Mambo ya kuzingatia baada ya kuajiriwa

Umesikia tangazo la nafasi ya kazi, umeomba kazi, umeitwa kwenye usaili na umeshinda.

Nini kinafuata unapokuwa kwenye kipindi cha matazamio?

Kipindi cha matazamio kina faida kwa pande zote mbili. Kwanza, kwa mwajiri kinamsaidia kujiridhisha ikiwa kweli mwajiriwa mpya ana sifa na ujuzi.

Pia, kwa upande wa mwajiriwa, kipindi hiki kinamsaidia kufanya maamuzi ikiwa mazingira ya kazi yanamfaa.

Katika kufanya tathmini, mwajiriwa hafungwi sana na mkataba alionao na mwajiri.

Kwa mfano, mwajiriwa anaweza kuacha kazi bila kulazimika kufuata matakwa ya mkataba.

Mwajiri naye kwa upande mwingine anaweza kumwachisha kazi mwajiriwa bila kulazimika kufuata matakwa ya mkataba.

Hata hivyo, kutokufungwa na mkataba hakumaanishi una uhuru wa kumtendea mwajiriwa/mwajiri chochote bila kufuata taratibu za kazi.

Katika mazingira ambayo mwajiri anafikiri hajaridhishwa na mwajiriwa mpya, analazimika kufuata Sheria ya Ajira na Uhusiano Kazini ya Mwaka 2004, Kanuni za Ajira na Uhusiano Kazini za Mwaka 2007, Sheria ya Usalama na Afya Mahala pa Kazi ya Mwaka 2003 pamoja na marekebisho yake.

Makala haya yanaonyesha mambo ya kuzingatia unapokuwa kwenye kipindi hiki ili kukusaidia kufikia hatua ya kuthibitishwa kazini.

Kidhi matarajio ya mwajiri

Kazi yako ya kwanza baada ya kuajiriwa ni kumthibitishia mwajiri wako mpya kuwa unao ujuzi uliouonyesha kwenye mchakato wa kukupata.

Usifanye kosa la kujisahau ukajikuta unashindwa kufikia matarajio yake.

Katika kukusaidia kuelewa wajibu wako ni upi, mwajiri makini atakupa barua inayofafanua majukumu yanayoambatana na nafasi yako mpya pamoja na mkataba wa kazi. Soma nyaraka hizi na uzitunze vizuri kwa sababu ndizo zinazokulinda kwenye eneo la kazi. Mwajiri kwa upande wake, ana wajibu wa kuweka utaratibu mzuri wa kukuwezesha kutekeleza majukumu yako kwa viwango anavyovitarajia.

Hiyo ni pamoja na kukufahamisha tunu na miiko ya nafasi ya kazi uliyopewa; mambo yatakayotazamwa katika kipindi cha majaribio; ujuzi unaotarajiwa kuwa nao na mpango utakaotumika kubaini changamoto za kazi zitakazojitokeza katika kipindi hicho.

Unapopata changamoto katika kipindi hiki, ni vizuri kushirikiana na ofisa (idara ya) rasilimali watu kazini kwako ili kupata ushauri na maelekezo yatakayosaidia kutekeleza majukumu yako vizuri.

Onyesha umakini kazini

Ufanisi katika kazi, kwa kiasi kikubwa, unategemea nidhamu. Namna gani wewe kama mwajiriwa mpya unaheshimu kazi yako kwa kuwahi kazini na kuwasilisha mrejesho wa kazi kwa muda uliopangwa hiyo ndiyo inaitwa nidhamu ya kazi.

Hakikisha unawahi kazini mapema. Kama ofisi ina utaratibu wa kusaini kitabu cha mahudhurio, usiache kusaini ndani ya muda uliopangwa. Usiwe mtu wa kukosa vikao vinavyoitishwa kazini. Unapokosekana kwenye vikao, ni rahisi kuonekana huna nidhamu ya kazi inayotakiwa.

Kadhalika, nidhamu ya kazi ni pamoja mpangilio mzuri wa jumla wa majukumu yako ya kila siku.

Huwezi kupangilia majukumu yako kama huwezi kutunza muda wako vizuri. Amka mapema, anza safari ya kwenda kazini.

Tumia kitabu cha kumbukumbu za kila siku kuainisha majukumu unayotakiwa kuyakamilisha kila siku. Unapofanya hivyo, utaweza kupima utendaji wako na hivyo kukamilisha na kukabidhi ripoti zako kwa muda unaotarajiwa.

Kuchelewesha kazi si dalili nzuri kwa mwajiriwa mpya anayetakiwa kuthibitisha kuwa ana ari na weledi wa kutekeleza majukumu yake ipasavyo.

Fahamu utamaduni wa taasisi

Kila eneo la kazi lina utamaduni wake. Huu ni utaratibu usio rasmi uliozoeleka katika taasisi ambao kila mmoja anajikuta akiufuata ingawa haujaandikwa kokote.

Unawajibika kudadisi na kujua taasisi yako inaongozwa na utamaduni upi. Kwa mfano, kuna taasisi zisizoruhusu mavazi ya namna fulani kuvaliwa kazini. Kuwa mwepesi kujifunza mambo kama hayo.

Kadhalika, kila taasisi inaongozwa na ‘siasa’ zake za ndani na nje. ‘Siasa’ ni taratibu zisizo rasmi zinazongoza uhusiano baina ya wafanyakazi ndani ya taasisi na namna taasisi inavyojenga taswira yake machoni pa jamii. Unalazimika kufanya kazi ya ziada kuzielewa.

Jenga uhusiano na watu

Huwezi kufanikiwa kama huna uhusiano mzuri na watu. Kumbuka watu uliowakuta kazini, hata kama umewazidi elimu, bado wana uzoefu kuliko wewe. Unapojenga uhusiano mzuri na watu hawa unajiweka kwenye nafasi nzuri ya kupunguza makosa.

Tafiti kujua nani ana sauti ipi kwa wakati gani. Kuna watu wana nguvu kubwa kwenye taasisi. Ukiwafahamu itakusaidia kujua unaanzia wapi unapokuwa na wazo jipya. Pia, hawakosekani watu wanaopenda majungu. Huhitaji muda mrefu kuwabaini watu wa namna hii na kujua namna bora ya kufanya nao kazi bila kuwa sehemu ya mtandao wa majungu kazini.

Christian Bwaya ni Mhadhiri Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge, Moshi. Mawasiliano +255 754870815