ZANZIBAR WIKI HII: Wimbi la Maalim Seif Pemba, baba amgomea mwanaye

Wednesday April 10 2019

 

By Muhammed Khamis, Mwananchi [email protected]

Ngome mpya ya CUF ikiongozwa na Profesa Ibrahim Lipumba huenda ikawa na wakati mgumu kufanya siasa Zanzibar, hasa Pemba, ambako kwa miaka mingi iliaminika ndiyo ngome yake kuu.

Hivi karibuni imeshuhudiwa karibu wanachama wake wote na viongozi kuhamia ACT-Wazalendo.

Hata Makamu mwenyekiti mpya wa CUF Zanzibar, Abass Juma Muhunzi ameanza kutikiswa baada ya baba yake mzazi, Mzee Juma Muhunzi pamoja na wana familia kadhaa kukabidhiwa kadi za ACT-Wazalendo katika ofisi za chama hicho zilizopo Ngezi, Wilaya ya Mkoani, Kusini Pemba.

Mzee Muhunzi anasema hakuwa tayari kumfuata au kumpa baraka mtoto wake kwa kile alichodai kuwa “amewasaliti ndugu zake waliosota naye kwa miaka mingi kuisimamisha CUF chini ya Maalim Seif.”

Anasema asingekubali kuona walio wengi wanasalitiwa na ndio maana hakusita kujitokeza hadharani kuchukua kadi ya ACT ili kuudhihirishia umma kwamba haungi mkono kinachofanywa na mtoto wake.

Mzee huyo alisema kijana huyo hana budi kubadili mwelekeo na kuwafuata walio wengi waliohamia ACT-Wazalendo.

Anasema uamuzi wa mwanaye umekuwa ukimfanya aishi maisha magumu ya mawazo na yenye kuufikria.

“Kuna wakati nilipata tetesi kwamba majirani zangu walikuwa wakiamini na mimi ni mshirika wa mwanangu katika hili la kumsaliti Maalim Seif, lakini wapi mimi simo na wala siwezi kuwemo,” aliongezea mzee huyo.

Mzee huyo alikwenda mbali aisema hawezi kushirikiana na mtoto wake hadi pale atakapokua tayari kuunganisha nguvu zake kwenye chama cha ACT.

Akizungumza na gazeti hili Abass alisema kutofautiana na baba yake ni ustaarabu mkubwa kwenye siasa kwa sababu kunaonyesha demokrasia ya kweli na watu kufuata maamuzi yao.

Anasema kilichotokea kinatokana na msisitizo wa majirani waliokuwa wakimfuata mzee huyo na kumuita majina mbalimbali yenye kuashiria usaliti na ndiyo maana alikuwa akiishi kwenye wakati mgumu.

“Aliitwa msaliti na hata watoto wadogo kule kijijini kwetu. Ukweli mzee hakuwa na furaha na nahisi ndiyo maana alipofuatwa kwenda kwenye mkutano wa Zitto hakuweza kukataa.

Pamoja na hayo, Abass alisema uwepo wa tofauti baina yake na mzazi wake unatokana na ushawishi mkubwa wa majirani.

Aidha, alisema ifike wakati watu wafahamu kwamba kilichowaunganisha kuwa familia moja si siasa bali ni baba na mwana, hivyo mazingira hayo hayatopotea na yataendelea kubaki hivyo na kwamba siku moja mzazi wake huyo atafahamu ukweli uliopo.

Kuhusu mazingira ya CUF kufanya siasa Pemba kwa sasa, alisema hakuna ugumu wowote ule na muda mfupi kuanzia sasa kazi hiyo itaanza.

Wasemavyo majirani

Miongoni mwa majirani na marafiki wa karibu na Abass, Khamis Kassim Mohamed ambaye ni muumini na mfuasi wa Maalim Seif, alisema muda wote alioishi na Abass hakuwahi kugundua kama alikuwa tofauti na Maalim Seif ingawaje wakati mwingine alikuwa na misimamo ambayo si rahisi kueleweka.

Amesema Abass ni mwanasiasa mwerevu na ambae anaamini iwapo angeunganisha nguvu zake ACT-Wazalendo bila shaka kungekua na tija kubwa.

Hata hivyo, alisema licha ya uwezo wake, hadhani kama atafanya siasa zake kama awali.

Wiki moja iliyopita ziara ya Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe na Maalim Seif kisiwani Pemba ilibadili upepo wa kisiasa kwa kuwazoa viongozi wa CUF wa wilaya zote nne.

Viongozi hao wapatao 478 ni wa nafasi ya wenyeviti wa wilaya makatibu pamoja na wajumbe wa kamati tendaji wa majimbo yote 18 ya kisiwa cha Pemba.

Hii ni dhahiri ACT imevunja ngome ya CUF iliyojengwa kwa miaka 26 kwa siku tatu tu.

Wakati akikabidhi kadi za wanachama wapya, Zitto mara zote alisisitiza umoja na mshikamano kuwa ndiyo silaha pekee itakayowakomboa Wazanzibari na Watanzania kwa ujumla kuishi kwenye utawala unaoheshimu haki za binadamu na utawala bora.

Alichokisema Maalim Seif

Katika ziara hizo mwanachama mpya wa ACT-Wazalendo na aliyekuua katibu mkuu wa CUF, Maalim Seif aliwataka waliokuwa wanachama wa CUF kutokuingia kwenye mtego wa kukubali kuchokozeka ili kuepuka hujuma zinazopangwa dhidi yao.

Alisema kuwa wengi hawakufahamu kwamba alikuwa na mpango mbadala baada ya kumnyang’anya CUF, lakini baada ya kujiunga na ACT ambayo inawatesa.

Aliwataka waliopewa nafasi za kukaimu uenyekiti wa majimbo na wilaya wafanye kazi za kuratibu wanachama wapya kila leo huku wakijipanga kwa uchaguzi mkuu wa 2020.

Waliojiunga ACT watoa neno

Miongoni mwa wanachama wapya ACT ni aliyekuwa mwenyekiti wa CUF Wilaya ya Micheweni, Rashid Khalid ambaye alisema kila kitu kimekamilika katika kuratibu zoezi la uandikishaji wanachama wapya.

Alisema katika Wilaya ya Micheweni ACT itakuwa na nguvu zaidi kuliko chama chochote kile Zanzibar.

Aliyekuwa katibu wa CUF Wilaya ya Chakechake Saleh Nassor Juma alisema kwa upande wake kazi imemalizika na ndio maana kumekuwa na mapokezi makubwa ya ACT wilayani humo.

Advertisement