara hii kama vile wauza vifaranga na vyakula vya kuku hivyo kuepuka adha ya kuuziwa vitu feki na madalali,’’ anasema.

Suluhisho la wadau

Wadau wa taasisi za fedha wamekuja na njia njingine ya kukopesha wafugaji wa kuku. Njia hii ni ile ya kuwapa wafugaji vifaa pamoja na mahitaji katika kipindi chote wanachofuga mpaka kupeleka bidhaa zao sokoni bila ya kuwapa mikopo ya fedha.

Antony anasema baada ya kutambua udhaifu wa pande zote mbili yaani wafugaji na watoa mikopo wao wamekua wakijitaidi kutoa semina ili kuwajengea uwezo wahusika.