Ikipatikana nishati mbadala ya kupikia matumizi ya mkaa yatakwisha

Wakazi wa wilayani Magu jijini Mwanza wakiwa na Mkaa eneo la Kisesa wakitafuta wateja. Picha na Michael Jamson

Muktasari:

  • Kutokana na mjadala ulioendeshwa na Kampuni ya Mwananchi Communications (MCL) kuhusu matumizi ya mkaa nchini, mtaalamu wa mazingira ambaye kwa sasa ni mwenyekiti w abode ya wakurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania (Tafori), Dk Felician Kilahama ameandika maoni yake.

Awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kupata fursa ya kubadirishana mawazo juu ya umuhimu wa mkaa na athari zake kwa mazingira.

Vilevile, niipongezea menejimenti za Mwananchi Communications Limited kwa kubuni na kuandaa mjadala juu ya biashara ya mkaa na mazingira ambao ulirushwa mubashara kupititia televisheni ya ITV na Radio One kuanzia saa 3:00 mpaka 5:00 usiku wa tarehe 7 Februari. Hongereni sana.

Namshukuru Januari Makamba, waziri wa nchi, ofisi ya makamu wa Rais-mazingira kwa takwimu na maelezo mazuri. Kwa kufanya hivyo aliweka msingi mzuri wa majadiliano kwa wachangiaji waliofuata.

Mkaa ndicho chanzo kikuu cha nishati ya kupikia katika miji mingi nchini. Zipo sababu kadhaa ukiwamo urahisi wa kuupata kutokana na kusambazwa maeneo mengi hata zisizofikika kirahisi ambako baisikeli, pikipiki na mikokoteni hutumika kuubeba.

Gharama za mkaa pia ni rafiki kwa mtumiaji wengi ukilinganisha na umeme, gesi au mkaa mbadala (briquettes). Mathani, kununua mkaa kwa matumizi ya kila siku ni njia rahisi kumudu maisha kuliko kununua gesi ya kupikia au kulipa gharama za umeme kwani fedha nyingi huhitajika ambazo mtumiaji hana.

Inakuwa rahisi kubangaiza ukapata kiasi kidogo cha fedha ukilinganisha na Sh15,000 au zaidi na zote zikaishia kununua gesi.

Kwa mtazamo wetu inaonekana mkaa ni chanzo rahisi cha nishati ya kupikia na chanzo cha mapato kwaWatanzania waishio mjini hata vijijini wanaojishughulisha na uchomaji, upakiaji, usafirishaji, wapakuaji, usambazaji pamoja na uuzaji rejareja.

Kulingana na mazingira ya biashara ya mkaa yalivyo, inaonekana ni nishati nafuu ingawa kiuhalisia siyo kweli. Makamba alijitahidi kulifafanua hili kwamba, iwapo miti inayotumika kutengeneza mkaa, ingelipiwa ipasavyo mkaa usingekuwa nafuu ukilinganisha na vyanzo vingine vya nishati.

Maeneo mengi ya misitu ya asili hayana usimamizi wa kutosha kiasi kwamba kila anayetaka huingia na kujihudumia. Hivyo wachoma mkaa wanakata miti yenye thamani kubwa mfano mininga, mipingo au miyombo bila kuigharamia.

Serikali inatoza kiasi kidogo cha fedha kwa kila gunia la mkaa ambacho hakilingani na thamani ya miti iliyotumika kuuchoma. Iwapo miti ingelipiwa sawasawa tusingethubutu kusema ni nafuu maana ungepambana na vyanzo vingine vya nishati.

Sheria ya misitu inakataza kukata miti ya asili bila kibali na hairuhusiwi kuvuna miti kwenye eneo ambalo halina mpango wa usimamizi. Kwa misingi hiyo, mkaa mwingi unaotumika nchini ni biashara haramu.

Wadau wanafanya hivyo wakijua usimamizi wa misitu ya aslili ni hafifu. Watumishi wa umma kupitia TFS na Serikali za Mitaa ni wachache sana na vitendea kazi havitoshelezi mahitaji. Hivyo wengi wanakata miti bila kuulizwa wala kudhibitiwa kwa mujibu wa sheria na udhaifu huu unachangia kuuona mkaa kama bidhaa nafuu kuipata na kuitumia.

Matumizi ya mkaa yanaongezeka kila mwaka kutokana na ongezeko kubwa la watu mjini. Mwaka 2012 zaidi ya tani milioni 2.3 za mkaa zenye thamani ya Sh980 bilioni zikiwanufaisha watu 225,000. Ni biashara kubwa lakini ni njia kuu ya kuharibu misitu ya asili na kuhatarisha mazingira.

Utaalam na teknolojia ya kutengeneza mkaa ni duni na husababisha miti mingi kukatwa kupata kiasi kidogo tu. Tani moja ya mkaa hutokana na tani 10 mpaka 12 za miti.

Benki ya Dunia mwaka 2009 ilikadiria biashara ya mkaa iliingiza Dola 650 millioni za Marekani. Sehemu kubwa ya biashara hiyo ikifanyika jijini Dar es Salaam na kwenye miji mikubwa kama Mwanza, Arusha, Mbeya.

Hata hivyo ukusanyaji tozo za mkaa una changamoto nyingi kuanzia unakochomewa hata kusafirishwa kusikozingatia sheria. Kwa bahati mbaya masuala ya mkaa, kama chanzo muhimu cha nishati ya kupikia hayajapewa msukumo wa kutosha kitaifa.

Watunga sera na wafanya uamuzi huona mkaa mwingi pembeni mwa barabara na hakuna anayelalamika wala kuchukua hatua.

Kimsingi, Wizara ya Nishati imejielekeza zaidi kuendeleza vyanzo vingine vya nishati kama vile umeme, gesi na mafuta. Ni muhimu kuwapo sera inayoeleweka kuhusu nishati ya kupikia na huu ni wajibu wa Wizara ya Nishati.

Kazi kuu ya wataalaam wa misitu ni kutunza na kusimamia rasilimalimisitu ili bidhaa zake mfano mbao, magogo, kuni, mkaa na nguzo ziwe endelevu bila kuathiri uwezo wa misitu kuhifadhi mazingira na kuendeleza ikolojia kama vile kutunza vyanzo vya maji.

Vilevile, miti iliyokomaa ndiyo inatakiwa kuvunwa lakini kwa sababu uwezo wa TFS na Serikali za Mitaa kudhibiti hali hiyo ni mdogo, misitu ya asili mingi haina usimamizi wa kutosha na watu wanavuna miti bila na kukata miti michanga.

Isitoshe miti inayotengeneza mkaa hailipiwi hivyo kusababisha mkaa uonekane wa gharama nafuu ukilinganisha na vyanzo vingine vya nishati. Gharama halisi za mkaa zikijumlisha kulipia thamani ya miti ipasavyo, zitaufanya usiwe wa bei nafuu kama tunavyofiria.

Mwisho nashauri watunga sera na wafanya uamuzi waone upatikanaji nishati ya kupikia kama ni jukumu la Wizara ya Nishati. Iwepo sera na utaratibu wa kisheria pamoja na usimamizi madhubuti katika Wizara ya Nishati ili uwajibikaji juu ya nishati ya kupikia uwe wa uhakika.

Pili, mamlaka za kusimamia misitu kama TFS, Serikali za Mitaa na idara ya misitu ziwajibike kusimamia utekelezaji wa sera na sheria za misitu kwa kuzuia kukata miti michanga na kuhakikisha rasilimalimisitu inanufaisha Taifa na mkaa ukiwa ni zao endelevu.

Usimamizi wa misitu uimarishwe sana ili yeyote atakayevuna afuate utaratibu. Matumizi ya mkaa liwe ni jukumu la mamlaka zinazohusika na masuala ya nishati kama Ewura.

Mwandishi ni mtaalamu na mdau wa mazingira wa mazingira ambaye kwa sasa ni mwenyekiti wa bodi ya Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania (Tafori). Kwa maoni na ushauri, anapatikana kwa namba [email protected].