Watoto wa masta wenye ufuasi mkubwa Instagram

Saturday June 30 2018

 

By Kevin Kagambo, Mwananchi

Muziki na kila sanaa kwa sasa imehamia kwenye mitandao ya kijamii hasa Instagram. Hii imekua mno kiasi kwamba kuna wasanii sasa wakitaka kuachia kazi mpya hawamalizi tena soli za viatu kwenda kwenye vyombo vya habari.

Wanatangaza kwa kiasi kikubwa katika mitandao ya kijamii hasa Instagram, Twitter, Facebook na Snapchat na kuiachia hukohuko kwenye mitandao kama Youtube na Vimeo.

Instagram imekuwa kitendea kazi kikuu kwa sasa kiasi kwamba hata kuna baadhi ya kampuni hazimpi msanii shavu la matangazo bila kupima ana wafuasi wangapi kwenye mitandao ya kijamii hasa Instagram.

Umuhimu wake umeongezeka hadi katika kuvuta michongo na hii imesababisha wasanii waanze kutengeneza hadi akaunti kwa ajili ya watoto wao — lengo likiwa ni kuzikamata kampuni zinazotaka kutangaza bidhaa zao kama vile nguo za watoto, shule na benki.

Kwa sababu hiyo ndiyo tukaingia chimbo kukuletea orodha ya watoto wa mastaa wenye wafuasi wengi zaidi Instagram na namna akaunti zao zinavyoendeshwa.

Hata hivyo, sheria za mtandao wa Instagram haziruhusu mtu mwenye umri chini ya miaka 13 kutumia mtandao huo. Kwa hiyo akaunti hizi zina majina ya watoto hao huku zikiwa zinaendeshwa na wazazi au watu walioajiriwa kuendesha akaunti hizo.

Tiffah

Latiffah ndiye mtoto maarufu zaidi Afrika Mashariki kwa kuwa na ufuasi mkubwa Instagram. Ni ‘zao’ la muungano wa mwanamuziki ghali nchini Diamond Platnumz na mwanamke mfanyabiashara kutoka nchini Uganda, Zarina Hassan.

Tiffah alizaliwa Agosti 6, 2015. Wakati akaunti yake ya Instagram ilitengenezwa siku moja kabla ya kuzaliwa kwakwe — yaani Agosti 5.

Tangu hapo hadi leo amejikusanyia jumla ya wafuasi milioni 1.8 na kumfanya kuwa mtoto mwenye wafuasi wengi zaidi Instagram.

Tangu ifunguliwe hadi sasa imechapisha picha na video zinazofikia 1091 huku kila video ikipata wastani wa kupendwa na watu 159,510 na maoni 668. Pia, takwimu zinaonesha kurasa ya Tiffah ndiyo yenye ‘ubize’ zaidi ya kurasa ya mtoto yeyote Tanzania kwa sababu inachapisha wastani wa picha nne hadi tatu karibu kila siku.

Nillan

Anashikilia namba mbili. Ni mtoto wa Pili kwa Diamond Platnumz na watano kwa Zarina Hassan ambaye pia anaonesha kupita kwenye nyendo za dada yake Tiffah.

Akaunti ya Instagram ya Nillan inashikilia namba mbili ikiwa na wafuasi 670,000 na yenyewe pia ikiwa inafuata watu watano tu — yaani mama yake, kaka zake watatu na dada yake Tiffah. Hadi sasa imechapisha jumla ya picha na video 331 huku kila picha au video ikipata wastani wa kupendwa na watu 56,521 na kupata maoni 329.

Cookie

Ni kama kila kinachohusiana na WCB ni rahisi kupata wafuasi.

Cookie ni mtoto wa muigizaji Aunt Ezekiel na Moses Iyobo ambaye ni mnenguaji wa Diamond.

Akaunti ya Instagram ya binti mfalme huyo ina takriban wafuasi 476,000 huku ikiwa imechapisha picha 343 tangu ifunguliwe mwaka 2015.

Dylan

Diamond humuita Young Lion. Ni mtoto mwingine wa Diamond lakini huyu si wa Zari bali Hamisa Mobetto akishika nafasi ya nne akiwa na wafuasi 319,000 huku na posti 79 tu.

Jaydanvanny

Mtoto wa mwanamuziki Rayvan na kisura Fahyma anakamata namba tano.

Akaunti yake inayotumia jina la Jaydanvanny ina jumla ya wafuasi 210,000, idadi ambayo kuna baadhi ya wasanii hawajaifikia.

Jaden

Huko Instagram anatajwa kama mtoto mzuri zaidi. Na hili lilikuja baada ya kuzua gumzo pindi baba yake, muigizaji Vicent Kigosi maarufu Ray alipochapisha picha yake kwa mara ya kwanza —ilipata zaidi ya ‘likes’ 23,000 kiwango ambacho ni cha juu mno ukilinganisha na likes anazopata baba yake katika picha zake za kawaida.

Akaunti yake ya Instagarm ina wafuasi 171,000. Hiyo inamfanya kushika namba sita huku akiwa na post 139 ambazo kwa kawaida hupata wastani wa ‘likes’ 9,607 na ‘comments’ 49.

Wengine

Namba saba inashikiliwa na mtoto wa Alikiba, Sameer ikiwa na wafuasi 132,000. Vigrochoseen wa Hemed PhD anashika namba nane kwa ‘followers’ 84,4000 huku wafuasi 77,100 wakimuweka mtoto wa Aslay aitwaye Mozzah kwenye namba tisa. Namba 10 ni AmayaKiba wa Alikiba kwa ‘followers’ 65,500.

Takwimu hizi ni za hadi Juni 27, 2018.

Advertisement