Breaking News

Mitizamo ya kiuchumi kuhusu kuporomoka kwa Shilingi

Thursday March 7 2019

 

By Profesa Honest Ngowi

Kati ya mijadala ya uchumi na biashara iliyoibuka hivi karibuni nchini ni kuporomoka kwa thamani ya Shilingi ikilinganishwa na Dola ya Marekani.

Kuporomoka huku kunapimwa kwa kutizama viwango vya kubadilisha Dola moja kwa Shillingi na kinyume chake. Kwa baadhi ya maduka ya kubadili fedha za kigeni, Dola moja imeuzwa kwa zaidi ya Sh2,400 ikipanda kutoka Sh2,230 siku za karibuni.

Kutokana na mabadiliko hayo ndani ya muda mfupi, ipo mitizamo mbalimbali kuhusu sababu na athari za Shilingi kuporomoka na muhimu zaidi suluhu yake.

Ni vyema kufahamu mambo ya msingi linapozungumziwa suala la thamani ya sarafu yoyote. Shilingi inakuwa imara dhidi ya sarafu za nje pale tunapotumia Shilingi chache kupata sarafu moja ya nje kama vile Dola.

Kwa kadiri tunavyotumia Shilingi nyingi zaidi kupata sarafu moja ya nje ndivyo thamani ya Shilingi inavyoporomoka. Kwa ujumla, uimara wa Shilingi unategemea wingi wa Dola na fedha nyingine za kigeni sokoni. Zinapokuwa nyingi Shilingi inaimarika.

Dola zinapatikana kwa kuuza nje bidhaa na huduma, kupata watalii kutoka nje, misaada na mikopo, uwekezaji kutoka nje na fedha zinazotumwa na Watanzania waishio nje.

Advertisement

Mauzo, ununuzi nje

Sababu kuu ya upungufu wa Dola sokoni sasa hivi inaonekana ni kutouzwa korosho nje ya nchi. Kwa kutofanya hivyo basi Dola hazikuingia sokoni kama kawaida. Kumekuwapo hoja ya upungufu wa watalii kwa sababu sio msimu wake.

Inaweza kuwa imechangia bali kwa kiasi kidogo. Hii ni kwa sababu misimu mingine isiyo ya utalii siku za nyuma Shilingi haikupoteza thamani kwa kiasi kikubwa kama sasa. Kufungwa kwa maduka ya kubadili fedha za kigeni kunaweza kuchangia uhaba wa Dola hivyo kushuka kwa Shilingi.

Kutokana na ujenzi wa uchumi, uhitaji mkubwa wa Dola unaweza kuwa umechangia Shilingi kuporomoka. Uhitaji huu unaweza kusababishwa na ununuzi mwingi na mkubwa wa bidhaa au huduma kutoka nje ya nchi.

Ununuzi huu yaweza kuwa ni unaofanywa katika miradi mikubwa kama vile ya ujenzi wa miundombinu. Uhitaji mwingine ni ulipaji wa deni la Taifa…linapolipwa kwa Dola hupunguza kiasi cha sarafu hiyo kwenye mzunguko. Uhitaji mkubwa wa Dola na ununuzi mkubwa kutoka nje husababisha Shilingi kuwa dhaifu.

Kupanda kwa Dola kunawanufaisha watu na taasisi zinazolipwa kwa sarafu hiyo lakini zikitumia kwa Shilingi. Pia huwanufaisha wenye akiba za Dola benki. Bidhaa na huduma kutoka Tanzania zinazouzwa nje huwa na bei ndogo zaidi kwa Dola hivyo wauzaji nje ya nchi huuza zaidi.

Wanaopoteza katika suala la kushuka kwa thamani ya Shilingi ni wale ambao matumizi yao yanahusiana na Dola wakati vipato vyao vipo katika Shilingi. Bidhaa na huduma kutoka nje huwa ghali kuliko kawaida.

Suluhu

Ipo mitizamo na mijadala mingi kuhusu namna ya kutoka hapa tulipokwama. Huu ni mjadala muhimu kwa nchi. Kati ya maoni yaliyopo ni kutumia akiba ya fedha za kigeni kuimarisha Shilingi. Hii hufanywa kwa Benki Kuu kuingiza sehemu ya akiba hii katika maduka ya fedha za kigeni.

Kimsingi hii ni hatua ya muda mfupi. Sio endelevu na haitatui tatizo la msingi la uhaba wa Dola sokoni. Pia akiba hii haitakiwi ‘kuchezewa’. Akiba ya fedha za kigeni huwekwa ili kukidhi ununuzi kutoka nje kwa muda fulani ikitokea sababu yeyote ile fedha za kigeni haziingii nchini.

Hata hivyo kwa muda mfupi Benki Kuu inaweza kuingilia soko ili mporomoko wa Shilingi usiende nje ya uwezo wa kuudhibiti.

Kwa muda wa kati na mrefu ni lazima kupata suluhu endelevu. Suluhu hii ni kuongeza kiasi cha Dola sokoni kupitia mwingiliao huru wa nguvu za soko. Hii ni pamoja na kuwepo na mazingira rafiki na ya kuvutia kuingiza Dola nchini.

Haya ni pamoja na mazngira ya kisheria, kisera na kiudhibiti. Haya ni mazingira muhimu kuwezesha uzalishaji na uuzaji wa bidhaa na huduma nje ya nchi, kuvutia watalii kutoka nje, au kuvutia na kubakiza wawekezaji toka nje.

Mazingira hayo pia ni mazuri kuvutia misaada na mikopo kutoka nje, kuvutia fedha za Watanzania waishio nje ya nchi kuja nchini na kuzalisha ndani ya nchi baadhi ya bidhaa na huduma zinazonunuliwa kutoka nje ya nchi.

Advertisement