Wanakijiji wapatiwa neema ya kituo cha afya

“Kinga ni bora kuliko tiba,” hii ni methali iliyowalazimisha wananchi wa Kijiji cha Mafinga kilichopo Wilaya ya Wanging’ombe mkoani Njombe kuitekeleza kwa vitendo tangu kianzishwe mwaka 1976.

Wananchi wa kijiji hicho chenye miaka 43 walilazimika kusafiri umbali mrefu kufuata tiba na kutumia gharama kubwa zikiwamo za usafiri na zile za kujikimu.

“Tulilazimika kusafiri umbali wa kilomita 70 kwenda kupata tiba kwenye Kijiji cha Ilembula au kwenda Kijiji cha Ikonda au Kibena iliyopo umbali wa kilomita 50. Zahanati ya karibu kwetu ni Kipengele iliyopo umbali wa kilomita,” anasema Rafikinjema Mgaya mwenye umri wa miaka 56.

Mgaya ambaye ni mmoja wa viongozi kwenye Kijiji cha Mafinga alikuwa miongoni mwa wananchi waliofika kushuhudia kukamilika kwa ujenzi wa Kituo cha Afya, mradi unaosimamiwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf).

“Tasaf ni mkombozi wetu, niliwahi kuzalia njiani baada ya kuzidiwa na uchungu wakati nikipelekwa hospitali kujifungua,” anasema Mgaya.

Pia, anasema ni wanawake wengi wa kijijini kwao ambao walijifungulia njiani. “Sababu kubwa ni kukosa fedha kwa ajili ya gharama za kusubiri muda wa kujifungua hospitalini.”

Mgaya anasema gharama za kusubiri kujifungua hospitali ambayo inamilikiwa na Misheni hufika hadi Sh80,000. Pia, anasema hata waliojifungulia njiani walitozwa faini na hospitali ambayo ni Sh20,000.

Anasema faini hiyo ni adhabu kwa wanaojifungua nje ya hospitali lengo ni kudhibiti uzembe na matatizo yanayoweza kutokea wakati wa kujifungua.

Mgaya anasema Kituo cha Afya kilichojengwa na Tasaf kitasaidia vijiji vya jirani vya Miyango na Milamba ambavyo pamoja na Mafinga viko kwenye Kata ya Kipengele.

Kiongozi mwingine katika kijiji hicho Rahabu Refesi Chaula (28) anasema naye alizaliwa njiani kutokana na mama yake kushindwa kufika hospitali baada ya kuzidiwa na uchungu njiani.

“Mimi ni mtoto wa pili, mama yangu Josina Chaula aliniambia alinazalia njiani baada ya kushindwa kufika hospitali kutokana na umbali,” anasema Chaula.

Anasema kijiji chao kimepata mkombozi na kwamba mradi wa hospitali hiyo ni chaguo la wananchi na walijitolea nguvu zao kufanya kazi kama vile ufyatuaji na ubebaji wa matofali.

“Hiki ni kituo cha Serikali tofauti na vingine ambavyo ni vya binafsi,” anasema Chaula na kuongeza kuwa hospitali hiyo itasaidia kuwaondolea gharama walizokuwa wakiingia kufuata tiba kwenye hospitali za mbali.

Mratibu wa Tasaf katika halmashauri ya Wanging’ombe, Joyce Mdemwa anasema mradi huo ulibuniwa na wananchi wenyewe baada ya kutaabika kwa miaka 43 kufuata matibabu kwenye maeneo ya mbali.

Anasema kipato cha wananchi katika kijiji hicho ni kidogo, hivyo kutokana na umbali wananchi wengi hawakuwa na uwezo wa kumudu gharama za kufuata matibabu kwenye maeneo hayo.

Mdemwa anasema hospitali hiyo inatarajiwa kukabidhiwa kwa wananchi na huduma kuanza kutolewa mwezi ujao.

Anasema hospitali hiyo iliyojengwa kwa gharama ya Sh65.2 milioni ushiriki wa wananchi ulikuwa ni nguvu zao na pia wameongeza jengo lingine mbali na yaliyofadhiliwa na Tasaf.

Mkakati wa Serikali

Hivi karibuni Serikali ilitangaza kujenga Hospitali za Wilaya 67, ikiwa ni sehemu ya mikakati ya kuimarisha sekta ya Afya nchini.

Akizungumza Katika Kipindi cha Tunatekeleza kinachorushwa na TBC, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tamisemi, Selemani Jafo anasema kuwa Serikali itatumia Sh105 bilioni kutekeleza mradi huo.

“Tangu tupate uhuru tulikuwa na hospitali za wilaya 77 lakini sasa Serikali ya Awamu ya Tano inaenda kuweka historia kwa mageuzi makubwa yanayofanyika katika sekta hii ya afya na tumejipanga kuhakikisha kuwa kila mwananchi anapata huduma bora za afya,” anasisitiza Jafo.

Anasema Serikali imeweka historia, kwa kuwa tangu Taifa lipate uhuru kulikuwa na vituo vya afya vinavyofanya upasuaji 115 nchi nzima, lakini katika mwaka wa fedha 2017/2018 Serikali imejenga vituo vya afya vyenye uwezo wa kufanya upasuaji 208 vinavyoenda sambamba na ujenzi wa hospitali za wilaya zinazoanza kujengwa mwaka huu.

Anasema Bohari Kuu ya Dawa (MSD) imeshapatiwa fedha ili iweze kusambaza vifaa tiba katika vituo vya afya vilivyojengwa ili viweze kuanza kufanya kazi. Katika mwaka wa fedha 2017/2018 Mamlaka za Serikali za Mitaa zimepata mafanikio makubwa katika kuimarisha sekta za elimu, afya na ujenzi wa miundo mbinu kama barabara, vyumba vya madarasa na miundo mbinu mingine inayochochea maendeleo ya wananchi.

Pia, ameziagiza halmashauri zote nchini kusimamia ukusanyaji wa mapato, lengo likiwa ni kuweka mfumo mzuri wa ufuatiliaji ili kuboresha makusanyo na kusimamia matumizi ya fedha hizo katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

“Nawataka wakurugenzi wote wawe wakali katika ukusanyaji mapato na tutatoa onyo maalum kwa halmashauri zote ambazo hazifanyi vizuri katika ukusanyaji mapato,” anasema Jafo.

Historia ya afya

Kabla ya Uhuru, huduma za afya nchini zilikuwa zinatolewa zaidi kwenye maeneo ya shughuli za kiuchumi kama miji na mashamba makubwa.

Baada ya uhuru, Serikali iliweka msukumo zaidi katika kupanua huduma za afya ili kuwafikia wananchi wengi hasa walioko vijijini.

Ili kufanikisha azma hii, Serikali iliweka mfumo wa rufaa wa huduma za afya. Kwa mfumo huu, zahanati, vituo vya afya, hospitali za wilaya, hospitali za mikoa, maalum, kanda na Taifa zilianzishwa.

Pia, anasema Serikali ilihamasisha na kuwezesha hospitali za mashirika ya kidini kushirikiana nayo kutoa huduma kwa wananchi. Kipaumbele kilikuwa katika utoaji wa huduma za tiba zaidi kuliko kinga.