Machungu ya mwalimu Mbilinyi ndani ya darasa la wanafunzi 342

Wednesday July 3 2019

 

By Juma Mtanda, Mwananchi [email protected]

Mpango wa elimu bure umewavutia wazazi wengi. Wale walioshindwa kusomesha watoto kwa hofu ya ada na michango, sasa wana ahueni. Watoto wao wapo shuleni.

Bila shaka hawa ndio walioongeza takwimu za uandikishaji wanafunzi wa darasa la saba kutoka watoto 1,568,378 mwaka 2015 hadi 2,120,667 mwaka mmoja baadaye.

Hata hivyo, mpango huo unapopambwa na takwimu za ongezeko la wanafunzi ambalo ni mafanikio ya kutia moyo, kwa upande mwingine mpango huo umeibua changamoto kubwa ya uhaba wa vyumba vya madarasa vinavyoweza kuwapokea wanafunzi hao.

Moja ya shule zenye changamoto hii ni Shule ya Msingi Msowelo iliyopo mkoani Morogoro. Katika shule hiyo wilayani Kilosa, wanafunzi 342 wanasoma katika darasa moja.

Hawa ni wanafunzi wa darasa la kwanza ambao kwa idadi yao walipaswa kugawanywa katika madarasa yasiyopungua saba kwa uwiano wa kila darasa kuwa na wanafunzi 45.

Kilio cha mwalimu wa darasa

Advertisement

Mwalimu Elizabeth Mbilinyi anayefundisha darasa hilo, anasema kwa zaidi ya miezi mitano maisha ndani ya darasa hilo hayamithiliki. Ana mzigo mkubwa wa kupitia madaftari 342, huku akikiri kuwa kazi hiyo ni muhali kwake.

“Mwalimu anapomfundisha mtoto ni jukumu lake kuangalia daftari la mwanafunzi kama kazi aliyoitoa ameifanya kwa usahihi na wapi amekosea na idadi hiyo ya watoto 342 katika darasa moja inaniwia vigumu kutekeleza majukumu yangu.”anasema na kuongeza kuwa amekuwa akikosa hata pa kukanyaga mkuu darasani kwa sababu ya wingi huo wa wanafunzi.

Huenda machungu anayopitia Mbilinyi yatapungua ifikapo Julai, wakati mpango wa kuwagawa wanafunzi hao katika mikondo miwili utakapoanza.

Wanafunzi wasimulia mateso

Hassan Jumanne anayesoma darasa hilo anasema: “Darasa letu lina matatizo mengi ikiwamo kugeuza goti kuwa meza ya kuegemezea daftari wakati wa kuandika masomo yanayotolewa na mwalimu wetu Mbilinyi.”

Anaongeza kusema kuwa mwalimu aliyepo ni mmoja na kazi anazowapa hushindwa kuzisahihisha kwa sababu ya wingi wao.

Hassan anaungwa mkono na mwenzake Mariam Ahmad anayesema:“Madarasa yapo machache na tunaandikia chini sakafuni kutokana na uchache wa madawati na inafikia kipindi madaftari yetu mwalimu hasahihishi kutokana na mwalimu kuelemewa na kazi

Uongozi wa shule

Mwalimu Mkuu wa shule hii ambayo idadi ya wanafunzi kwa kila darasa haipungui 120, Noel Chiselema anasema kwa sasa wanajipanga kuongeza vyumba vya madarasa na madawati wakishirikiana na wazazi na Serikali.

Anasema kuwa shule hiyo ina upungufu mkubwa wa walimu, vyumba vya madarasa na madawati kwani madawati yaliyopo ni 231 lakini idadi hiyo hailingani na wanafunzi 1692 waliopo shuleni. Madarasa yaliyopo sasa ni saba, yakiwamo mawili yanayojengwa.

“Shule yetu ina jumla ya wanafunzi 1692 na darasa lenye wanafunzi wachache ni darasa la tano ambalo lina wanafunzi 123 na darasa la kwanza ndio lililo na wanafunzi wengi zaidi’’ anasema huku akiishukuru benki ya NMB kwa kuwapa msaada wa madawati 70.

Maendeleo ya taaluma

Ikigubikwa na changamoto hizo tete, hali ya taaluma kwa mujibu wa Chiselema inatia moyo. Kwa mfano, kati ya wanafunzi 131 waliomaliza darasa la saba mwaka 2018, wanafunzi 105 walichaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza. Mwaka 2017 wanafunzi 52 kati ya 82 walichaguliwa kujiunga na sekondari.

Kauli ya uongozi wa wilaya

Akizungumza kwa niaba ya uongozi wa wilaya, Ofisa Mipango wa Wilaya ya Kilosa, Francis Kaunda anasema serikali ya wilaya inatambua kuwapo kwa changamoto katika utoaji wa huduma za jamii hasa elimu na afya na tayari wameanza mikakati ya kukabiliana nazo. ikiwamo kuwahimiza wazazi kuchangia wa vyumba vya madarasa.

Advertisement