TULONGE AJIRA: Sababu za biashara kukosa wateja

Wateja ndiyo nguzo muhimu katika mafanikio ya biashara yoyote. Muda mwingine unaweza ukajiuliza kwanini mteja au wateja fulani siku hizi huwaoni katika biashara yako? Unaanza kumtafuta mchawi ni nani katika biashara yako, kumbe mchawi ni wewe unayeweza ukawavuta wateja wengi au kuwapoteza.

Hii inatoka na namna unavyotoa huduma yako na kumhudumia mteja. Leo tutaangalia mambo yanayosababisha kumpoteza au kumkera mteja.

Kuchelewa kufungua biashara; kuna baadhi ya wamiliki wa biashara wanachelewa kufungua biashara na unakuta mteja anahitaji kupata huduma mapema ukilinganisha na muda wako unaofungua biashara. Sababu hii inaweza ikampoteza mteja au kumkera kama tabia yako ya kila siku ni kuchelewa; mteja anakusubiri katika eneo la biashara badala ya wewe kumsubiri mteja, sababu hiyo inaweza ikapoteza mteja wako.

Kufanya biashara kwa mazoea; unapokuwa umeamua kufanyabiashara basi fanya kila siku bila mazoea au kujisikia. Wafanyabiashara wengine wanafanya biashara kwa kujisikia au kwa mazoea. Mfano, leo anaweza kufungua biashara, kesho akafunga; sasa tabia kama hii inaweza kumsababishia mteja kupata kero na kukuhama kabisa. Ukiamua kufanya biashara fanya kila siku bila kukata tamaa.

Kuacha biashara peke yake; kuna tabia ya wafanyabiashara wanaweza kufungua biashara yao na kuacha peke yake. Kazi yake inakuwa ni kuzunguka zunguka au kwenda sehemu kupiga stori huku akiachia biashara yake wazi. Mteja akija anapata shida ya kumtafuta mtoa huduma. Unafikiri kama kuna sehemu nyingine ambayo akiamua kwenda na kumkuta mtoa huduma na akamuhudumia vizuri, atashawishika kukuhama?

Kauli mbaya; unapokuwa unafanya biashara unatakiwa uwe na kauli nzuri zitakazomvutia mteja kuja kupata huduma kwako. Kuna wateja wengine ndiyo wanaweza kuwa na kauli mbaya lakini hupaswi kumjibu vibaya mteja, soma sana saikolojia ya mteja wako, muhudumie kwa upendo na ukarimu. Kwa hiyo kauli mbaya ni moja ya sababu zinazoweza kukuleteamatokeo hasi katika biashara yako.Chunga sana ulimi wako katika biashara.

Kutopenda biashara; kuna wafanyabiashara wengine wanatoa huduma kama vile wamelazimishwa kufanya biashara hiyo. Kutopenda kazi yako ni moja ya sababu zitakozomfanya mteja asivutiwe na biashara. Kwa elimu ya biashara, ujasiriamali na kilimo biashara fuatilia kupitia kurasa zetu; Facebook, Instagram na Twitter kwa jina la Elimika Ung’are.