Vipo vigezo rahisi kukusaidia kupimaji ukuaji biashara yako

Muktasari:

  • Ili biashara iwe na tija unayoikusudia ni lazima ikue kadri muda unavyoenda. Kama unatamani kupima ukuaji wa biashara yako basi tambua kuna vigezo muhimu vinavyoweza kukurahisishia kufanikisha lengo hilo.

Kati ya malengo ya kuanzisha biashara ni kuona inakua baada ya muda fulani. Ukuaji wa biashara ni muhimu kwani pia huchangia kuimarika kwa uchumi wa Taifa.

Pamoja na ukweli kwamba dhana ya ukuaji biashara si ngeni, si watu wote wanavifahamu vigezo vya kupima ukuaji biashara. Kutofahamu vigezo hivi kunaweza kusababisha kutokuwapo kwa ukuaji mzuri wa biashara na faida zitokanazo na ukuaji huu.

Kati ya vigezo unavyoweza kuvitumia ni kuangalia mauzo unayofanya. Biashara zipo kwa ajili ya kuuuza bidhaa na huduma mbalimbali. Mauzo ni mojawapo ya viashiria vinavyojumuisha kiasi cha mali inayouzwa na fedha zinazotokana na mauzo haya katika muda maalumu. Muda huu huweza kuwa saa, siku, juma, mwezi hadi mwaka.

Katika hali ya kawaida mauzo yanapoongezeka ni kiashiria kuwa kuna ukuaji wa biashara husika. Kinyume chake ni kweli pia. Mauzo yakipungua huashiria kutokufanya vizuri kwa biashara husika.

Kigezo kingine muhimu cha kupima ukuaji wa biashara ni faida. Lengo kuu la biashara ni kutengeneza faida. Kati ya vigezo vya kupima kama biashara inafanya vizuri au laa ni kuangalia mwenendo wa faida katika biashara husika.

Kinachotakiwa ni kujua jinsi faida ya biashara inavyobadilika tangu kuanza hadi wakati upimaji wa ukuaji unapofanywa. Ni muhimu kuelewa kuwa faida inaweza kukua, kushuka au kubaki vilevile ilivyokua. Kwa anayetaka biashara ikuwe lazima kuongeza faida au mauzo.

Mwenendo wa mtaji ni kigezo kingine muhimu. Biashara huanza kwa mtaji fulani kutoka vyanzo mbalimbali, inaweza kuwa fedha za mwanzilishi wa biashara husika, mkopo, ruzuku kutoka sehemu tofauti na urejeshaji wa faida katika biashara husika.

Yeyote anayeanzisha biashara ana lengo la kuhakikisha pamoja na mambo mengine mtaji unakua baada ya muda. Ukuaji wa biashara unahusishwa na ongezeko la mtaji. Mtaji unapoongezeka kwa kawaida kunakuwapo ukuaji wa biashara. Kinyume chake ni kweli pia.

Unaweza kuangalia ongezeko la wateja pia. Kati ya mambo ya msingi katika biashara yoyote ni kuwa na wateja ambao ndio hununua bidhaa au huduma zinazouzwa na biashara husika. Kwa kawaida biashara huanza na wateja wachache.

Wateja hawa huweza kukua kadri muda unavyokwenda. Ukuaji wa wateja ni kati ya viashiria vya ukuaji wa biashara. Hii ni kwa kuwa biashara inayofanya vizuri huvutia wateja wapya na kuwabakiza waliopo.

Kwa kawaida wateja wanavyoongezeka ndivyo biashara inavyokua. Hii ni kwa sababu wateja wanapoongezeka tegemeo ni kuwa mauzo na faida vinaongezeka pia. Ongezeko la mauzo na faida ni afya kwa ukuaji wa biashara.

Kufungua matawi ni jambo jingine unaloweza kulitumia kutathmini kukua kwa biashara yako. Biashara nyingi huanza kwa kuwa na tawi moja kisha huongezeka na kukua hadi kuwa na matawi mengi. Haya yanaweza kuwa eneo moja kama vile mkoa, wilaya, kata au kijiji.

Pia huweza kuwa yametawanyika sehemu mbalimbali ndani hata nje ya nchi. Ongezeko la matawi ya biashara baada ya muda fulani tangu kuanzishwa ni kati ya ishara kuwa biashara husika inakua.

Katika hali ya kawaida, ongezeko la matawi linaendana na ongezeko la wateja, idadi ya bidhaa na huduma zinazouzwa, fedha zitokanazo na mauzo na faida itokanayo na miamala husika.

Vilevile, ukuaji wa biashara unaweza kupimwa kwa kutizama idadi na ubora wa bidhaa na huduma zinazozalishwa katika biashara husika. Kwa kawaida biashara huanza kwa kuzalisha au kuuza bidhaa na huduma chache.

Kati ya sababu za kuwa na uchache wa bidhaa au huduma ni kuwa na mtaji mdogo au kujaribu soko kabla ya kuongeza aina na wingi wa bidhaa na huduma. Ongezeko la wingi na aina za bidhaa na huduma katika biashara ni kiashiria kuwa biashara inakua.

Hii ni kwa sababu pamoja na mambo mengine, ili kuongeza wingi na aina ya bidhaa na huduma inahitaji biashara kuwa na mtaji zaidi.

Ushauri

Ni vizuri kwa wafanyabiashara kutambua na kuvifanyia kazi vigezo vya ukuaji wa biashara na kujipima kwa kila kigezo kuhakikisha kuwa miradi yao inashamiri maeneo yote.

Kigezo kimoja kati ya vilivyoorodheshwa hapo juu hakitoshi kutoa picha ya jumla ya ukuaji wa biashara. Kwa kawaida inabidi kutizama vigezo mbalimbali ili kupata picha ya jumla.

Hata hivyo, ukuaji wa biashara kwa kila kigezo ni muhimu. Ili kupima ukuaji vizuri, haina budi kuwa na utaratibu wa kutunza kumbukumbu kuanzia biashara inapoanzishwa.

Wakati wa kupima ukuaji, ni suala la kutafuta tofauti kati ya hali ilivyokuwa wakati wa uanzishaji biashara au wakati upimaji ulivyofanywa mara ya mwisho na hali halisi wakati wa upimaji.