Mbinu za kurudisha ari ya kazi iliyopotea

Labda unajisikia kuchoka. Umefanya kazi kwa miaka mingi lakini hupati mafanikio uliyoyatarajia.

Huna tena morale ya kazi na huna tena ule msisimko wa kujitambulisha na kampuni au taasisi.

Labda kipato hakitoshi na mwajiri naye haonekani kujali kazi kubwa unayofanya. Hapa ninakupitisha kwenye maeneo saba ya kutafakari unapojisikia kuchoka na kazi yako.

Tathmini kazi yako

Kufanya kazi hiyo hiyo kwa muda mrefu kunachosha. Majukumu yale yale, watu wale wale, malengo yale yale yanaweza kuwa sababu ya kutamani mabadiliko. Ufumbuzi hapa unaweza kuwa kujitathmini.

Tazama malengo ya kazi yako na kuona kama majukumu uliyonayo yanaakisi malengo ya kazi yako. Ikiwa ndivyo na bado unajisikia kuchoka, pengine hiyo ni ishara kuwa uwezo wako haujatumika vya kutosha. Katika mazingira haya pengine ni wakati wa kupanua malengo yako kwa kujiongezea majukumu yanayoakisi uwezo na vipawa ulivyonavyo.

Tafuta watu wapya

Mafanikio kazini, wakati mwingine, yanategemea aina ya mtandao wa watu tulionao.

Ikiwa umezungukwa na watu wanaokukatisha tamaa, watu ambao mazungumzo yao hulenga kukufanya ujione huna thamani, uwezekano ni mkubwa utaishia kukata tamaa na hutaweza kufurahia kazi yako.

Tathmini aina ya watu wanaokuzunguka. Je, watu unaotumia nao muda wako wa ziada wanakufanya uwe na matumaini au wanakukatisha tamaa? Pengine ni wakati wa kupunguza ukaribu na watu ambao kila mkikutana mnazungumza mambo yale yale, mnalalamikia mfumo, mnabishania siasa na kuishia kukatishana tamaa.

Pengine ni wakati wa kuongeza wigo wa watu wapya wanaoweza kukupa mawazo mapya.

Marafiki wenye umri kama wa kwako lakini wenye fikra zinazochemka watakaokufanya uyaone maisha kwa mtazamo tofauti. Kwa kufanya hivyo hamasa yako ya kazi inaweza kurejea.

Jitolee

Kujitolea ujuzi wako, uzoefu na muda wako kuwasaidia wengine bila malipo inaweza kuwa namna moja wapo ya kurejesha furaha iliyopotea. Unapojitolea mbali na kujiongezea wigo wa marafiki, pia unajifunza mambo mapya katika mazingira mapya.

Ingawa ni ukweli kuwa unapokuwa mwajiriwa, muda unaweza kuwa changamoto kubwa, lakini bado unaweza kutengeneza ratiba yako vizuri ukajitolea kufanya kitu kingine nje ya ajira yako kitakachokufanya ujisikie umekuwa msaada kwa mtu aliyeuhitaji msaada wako.

Tafuta fursa hizi kwenye maeneo uliyopo ili kuangalia namna gani maarifa na ujuzi ulionao yanavyoweza kuwa ufumbuzi kwa tatizo fulani.

Jiongezee thamani

Kuchoka kazi wakati mwingine kunasababishwa na kukosa ujuzi stahiki. Unapofanya vitu kwa mtindo ule ule unafika mahali huoni tija ya kile unachokifanya. Katika mazingira haya, kujifunza ujuzi mpya kunaweza kukusaidia kurudisha ile ari ya kazi iliyopotea.

Kwa nini usijiandikishe kujiendeleza kimasomo? Huenda ukiongeza kidogo kiwango cha elimu utaanza kujisikia utoshelevu zaidi. Kama ajira yako hairuhusu kupata likizo ya masomo, tafuta kozi fupi au ndefu zinatolewa kwa njia ya masafa, nyakati za jioni au mwisho wa wiki.

Ikiwa hilo haliwezekani, soma vitabu na majarida kuhusu eneo lako la ujuzi. Kwa kufanya hivyo, ujuzi wako utaongezeka, thamani yako kazini itaongezeka na morale yako ya kazi itarudi.

Jiongezee kipato

Inawezekana umechoka kazi kwa sababu juhudi zako kazini hazikupi kipato unachotarajia. Kwa nini usifikirie kutumia muda wako wa ziada ‘kuhangaika’ kidogo? Badala ya kutoka kazini na kwenda vijiweni ‘kupiga stori’ kwa nini usione uwezekano wa kutumia uzoefu wako kazini kujiongezea kipato?

Kama wewe ni mhasibu aliyethibitishwa na bodi, kafundishe wahasibu wanaojiandaa na mitihani ya bodi. Kama wewe ni mwalimu, fungua ‘tuition’ kwa wanafunzi. Siyo lazima kufanya biashara ya kuchuuza bidhaa. Unaweza kutumia utaalam wako kufanya usadi (consultancy) na ukajiongezea kipato.

Tafuta ushauri

Wakati mwingine unajisikia kuchoka kwa sababu tu umekosa mwelekeo wa maisha. Si wakati wote huwa tunajua kuwa hatujui cha kufanya. Tunaamini tunajua lakini kumbe hatujui. Matokeo yake tunajikuta hatupendi kazi na hatujui sababu.

Mtafute mtu mwenye uzoefu anayefanya kazi isiyotofautiana sana na hiyo unayoifanya akusaidie mawazo. Uzoefu alionao mtu huyu unaweza kukufungua macho na hivyo ukajifunza uzoefu mpya. Mtu aliyekutangulia anajua siri nyingi za maisha. Mkabidhi mipango yako hatakuacha.

Jitafakari

Pamoja na sababu nyingine kuchoka kazi kunaweza kuwa ishara kwamba umechoshwa na mazingira ya kazi. Tafiti za ajira na kazi zinaonyesha kuwa watu wanaofanya kazi eneo hilo hilo kwa zaidi ya miaka mitano wanazoea kazi na kupoteza ari ya kazi.

Christian Bwaya ni Mhadhiri wa Saikolojia, Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge (MWECAU). Mawasiliano 0754870815, twitter: @bwaya