Maamuzi ya mawaziri yanavyoiyumbisha sekta ya elimu

Tuesday May 7 2019

 

By Tumaini Msowoya, Mwananchi [email protected]

Kati ya mambo yanayotajwa kuwa yanachangia kuathiri elimu ni hatua ya kila waziri mwenye dhamana ya elimu anapoingia madarakani kuwa na uhuru wa kuweka kando mipango ya awali na kuanza mingine.

Historia ya sekta ya elimu nchini ni shahidi wa hili. Kwa mfano, miaka ya 2000- 2005, aliyewahi kuwa waziri wa elimu Joseph Mungai alifanya mabadiliko yaliyowashtua wadau wengi wa elimu. Alifuta masomo ya biashara, kilimo na ufundi, huku akiyaunganisha masomo ya Fizikia, Kemia kuwa somo moja.

Hakutosheka, kwa mamlaka aliyonayo alifaniki pia kufuta mashindano ya michezo

Aidha, wakati wa Serikali ya utawala wa nne, aliyekuwa Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, alianzisha mfumo wa ufaulu wa GPA badala ya madaraja kwa wahitimu wa kidato cha nne ambao baadaye mrithi wake, Profesa Joyce Ndalichako alikuja kuukosoa.

Ni wakati huohuo wa awamu ya nne, mfumo wa ufaulu ukabadilishwa kwa waziri kufuta daraja sifuri kwa wahitimu wa kidato cha nne na kuliita daraja la tano.

Aidha, ni ndani ya utawala huohuo, Sera mpya ya elimu ikaandaliwa huku ikielekeza kuwa elimu ya msingi itaishia darasa la sita badala ya miaka saba,

Advertisement

Hata hivyo, utaratibu huu baadaye ukawekwa kapuni na Serikali ya Awamu ya Tano.

Mwenendo huu ndio uliomuibua Mbunge wa Nzega, Hussein Bashe aliwahi kuwasilisha hoja binafsi bungeni akitaka Bunge liunde sheria ya kuundwa kwa tume ya kitaalamu, ili kufanya mapitio ya elimu na kubana matamko ya kisiasa kwenye sekta hiyo.

Wadau wa elimu waliozungumza na Mwananchi wanapinga mawaziri kuwa na uhuru wa kubadilisha mambo, kwa sababu sio tu yanawachanganya wananchi bali yanayumbisha elimu nchini.

Wanashauri kuwepo kwa chombo kitakachosimamia elimu ili maamuzi yoyote yanayofanywa yawe na eneo moja la kuchakatwa na kufanyiwa kazi kisera na kiutekelezaji.

Mratibu mstaafu wa Mtandao wa Elimu Tanzania (Ten/Met), Cathleen Sekwao anasema ni kweli kwamba mawaziri wana uhuru wa kubadilisha mambo wizarani na kwamba wakati mwingine wanafanya hivyo bila ya kuwapo kwa utafiti.

Anasema kabla ya mabadiliko ni muhimu kufanya utafiti utakaoleta majibu ya faida ya kile kinachofanyika kwenye elimu.

INAENDELEA UK 14

INATOKA UK 13

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Profesa Benson Bana anasema hatua ya kila waziri kuja na mipango au matamko yake, inapotosha mfumo wa elimu.

Anasema kwa kawaida waziri wa elimu anapokabidhiwa wizara hiyo huwa anafanya kazi kulingana na sera ya elimu iliyopo, maelekezo ya Rais hasa kwa yale aliyoahidi katika kampeni pamoja na dira ya maendeleo ya kipindi husika.

Mfano katika utawala wa 2015-2020 Rais John Magufuli ameamua kutekeleza sera ya elimu bila malipo, hivyo kumlazimisha waziri kufanyia kazi mpango huo.

Mwenyekiti wa Kigoda cha Mwalimu Nyerere kupitia taluma za Kiswahili, Profesa Aldin Mutembei anasema haamini kama waziri anaweza badilisha mfumo wa elimu bila kushirikisha ngazi mbalimbali kwenye uongozi wake.

“Sasa kama ataweza kujiamulia mwenyewe hilo ni tatizo lakini ninavyojua maamuzi hayafikiwi hivyo kuna washauri na wataalamu mbalimbali wanahusika, sio rahisi kubadilisha ghafla lazima kuwe na mchakato unaoweza kuchukua muda,” anasema Profesa.

Mkurugenzi wa Shirika la Furaha Pamoja Foundation, John Paul anasema inawezekana kuwa na sera ya elimu isiyoingiliwa na maamuzi mengine ambayo lazima iwe inabadilishwa kulingana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia.Anasema hata suala la mawaziri kuja na mipango yao linaweza kutatuliwa kupitia sera ambayo itaonyesha mamlaka zao zinaishia wapi.

“Wakati mwingine yanaweza kufanyika maamuzi sahihi kabisa lakini yakiwa ya kukurupuka bila kupitia kwenye sera ni hatari, kwa sababu hayatotekelezwa atakapokuja waziri mwingine,” anasisitiza.

Akitolea mfano, amesema zamani wanafunzi walikuwa wakifanya mtihani wa hesabu kwa kuonyesha njia na kutoa jibu, lakini baadaye wakaanza kupewa mtihani wa kuchagua.

“Hili nalo halikuwa jema kwa sababu msahihishaji hawezi kujua kama mwanafunzi huyu anauelewa au amekisia tu. Njia inaweza kufanya mtu ajue uelewa wa mtoto badala ya kuchagua,” anaeleza.

Sera imara ni muhimu

Profesa Bana anashauri kuwepo kwa sera mwafaka ya elimu ambayo kama itabadilishwa iwe ni kwa sababu ya mabadiliko ya sayansi na teknolojia au mahitaji halisi ila sio kwa sababu ya matakwa ya waziri husika.

“Malengo ya elimu duniani yabaki palepale, elimu lazima ije kutatua changamoto za kijamii hivyo inapaswa kumuandaa kijana kwa sababu hiyo. Hatuwezi kuongoza wizara kwa matamko, matamko kama kufuta michezo ndiyo ambayo hatuyapendi,” anasisitiza.

Kwa upande wake, Profesa Mutembei anasema kama angepewa nafasi kushauri angejikita kwenye lugha ya kufundishia kwa sababu sera ya elimu iliyopo sasa imetaja lugha mbili lakini haijaeleza kivipi.

“Tumefikia hatua ambapo tunaweza kutumia Kiswahili kama lugha ya msingi ya kufundishia, lakini sera ya mwaka 2014 haijasema kivipi, zichanganywe darasani? Bado kuko kimya hapo,” anasema.

Advertisement