Upungufu vyumba vya maabara unavyozitesa shule za sekondari nchini -5

Tuesday June 11 2019

 

Mwanza mjini

Halmashauri ya jiji la Mwanza ni ya tatu kitaifa kwa idadi kubwa ya wanafunzi, hii ni kwa mujibu wa takwimu za Baraza la Mitihani la Taifa (Necta-2018).

Pia, kwa Takwimu za Elimu Msingi (BEST) mwaka 2017, halmashauri hiyo ilikuwa inaongoza kwa kuwa na jumla ya maabara 167, kati ya hizo 57 ni za somo la kemia, 54 baiolojia huku 56 zikiwa za fizikia.

Kati ya maabara hizo, 90 ni kwa ajili ya shule za umma 30 kwa maana ya maabara tatu katika kila shule, huku nyingine zikiwa ni za shule binafsi na taasisi mbalimbali.

Mwananchi imefanya mahojiano na kuzuru baadhi ya shule jijini humo na kubaini kwamba shule zenye maabara za kujitosheleza ni chini ya 10 ingawa mikakati ya kuendelea na ukamilishaji inaendelea.

Mkuu wa Shule ya Sekondari Igoma jijini Mwanza, Bregery Nyakyuma anasema shule hiyo ina maabara tatu ambazo hazina vifaa. Alisema maabara hizo kwa sasa zinatumika kama vyumba vya madarasa kutokana na idadi kubwa ya wanafunzi.

Advertisement

“Tumetenga chumba kimoja kufanyia shughuli za maabara ingawa hatuna vifaa,” anasema.

Kwa upande wake Pastory Mazula ambaye ni Mkuu wa Shule ya Sekondari Buhongwa, anasema kwa bahati nzuri shule hiyo ina maabara tatu na zote zinafanya kazi. Anasema kutokana na nguvu kazi za wazazi na wananchi, wameweza kuongeza maabara nyingine kwa ajili ya mafunzo ya kompyuta.

“Sisi tuna jumla ya maabara nne na kwa kweli zimeweza kutusaidia sana kwenye masomo ya sayansi ikilinganishwa na kipindi cha nyuma.” anasema.

Ofisa elimu jijini Mwanza, Venance Babukege anasema maabara zote zipo katika hatua nzuri kimajengo, ingawa kuna baadhi zinaendelea kufanyiwa ukarabati maalumu.

Anasema jiji hilo lina jumla ya shule 54 za sekodari na kati ya hizo 30 ni za umma huku 24 zikiwa za taasisi mbalimbali na binafsi.

Anafafanua kwamba shule hizo za umma 30 zina walimu 312 wa masomo ya sayansi ambao hawakidhi idadi kubwa ya wananfunzi waliochagua mchepuo wa sayansi.

Anasema kwamba jiji hilo linapaswa kuwa na walimu 677 wa masomo ya sayansi kwa mujibu wa mtaala.

Mmoja kati ya wanafunzi waliofanya mtihani wa kidato cha nne mwaka 2018 kutoka Shule ya Sekondari Igoma, Baraka Mwita anasema kushindwa kufanya masomo ya sayansi kwa vitendo kulichangia kufeli kwake, kidao cha nne.

“Pale hatuna vitendea kazi ni majengo tu. Ina maana asilimia kubwa ya kazi zilizohitaji vitendo hatukuweza kufanya hivyo,” anasema Baraka.

kauli sawa na hiyo ilitolewa na Elikana Charles, ambaye alifanya mtihani wake kutoka shule ya Fumagila jijini humo ambapo anasema siku ya mtihani, ilikuwa ndiyo mara yake ya kwanza kuona baadhi ya vifaa ikiwamo, bunsen burner.

Hata hivyo, Maria James ambaye alimaliza kidato cha sita katika shule ya sekondari Pamba mwaka 2017, anasema kipindi hicho walikuwa na upungufu mdogo wa baadhi ya vitendea kazi lakini kwa sasa shule hiyo inakidhi vigezo vyote vya maabara.

“Nashukuru maana kipindi nasoma pale Pamba sekondari maabara ya kemia tu ndiyo ilikuwa haina baadhi ya kemikali ambazo zilikuwa ni muhimu, walimu walilazimika kuazima hasa wakati wa mtihani.”

Ofisa elimu (taaluma) wa halmashauri ya Mwanza, Malima Chisumu alifafanua kwamba jiji hilo lilipata nafasi ya 24 kati ya halmashauri 173 nchini kwenye ufaulu wa matokeo ya kidato cha nne mwaka 2018, na ya 17 kati ya 195 mwaka 2017.

Katika hatua nyingine, halmashauri ya jiji la Mwanza ilishika nafasi ya 20 kati ya halmashauri 184 mwaka 2018, kidato cha pili.

Alizitaja baadhi ya shule ambazo zimekamilika kwa kuwa na maabara ni Nsumba, Nganza, Mwanza, Pamba na Buhongwa.

“Unajua ili maabara ikamilike ni lazima iwe na vifaa vyote vya kutekeleza kazi kwa vitendo, lakini pia kuwa na mifumo ya gesi inayofanya kazi. Kwa sasa maabara zote zimekamilika kwa majengo ila ukarabati kwa ajili ya kuboresha unaendelea,” anasema Chisumu.

Wadau wa elimu watoa ushauri

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Ubunifu Tanzania (EIT), Benjamin Mkonya anasema vipaumbele vya Serikali vipo kwenye kuboresha miundombinu na kushauri kuwa kueleukea uchumi wa kati wa viwanda, ni lazima iangalie uhitaji wa wataalamu katika kipindi hicho.

“Tunategemea kutakua na uhitaji mkubwa wa wataalamu ikiwamo wahandisi, madaktari na wataalamu wa kilimo, lakini je tumewaandaa?” alihoji.

Mkonya alifafanua kuwa kuna haja kwa Serikali kuandaa mazingira ya kuuendea uchumi wa kati kwa kuboresha miundominu ya kujifunzia masomo ya sayansi.

“Ningeishauri Serikali ifute ufadhili wa masomo ya sanaa kwa wanafunzi wa masomo hayo na fedha hizo ziende kuboresha miundominu ya masomo ya sayansi.

“Kuna haja ya kuboresha mazingira kwa wafanyakazi ikiwamo walimu wa masomo ya sayansi kwa kuwapa mishahara tofauti na wale wa masomo ya sanaa, kuwawekea mazimgira mazuri ya kufanyia kazi wataalamu mbalimbali kama madaktari na maofisa kilimo ili kuwavutia,” anasema.

Kwa upande wake Ofisa Elimu wa Sekondari Wilaya ya Lushoto, Ndabazi Paul anasema maabara za masomo ya sayansi sio majengo bali ni kuwa na vifaa vya kutosha. “Unaweza ukawa na jengo moja tu lakini ukiwa na vifaa vya kutosha unabadilisha tu pale unapotaka kufanya somo fulani.”

Naye Meneja Program wa Mtandao wa Elimu Tanzania (TENMET), Nicodemus Eatlawe anasema upungufu wa maabara unamaanisha kuna uwezekano mkubwa wa wanafunzi kufanya vibaya kwenye mitihani yao kwani asilimia 50 ya matokeo ya mitihani hiyo ni masomo ya vitendo.

Eatlawe anasema tatizo lililopo ni vipaumbele vya Serikali kwa kipindi hiki na kueleza kuna haja ya wazazi na jamii kushirikiana ili kuhakikisha kuna mabadiliko ya vipaumbele. “Katika jamii ndiko kuliko na awapigakura, kama watakua pamoja na wakashirikiana kwa kutaja vipaumbele vyao lazima viongozi wao (wabunge) watabadilika”.

Advertisement