Uhaba wa maabara unavyozitesa shule za sekondari-1

Upungufu wa maabara za sayansi katika shule za sekondari nchini umeendelea kuwa changamoto katika ufaulu wa wanafunzi wa masomo hayo.

Hii inaathiri upatikanaji wa wanafaunzi waliofanya vizuri katika masomo hayo hivyo kuendelea kuonyesha alama nyekundu juu ya upatikanaji wa wataalamu wa masomo ya sayansi pamoja na walimu wa masomo hayo, hasa katika kipindi hiki cha mabadiliko makubwa ya sayansi na teknolojia na uchumi wa viwanda tunaoutegemea.

Licha ya juhudi za Serikali kuonyesha juhudi kubwa katika kukabiliana na tatizo hilo kwa kuongeza miundombinu ya maabara lakini bado tatizo lipo.

Kwa mujibu wa Tamisemi katika mwaka wa fedha 2018/19 Serikali ilijenga maabara 165 za masomo ya sayansi katika shule mbalimbali nchini.

Serikali inataka kila shule inayofundisha masomo ya sayansi kuwa na maabara tatu za masomo ya Fizikia, Kemia na Baiolojia.

Licha ya jitihada hizo za Serikali, takwimu za elimu za elimu msingi (BEST) mwaka 2017 zilionyesha kulikuwa na upungufu wa asilimia 42.7 za maabara katika shule zote nchini.

Takwimu hizo zilionyesha kwa mwaka 2017 shule za sekondari nchini zilikuwa na jumla ya maabara 8,258 za masomo ya sayansi, ukilinganisha na mahitaji ya maabara 14,420 sawa na upungufu wa maabara 6,162.

Maabara za Fizikia

Uchambuzi wa takwimu unaonyesha, kati ya masomo yote somo la Fizikia ndilo lililokuwa na uhaba mkubwa zaidi wa asilimia 55.2, ikiwa ina maana kuwa zaidi ya nusu ya shule zote za Serikali nchini zina upungufu wa maabara za fizikia.

Mwaka 2013 hali ilikuwa mbaya zaidi kwa kuwa na upungufu wa asilimia 76.4.

Mwaka 2017 kulikuwa na maabara 2,151 katika shule za sekondari nchini, mahitaji yalikuwa 4,797. Hali hii ilionyesha upungufu wa maabara 2,646.

Hata hivyo, wilaya 18 kati ya 184 zilizorodheshwa zilikuwa na upungufu uliozidi asilimia 50.

Hali ilikuwa mbaya zaidi wilayani Lushoto mkoani Tanga ambapo kulikuwa na upungufu wa asilimia 92.2. Takwimu hizo zilionyesha maabara zilizokuwepo ni 15 pekee wakati mahitaji yakiwa ni 62 sawa na upungufu wa maabara 47.

Wilaya ya Rombo mkoani Kilimanjaro ilikuwa na upungufu wa asilimia 76.5 sawa sawa na maabara 39. Zilizokuwepo ni 12 pekee wakati uhitaji ulikuwa ni 51.

Dodoma mjini ndiyo iliyofuatia kwa na upungufu wa asilimia 72.5, upungufu ulikuwa ni 37 wakati maabara zilizokuwepo ni 19 pekee ukilinganisha na mahitaji ya 56.

Wilaya zisizokuwa na upungufu

Hali ni tofauti Mwanza mjini ambapo kulikuwa na ziada ya asilimia 21.1 ya maabara, hii ni sawa na maabara nne. Mahitaji yalikuwa 52 wakati zilizokuwepo ni 56.

Maabara za Baiolojia

Hadi mwaka 2017 takwimu za BEST zilionyesha kulikuwa na upungufu wa asilimia 43.6 ya maabara za Baiolojia katika shule za sekondari nchini ikiwa ni sawa na maabara 2,093 ukilinganisha na mahitaji ya jumla ya maabara 4,796.

Hali hii ilikuwa ni afadhali ukilinganisha na mwaka 2013 ambapo kulikuwa upungufu wa asilimia 76.4 wa maabara za Baiolojia.

Upungufu kwa wilaya

Wilaya 13 pekee kati ya 184 zilizoorodheshwa ndizo ambazo shule zake zilikuwa na upungufu wa zaidi ya asilimia 50 kwa maabara za somo hilo.

Shule za Wilaya ya Lushoto mkoani Tanga ndizo zilizokuwa na upungufu mkubwa zaidi wa asilimia 90.9. Kulikuwa na maabara 12 pekee kati ya maabara 62 zilizohitajika sawa na upungufu wa maabara 50.

Wilaya iliyofuata ni Dodoma mjini ambayo ilikuwa na upungufu wa asilimia 65.5. Wilaya hii ilikuwa na maabara 19 kati ya 55 zilizohitajika sawa na upungufu wa maabara 36.

Iliyofuata ilikuwa Rombo ya Kilimanjaro iliyokuwa na upungufu wa asilimia 60. Zilizokuwepo zilikuwa 16 wakati mahitaji yakiwa ni 49 na upungufu ni maabara 33.

Wilaya zisizokuwa na upungufu

Hali ni tofauti katika shule za Mwanza mjini ambapo kulikuwa na ziada ya asilimia 16 ya maabara. Wilaya hiyo ilikua na jumla ya maabara 54 ukilinganisha uhitaji wa maabara 51 pekee.

Wilaya nyingine ni Buchosa iliyokuwa na ziada ya maabara moja. Kulikuwa na jumla ya maabara 20 ukilinganisha na uhitaji wa maabara 19.

Maabara za Kemia

Kati ya masomo yote ya sayansi ni somo la Kemia pekee lilikuwa na upungufu wenye afadhali ukilinganisha na masomo mengine. Shule zenye maabara ya kemia zilihitaji maabara 4,827 wati zilizokuwepo mpaka wakati huo ni 2,909.

Hii ni sawa na upungufu wa asilimia 39.7 ikiwa ni jumla ya maabara 1,918. Hata hivyo, ni wilaya nne pekee zilizokuwa na upungufu wa zaidi ya asilimia 50. Hali ilikuwa mbaya zaidi mwaka 2013 ambapo upungufu ulikua ni asilimia 72.7.

Wilaya ya Lushoto ndiyo ilikua na upungufu wa asilimia 75 ikiwa ndio upungufu mkubwa zaidi ukilinganisha na wilaya nyingine. Shule za wilaya hii zilikuwa na jumla ya maabara 17 pekee ukilinganisha na maabara 62 zinazohitajika sawa na upungufu wa maabara 45.

Iliyofuata ilikuwa ni Rombo ya Kilimanjaro iliyokuwa na upungufu wa asilimia 60, ambapo kulikuwa na maabara 24 kati ya 60. Nayo Dodoma manispaa ilikuwa na upungufu wa asilimia 58.3 sawa na jumla ya maabara 35 huku mahitaji yakiwa ni maabara 55.

Jumanne ijayo tutaangalia upungufu wa jumla wa wilaya, mikoa na nchi nzima na kauli ya Serikali