USHAURI WA DAKTARI: Fanya haya kusaidia moyo wako kufanya kazi vizuri

Ipo mikakati ambayo mwanadamu akiifanya huchangia afya njema ya moyo hivyo kufanya kazi yake ya kusukuma damu kwa ufanisi na muda mrefu bila kupata magonjwa ya moyo.

Jambo la kwanza ni kuepuka matumizi ya vyakula vya mafuta mabaya (saturated fats) badala yake watu watumie mafuta yatokanayo na mimea pamoja na kula nyama nyeupe ikiwamo samaki.

Ikumbukwe matumizi ya muda mrefu ya mafuta yatokanayo na wanyama huchochea kuongezeka lehemu mbaya mwilini ambayo husababisha uharibifu wa mishipa inayopeleka damu katika misuli ya moyo.

Tumia samaki zaidi kwani wana mafuta yajulikanayo kama Omega 3 ambayo ni mazuri kwa afya ya moyo.

Ulaji wa matunda yaliyoiva au ya njano na mboga mboga za kijani ni vyakula ambavyo vimesheheni virutubisho na madini mbalimbali ambavyo husaidia kuwa na msukumo imara wa damu na kuimarisha afya ya moyo.

Punguza kiasi cha sukari unachotumia kwa siku, wataalam wa afya ya moyo duniani wanapendekeza kwa mwanaume kutozidisha vijiko tisa vya sukari kwa siku na kwa mwanamke vijiko sita kwa siku. Kutekeleza jambo hili unahitajika kuepuka kutumia vyakula vyenye sukari nyingi ikiwamo soda, pipi, chokleti na juisi za kutengenezwa viwandani.

Vyakula vyenye sukari vinachangia kupata unene uliopitiliza hivyo kuupa moyo mzigo mkubwa wa kiutendaji.

Dhibiti kiasi cha chumvi unachotumia wakati wa ulaji wa vyakula hasa nyama choma, chipsi na vyakula vya sherehe. Ulaji wa chumvi unasababisha mwili kujaribu kudhibiti kiasi kilichozidi cha chumvi kwa kubakisha maji mengi mwilini.

Hali hii inasababisha ujazo wa damu kuongezeka mwilini hivyo moyo huhitajika kudunda kwa nguvu ili kutoa msukumo mkubwa katika mzunguko wa damu.

Hali hii inapodumu kwa muda mrefu inaweza kusababisha madhara ikiwamo shinikizo la juu la damu na moyo kushindwa kufanya kazi.

Kiwango cha chumvi ambacho ni salama kinachopendekezwa na wataalam wa afya duniani ni miligramu 1,500 kwa siku ambacho ni karibia na nusu kijiko cha chai na isizidi miligramu 2,300.

Ni vizuri kujenga utamaduni wa kupata elimu sahihi ya lishe kwa kusoma vijarida na kusikiliza vipindi mbalimbali vya afya ili kujua zaidi vyakula salama ambavyo ni rafiki wa afya ya moyo.

Kufanya mazoezi mepesi yaani (aerobic exercise) mara kwa mara, mazoezi haya husaidia kuchoma mafuta yaliyorundikana mwilini na pia kusaidia kuwa na mpangilio mzuri wa mapigo ya moyo na mzunguko wa damu.

Mazoezi mepesi ni pamoja na matembezi ya umbali mrefu, kukimbia kidogo kidogo, kuogelea, kupanda ngazi, kufanya shughuli ndogo ndogo, kuendesha baiskeli, kucheza muziki au michezo kama tenisi.

Mazoezi haya ndiyo yanasifika kuleta afya njema ya moyo hivyo kuwafanya watu kuishi kwa muda mrefu bila matatizo ya kiafya, hii ni kutokana na kukuepusha kupata unene uliopitiliza.

Epuka uvutaji sigara kwani kemikali zilizomo ndani yake husababisha mishipa ya damu kunyauka na kuwa myembamba. Hali hii ikitokea inakuwa ni vigumu kwa moyo kubeba damu kwenda katika moyo na ogani nyingine.

Madhara haya pia humpata mvutaji wa pili ambaye ni yule anayekaa karibu na wavutaji au kuwepo katika mazingira hayo hivyo ni vizuri kukaa mbali na moshi wa sigara.

Itaendelea Jumapili ijayo...