Upungufu vyumba vya maabara unavyozitesa shule za sekondari-2

Tuesday May 14 2019

 

By Halili Letea, Mwananchi [email protected]

Takwimu za Elimu Msingi (BEST) zilionyesha asilimia 44.3 ya wilaya/ manispaa zilikua na upungufu wa maabara wa zaidi ya asilimia 50. Hii ni sawa na wilaya 82 kati ya 184 zilizoorodheshwa.

Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga ndiyo iliyokuwa na upungufu wa asilimia 92.6 ya maabara ikiwa ndiyo kubwa zaidi nchini. Wilaya hii ilikuwa na maabara sita pekee ukilinganisha na mahitaji ya maabara 81; huu ni upungufu wa maabara 75.

Wilaya iliyofuata ni Geita iliyokuwa na upungufu wa asilimia 92.0. Hadi mwaka 2017 kulikuwa na upungufu wa maabara 81 ukilinganisha na mahitaji. Zilizokuwepo ni saba pekee.

Nyingine ilikuwa ni Singida iliyokuwa na upungufu wa asilimia 91.6. Kulikuwa na maabara saba pekee kati ya 83 zilizohitajika.

Wilaya nyingine ni Nkasi iliyokuwa na upungufu wa asilimia (90.9), Nyang’wale (90.0), Handeni (90.0), Hanang’ (89.9) na Chemba (88.4).

Wilaya zisizokuwa na upungufu

Advertisement

Hali ni tofauti katika shule za sekondari wilaya ya Mwanza mjini iliyokuwa na ziada ya maabara 11. Wilaya hii ilikuwa na uhitaji wa maabara 156 pekee lakini zilizokuwepo ni 167.

Wilaya nyingine ni Buchosa ya Mwanza ambayo ilikuwa na ziada ya maabara tatu wakati mahitaji yalikuwa ni maabara 57 lakini zilizokuwepo ni 60.

Wilaya ya Makambako ilikua na ziada ya maabara mbili ukilinganisha na mahitaji ya maabara 45.

Hata hivyo, kulikuwa na wilaya tano ambazo mahitaji ya maabara katika shule zake yalilingana na uwepo. Wilaya hizo ni Mlele, Kyela, Momba, Kaliua, na Kilindi.

Uchambuzi kimikoa

Uchambuzi wa mikoa ulibaini kuwa mikoa 11 kati ya 26 ilikuwa na upungufu wa maabara uliozidi asilimia 50. Mikoa 12 ilikuwa na upungufu wa asilimia zaidi ya 10 na mingine mitatu pekee ndiyo ilikuwa na upungufu wa chini ya asilimia kumi.

Mkoa wa Singida ulikuwa na upungufu wa asilimia 79.0 na ndiyo mkoa ambao shule zake zilikuwa na upungufu mkubwa zaidi. Mahitaji ya maabara katika mkoa huo yalikuwa ni 486 wakati zilizokuwapo ni 102.

Mkoa uliofuata ni Dodoma ambao hadi mwaka 2017 ulikuwa na upungufu wa asilimia 76.1 wa maabara sawa na jumla ya maabara 502. Mahitaji yalikuwa ni 660 wakati zilizokuwepo ni 158.

Mkoa mwingine ni Rukwa uliokuwa na upungufu wa asilimia 74.4 wakati mahitaji yalikuwa ni maabara 270. Zilizokuwapo ni 69 sawa na upungufu wa maabara 201.

Mikoa iliyokuwa na afadhali

Ni mikoa mitatu pekee nchini ilikuwa na upungufu wa maabara usiozidi asilimia kumi.

Dar es Salaam ilikuwa na upungufu wa asilimia 8.7 pekee ukiwa ndiyo mkoa uliokuwa na afadhali zaidi. Hadi mwaka 2017 kulikuwa na upungufu wa maabara 85 pekee katika shule za sekondari mkoa huo. Mahitaji yalikua ni maabara 975 ukilinganisha na zilizokuwepo 890.

Mkoa uliofuata ni Katavi uliokuwa na upungufu wa asilimia 8.8 sawa na maabara kumi. Mahitaji yalikuwa maabara 114 na zilizokuwepo ni 104.

Mkoa mwingine ni Songwe uliokuwa na upungufu wa asilimia 9.0 sawa na maabara 29. Mkoa huo ulikuwa na maabara 295 ulikinganisha na mahitaji ya maabara 324.

Uchambuzi wa jumla

Mpaka kufikia mwaka 2017 kulikuwa na upungufu wa asilimia 42.7 wa maabara katika shule za sekondari nchini. Mahitaji yalikuwa ni jumla ya maabara 14,420 wakati zilizokuwepo mpaka kipindi hicho ni 8,258.

Hali ilikuwa mbaya zaidi kwa shule za sekondari za Serikali ambapo upungufu ulikuwa ni asilimia 51.4 sawa na maabara 5,602 ukilinganisha na uhitaji wa maabara 10,896.

Vilevile kwa shule zote za Serikali na somo moja moja ni somo la Fizikia lililokuwa na upungufu mkubwa zaidi wa maabara 2,150 (asilimia 44.8) ikifuatiwa na Bailojia lililokuwa na upungufu wa maabara 2,093 (asilimia 43.6) na Kemia maabara 1,887 (asilimia 39.3).

Hata hivyo hali hii ilikuwa ni afadhali ukilinganisha na mwaka 2013 ambapo upungufu ulikuwa asilimia 76.4 kwa Bailojia, 72.7 kwa Kemia Fizikia 75.3.

Licha ya kilimo kuajiri zaidi asilimia 75 ya Watanzania na kuwa ndio sekta muhimu zaidi ya uchumi nchini, somo lake lilikuwa na maabara chache zaidi na kuonyesha sio miongoni masomo yaliyopewa kipaumbele.

Serikali inasemaje

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo alilieleza Mwananchi kuwa Serikali inaendelea kuimarisha miundombinu ya maabara kwa shule za sekondari nchini kupitia miradi yake mbalimbali.

“Tumenunua vifaa vya maabara zaidi ya 1,682 vilivyogharimu karibu Sh16 bilioni; hizo zilikuwa ni mradi wa EQUIP II (Education Quality Improvement Programme). Lakini lakini kuna mipango kupitia miradi mingine,” anasema.

Jafo anaongeza kusema kuwa kama jitihada za kuendeleza nguvu za wananchi, Serikali imetoa Sh29.9 bilioni kwa shule zote nchini ili kuendeleza majengo ya maabara ambayo hayajakamilika.

Advertisement