Zamani wanaume waliimba kuhusu matatizo ya wanawake

Mume wangu Jerry wa Mlimani Park Orchestra, Mfaume wa Mlimani Park Orchestra, Mfaume wa Orchestra Makassy, Nimemkaribisha nyoka wa Tancut Almasi Orchestra, Mabruki wa Maquis, Mke Mkubwa wa Vijana Jazz, Rehani wa Oss Ndekule, Kalubandika wa Maquis na Ndoa ya Mateso wa Dar es Salaam International Orchestra ni baadhi ya nyimbo kati ya nyingi za bendi tofauti lakini zina kitu kimoja ambacho kinafanana.

Waimbaji walikuwa wanaume, walikuwa wakiimba nafasi za wanawake. Hebu tuangalie baadhi ya maneno katika nyimbo hizi. Wimbo Mfaume wa Orchestra Makassy uliimbwa na Issa Nundu na Kyanga Songa ulikuwa na maneno haya,

Ewe Mfaume umefikaa nyumbani kwetu

Mimi bado nasoma mama,

Ukanieleza kwamba unataka tufunge

Pingu za maisha pamoja

Nami nikakweleza subiri

Nikimaliza shule ewe Mfaume

Kwa kuwa siwezi kuolewa bado ningali mwanafunzi oyoo.

Sehemu ya wimbo wa Tancut Almasi Orchestra Nimemkaribisha Nyoka ulioimbwa na Kasaloo Kyanga ulikuwa na maneno yafuatayo.

Mume wangu alipotoka kazini,

Nikamuelezea mambo yote mama

Naye pia akakubali kama ni dada yake ambaye wamezaliwa tumbo moja

Basi tukaendelea kuishi kama mtu na wifi yake ndani ya nyumba

Marijani Rajabu akiwa na Dar es salaam International naye aliimba maneno haya katika wimbo Ndoa ya Mateso;

Niulizieni enyi walimwengu, huyu mwanaume anavyonitesa

Hii ndio haki au ni mateso, hii ndio haki au ni mateso,

Kanitoa kwetu kwa baba na mama, kwa vigelegele na heshima nyingi,

Tizameni sasa anavyonigeuka, Tizameni sasa anavyonigeuka

Ananipa mateso huku ugenini sina hata ndugu wa kunisaidia

Nami nina watoto jamani tabu gani

Nami nina watoto jamani tabu gani

Kwani kuolewa ni jambo la ajabu au kuolewa sawa na utumwa

Kama ndivyo hivyo mimi nimeshindwa

Kama ndio hivyo mimi nimeshindwa

Natoa ushahidi kwako we mjumbe, mwambie huyo bwana anipe talaka yangu

Nisije kuondoka ikawa maneno, nisije kuondoka ikawa maneno.

Wimbo ulioitwa Masikitiko wa Tancut Almasi Orchestra ulikuwa na maneno haya,

Kinachonisikitisha ni kuona kwamba nakosa mume, wa kunioa mama, nami nijisikie kama wenzangu waliobahatika kuolewa iyooo iyoo

Nyimbo hizi zilitungwa na kuimbwa na wanaume na ni nyimbo ambazo bado hazijapoteza umaarufu japo nyingine zina zaidi ya miaka 30 toka zilipoanza kusikika. Haikuwa kitu cha ajabu kwa wanaume kuimba kuhusu matatizo na maisha ya wanawake hapo zamani.

Moja ya sababu ilikuwa ni kukosekana kwa waimbaji wa kike katika muziki wa bendi za dansi, lakini hata pale ambapo bendi zilikuwa na waimbaji wa kike bado nyimbo zilizohusu wanawake zilitungwa na kuimbwa na wanaume bila kuweko na shida yoyote.

Ulikuwa usanii wa kiwango cha juu sana. Siku hizi ni nadra sana kusikia sanaa ya aina hii, na hakika ilipigwa vita na hata viongozi kadhaa ambao waliona ni kosa wanaume kuimba nafasi za wanawake.

Lakini jambo hili si geni kabisa katika sanaa, Tyler Perry ni muigizaji maarufu ambaye moja ya sifa yake kubwa ni kuigiza nafasi ya mwanamke, Mabel ‘Madea’ Simmons, na ameweza kutengeneza sinema nyingi akiigiza kama mwanamke Madea, na hakika ukiangalia sinema hizo utaona jinsi alivyoweza kuvaa nafasi yake. Hata hapa kwetu msanii Joti amekuwa na mafanikio makubwa katika kuigiza nafasi ya mwanamke katika vichekesho vyake vingi, na ndivyo ilivyokuwa kwa watunzi na waimbaji wengi wa bendi wa zamani. Siku hizi kuna waimbaji wengi sana wa kike lakini je wanazungumza matatizo ya wanawake kwa uzito uliokuwa unabebwa na wanaume katika nyimbo za dansi zilizotajwa? Kuna waimbaji wa kike mashuhuri kwa ‘mipasho’, hizi ni tungo ambazo mara nyingi ni kuwasema wanawake wengine na hasa katika kugombea penzi la wanaume. Kundi jingine la waimbaji wa kike wamejikita zaidi katika kuimba nyimbo za mapenzi, hivyo pengo la nyimbo zinazoongelea matatizo ya wanawake limebaki, pengine inasubiriwa wanaume waanze tena kutunga na kuimba nyimbo kwa kuvaa matatizo ya wanawake. Katika kuongea na baadhi ya waimbaji wa kiume wa siku hizi wengi walisema wanaona aibu kuimba nyimbo ambazo wanaimba kama ‘ mke wa mtu’, kubwa likiwa ni kuogopa kuhisiwa kuwa si wanaume kamili. Hakika hapa nalazimika kushangaa kidogo, kwani mwanamuziki huyohuyo ambaye ameamua kutoga masikio na kuvaa heleni na kutinda nyusi huku amesuka vizuri nywele zake, na suruali kashusha kuonyesha nguo yake ya ndani anasema anaona aibu kuimba nyimbo zenye maneno ya wanawake kwani atahisiwa vibaya!!!

Nadhani usanii huu wa wanaume kuimba nyimbo zenye ujumbe kwa wanawake, bado una nafasi katika sehemu kubwa ya jamii yetu ambayo haina hisia mbaya, na pia kwa kuwa waimbaji wa kike wenyewe hawataki kubeba jukumu lao la kuelimisha matatizo yao na ya wanawake wenzao. Nimalize kwa kuandika maneno ya wimbo Nirudishe Kwetu uliopigwa na Msondo miaka ya 70, na kuimbwa na akina Hassan Rehani Bitchuka na Mzee Muhidin Gurumo..

Mume wangu nirudishe kwetu, Nyumba yako imekwisha nishinda. Sababu watoto wako sielewani nao, kila nisemalo wasema mimi mama wa kambo

Kumbuka nilikueleza usimuache mama watoto wako

Kumbuka nilikueleza usimuache mama watoto wako

Watoto wengi mmekwisha zaa nae mrudishe mama watoto wako.