Mambo ya msingi uchambuzi na mjadala bajeti ijayo

Thursday March 28 2019

 

Kila Aprili hadi Juni, kila mwaka ni msimu wa bajeti Tanzania. Bunge hujadili bajeti mjadala unaotanguliwa na vikao vya kamati mbalimbali.

Pamoja na mambo mengine, Bunge linakutana kujadili na kupitisha bajeti za wizara kwanza kabla ya bajeti kuu kusomwa, kujadiliwa na kupitishwa ili kuanza kutumika mwaka mpya wa fedha unapoanza.

Ni muhimu kwa wananchi wote, kufuatilia, kuchambua na kuchangia mijadala ya bajeti. Japo kuna majukwaa kadha wa kadha yanayoweza kutumika katika kufanya hivi, kwa wawakilishi wa wananchi, jukwaa kuu ni Bunge la bajeti.

Wengine huwa na midahalo katika vyombo vya habari. Ni muhimu kuelewa mambo ya msingi katika uchambuzi na mijadala ya bajeti kwa mwaka wa fedha 2019/20 ili kuongeza nafasi ya bajeti ya Sh33.1 trilioni kufanikiwa.

Uchambuzi wa mapato

Bajeti ni makadirio ya mapato na matumizi kwa kipindi fulani maalumu. Bajeti ya Serikali ni makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka mmoja wa fedha.

Advertisement

Serikali huwasilisha makadirio ya mapato yake kwa kuonyesha jinsi fedha zitakazotoka katika vyanzo mbalimbali zitakavyotumika kugharamia bidhaa na huduma za umma.

Bajeti ya mwaka wa fedha 2019/20 inakadiriwa kuwa Sh33.1 trilioni. Haina maana kuwa fedha hizi zipo na zinasubiriwa kutumika. Ni fedha ambazo Serikali inategemea kuzikusanya kutoka vyanzo vyake mbalimbali.

Vipo vyanzo vya ndani vya mapato na vya nje pia. Kuna vya kodi na visivyo vya kodi. Ni muhimu kuchambua kila chanzo kimekuwa kikiingiza kiasi gani katika miaka ya karibuni na kwa mwaka ujao wa fedha kinatarajiwa kuingiza kiasi gani na kwa nini.

Ni muhimu kuuliza kama kiasi kinachooingizwa kina akisi uhalisia wa uwezo wa chanzo husika. Kama hapana ni kwa nini na nini kifanyike kwa mwaka huu wa fedha ili kuboresha mapato.

Ni muhimu kuchambua na kujadili uwekezaji unafanywa ili kuboresha kila chanzo cha mapato ya Serikali Kuu hata za mitaa. Ni muhimu kuwekeza vizuri kusudi mavuno pia yawe mazuri. Itapendeza pia kama tafakuri itafanywa kupata ubunifu wa vyanzo vipya vya mapato.

Pia ni muhimu kuuliza kila chanzo cha mapato kinachangia kiasi gani katika mapato yote. Na ni muhimu kuuliza na kujadili hatua zinazotumika kuongeza mapato bila kuleta athari kwa walipaji na vyanzo husika kama vile kampuni.

Matumizi Muhimu

Jumla kuu ya mapato kwa mwaka 2019/20 inategemewa kuwa Sh33.1 trilioni ambayo yataelekezwa katika matumizi mbalimbali. Ni muhimu kujadili na kuchambua matumizi ya maendeleo.

Ni muhimu kujua uwiano wa matumizi haya ya aina mbili katika sekta mbalimbali. Hii ni kwa sababu matumizi haya hutegemeana. Yakizidi au kupungua sana upande mmoja sio afya kiuchumi.

Kupanga matumizi katika bajeti ni jambo moja na kutekeleza yaliyopangwa ni jambo jingine. Ni lazima chambuzi na mijadala ya bajeti iulize kama matumizi hayakutekelezwa kama ilivyopangwa, kwa nini na athari zake ni nini.

Muhimu zaidi ni kujiuliza na kupata jibu la nini kinatakiwa kufanywa ili kurekebisha hali ya bajeti isiyotekelezwa. Pia ni muhimu kuchambua na kujadili mwendendo wa matumizi umekuwaje sio tu kwa mwaka wa fedha unaokwisha bali pia kwa miaka kadhaa nyuma.

Masuala Mengineyo

Uchambuzi na mijadala ya bajeti inakuwa mizuri pale mambo mengine yanapozingatiwa. Kusudi kuwa na mijadala yenye tija ni lazima kusoma na kuielewa bajeti vizuri sio bajeti pendekezwa ya mwaka 2019/20 bali za miaka kadhaa iliyopita.

Hii ni muhimu kwa ajili ya kulinganisha mambo. Kwa kifupi, ni lazima kusoma angalau bajeti ya mwaka mmoja wa nyuma. Pale penye tatizo kimapato au matumizi ni lazima kutafuta maelezo ya kina yenye kuonyesha viini na suluhu ya matatizo.

Inapendeza mijadala ikionyesha ubunifu na mambo mapya. Hii ni pamoja na kutoa mapendekezo ya vyanzo vipya vya mapato na kuepuka matumizi makubwa kuliko mapato, kupunguza utegemezi kwa mikopo na misaada.

Advertisement