Epanko, mgodi wa ‘graphite’ unaosubiri ridhaa ya wananchi Mahenge

Julius Mnganga, Mwananchi

Siku chache baada ya Rais John Magufuli kuteta na Kansela Angela Markel, kampuni ya Kiraban Resources ya Ujerumani imetangaza kupata mkopo wa kufanikisha ujenzi wa mgodi wa madini ya kinywe au graphite nchini.

Mwezi uliopita, Rais Magufuli alipokea simu ya Markel na wakazungumza mengi ikiwamo huimarisha uhusiano wa kiuchumi baina ya Tanzania na Ujerumani kwa kurahisisha mazingira ya biashara kwa wawekezaji wa mataifa haya mawili.

Kwa kinachoonekana kama mwanzo wa kuanza kwa utekelezaji wa makubaliano hayo ya wakuu wa nchi, Aprili Mosi, Kiraban imetangaza uhakika wa kupata mkopo kutoka Benki ya KfW IPEX ya nchini humo ili kutekelea mradi uliopo Kijiji cha Epanko wilayani Mahenge, Morogoro.

“Kibaran Resources inapenda kuujulisha umma kuwa imesaini mkataba wa mkopo na Benki ya KfW IPEX ili kufanikisha mradi wake wa Epanko. Mkataba huu umeridhiwa baada ya majadiliano na wizara ya madini, kamisheni ya madini na Benki Kuu ya Tanzania kukidhi mabadiliko ya sheria yaliyofanywa mwaka 2017,” inasomeka sehemu ya taarifa ya kampuni hiyo.

Kwenye taarifa yake, kampuni hiyo imebainisha kuwa mazingira ya uwekezaji nchini yanazidi kuimarika hasa katika sekta ya madini na benki kubwa duniani zinapata imani ya kufanikisha uwekezaji.

Ikiwa imewekeza zaidi ya Dola 35 milioni za Marekani mpaka sasa, kampuni hiyo ina uhakika wa kukopeshwa Dola 40 milioni na benki hiyo ya Kijerumani.

Mshauri wa masuala ya habari wa kampuni hiyo, Sauda Kilumanga anasema wanahitaji Dola 60 milioni kufanikisha sehemu iliyobaki kabla mgodi haujaanza kufanyakazi.

Masharti

Kabla ya kuanza utekelezaji wa mradi huo, kampuni ya Kibaran inatakiwa kukidhi matakwa ya sheria nchini. Benki ya KfW IPEX inaitaka kufanya upembuzi yakinifu unaokubalika kwenye taasisi za fedha, kuzingatia athari za kimazingira, afya na uchumi kwa mujibu wa vigezo vya Benki ya Dunia.

Ili kupata mkopo huo, kampuni hiyo inatakiwa kuwa na leseni na ripoti ya mazingira iliyothibitishwa na Baraza la Mazingira Tanzania (NEMC) pamoja na mkataba wa mauzo ya madini yatakayochimbwa.

Benki hiyo pia inaitaka kukamilisha matakwa yote ya kisheria ikiwa ni pamoja na fidia kwa wananchi.

Meneja wa uhusiano wa jamii wa kampuni hiyo, Bernard Mihayo anasema leseni na cheti cha mazingira wanavyo tangu mwaka 2015 na kinachoendelea hivi sasa ni mazungumzo na kaya 350 zilizopo Epanko.

“Asilimia 82 ya wananchi wote wameridhia kufanyiwa tathmini na kuwa tayari kuhamishiwa Kijiji cha Kitonga ambako watajengewa nyumba mpya na kulipwa hela ya chakula kwa miaka miwili,” anasema Mihayo.

Licha ya Dola 850 milioni zinazotarajiwa kulipwa na kampuni hiyo kama kodi, gawio, ada, mrabaha na ununuzi wa huduma na bidhaa tofauti ndnai ya miaka 20 ya operesheni yake, inakadiliwa itachangia zaidi ya Dola 2.5 bilioni kwenye pato la Taifa (GDP).

Pamoja na hayo yote, inatakiwa kujenga shule, ofisi za umma, hospitali, makanisa na kutoa huduma nyingine mfano bima ya afya ili kujenga uhusiano endelevu.

Mihayo anasema hayo yote yatafanywa ingawa baadhi yameshaanza kutekelezwa mara tu uthamini wa mali za wananchi wanaotakiwa kupisha mradi huo utakapokamilika.

“Katika kaya 350 zilizopo, asilimia 82 wamekubali kupisha mradi. Waliobaki bado tunaendelea kujadiliana nao. Khusu fidia, wapo wanaotaka fedha taslimu na wengine wakitaka kujengewa nyumba,” anasema.

Faida kwa jamii

Licha ya fidia itakayojumuisha kujengewa nyumba nzuri, kubwa na za kisasa kuliko zilizopo, Mihayo anasema kwa kuwa watakakohamia hakuna rutuba ya kutosha, kampuni itawapa chakula kwa miaka miwili wakati wataalamu wakisaidia kuboresha kilimo.

Pamoja na hilo, kila kaya itatakiwa kumpendekeza mtoto mmoja ambaye atasomeshwa ufundi stadi kisha kuajiriwa mgodini atakapohitimu na itaanzishwa Saccos au Vicoba itakayokuwa inatoa mikopo nafuu kufanikisha shughuli za wananchi hao.

Kwenye Kijiji cha Kitonga zitakakohamia kaya hizo, kuna kaya nyingine 45 hivyo kampuni hiyo itapaswa kujenga shule na zahanati kwa ajili ya huduma za jamii.

“Wananchi walioridhia kufanyiwa uthamini tumeshawafungulia akaunti Benki ya CRDB kilichobaki ni kuwashawishi wachache waliobaki. Endapo wataendelea kugoma, ikifika Novemba mchakato itabidi uanze upya,” anasema Mihayo.

Tume ya madini

Katibu mtendaji wa Tume ya Madini, Profesa Shukrani Manya anasema tangu kuanza kutumika kwa sheria mpya ya madini iliyopitishwa mwaka 2017, kampuni nyingi zimejitokeza kuomba leseni na zipo kwenye hatua mbalimbali za utekelezaji.

Kuhusu maendeleo ya mradi wa kinywe uliopo Mahenge na utekelezaji wake, anasema kuna kampuni mbili zinazotaka kuchimba madini hayo.

“Sijapata taarifa ya kampuni iliyopata mkopo wa kuwekeza Mahenge lakini nafahamu zipi mbili ambazo tumezipo leseni. Kilichobaki ni kumalizana na halmashauri kabla uchimbaji haujanza,” anasema.

Kwa utaratibu uliopo, baada ya kampuni kupewa leseni ya uchimbaji ambayo hutolewa kwa tume kujiridhisha kuhusu uwezo wa kitaalamu na fedha wa mwombaji na kiapo cha uadilifu, ni lazima wananchi washirikishwe

“Halmashauri ndizo zenye watu. Hilo hufanyika huko,” anasema Profesa Manya.

Hata hivyo, Mihayo anasema wanapata ushirikiano wa kutosha kutoka halmashauri na anaamini kila kitu kitakuwa sawa.