Joyce, mama wa nyumbani sasa anamiliki Shule ya msingi na chekechea

Dar es Salaam. Jitihada za wanawake kupambana na umaskini zimewafanya waamini wanaweza ikiwa wataamua kufanya kazi kwa bidii na kutokubali utegemezi.

Wanaamini kuwezeshwa kunawafanya wabweteke wakisubiri kufanyiwa kila kitu kwa maana ya kuwa tegemezi.

Joyce Ngalula, Mkurugenzi wa Shule ya chekechea na msingi ya Lusasaro, iliyopo Tabata Kisukuru jijini Dar es Salaam anasema uamuzi ndilo jambo la kwanza kumfanya mwanamke apige hatua. “Kwanza unaamua, baadaye unathubutu kisha unaweka bidii kwenye kile ulichoamua kufanya, utaona mafanikio makubwa,” anasema na kuongeza, “nafurahi kwa sababu nilipitia hatua hizo na leo shule niliyoanzisha imeshika namba moja kwa manispaa ya Ilala, ndoto inatimia polepole.”

Miaka 10 iliyopita, Joyce alikuwa mama wa nyumbani. Kazi yake kubwa ilikuwa kazi za nyumbani, kupika, kufua, kuandaa chakula na kuwasimamia watoto wake.

“Si rahisi kuitwa mama wa nyumbani japo kuna kazi unafanya ila hilo jina linakufanya uonekane umebweteka au tegemezi. Jina lilinifanya niamue kupiga hatua,” anasema Joyce.

Ilikuwaje?

Joyce anasema baada ya kufanya maamuzi ya kubadili jina aliamua kuwekeza kwenye elimu, akiamini ataweza kusaidia watoto wengi kufikia ndoto zao kimaisha.

“Unajua wakati huo wanangu walikuwa wanasoma Uganda, baba yao aliwapeleka na kurejea. Niliwaza sana, ni nini kinawafanya wakasome huko? Kwani siwezi kuwekeza kwenye elimu nisaidiane na Serikali ili tuboreshe elimu yetu?” Alisema Joyce na kuongeza, “nilitamani sana watoto wapate elimu bora, elimu itakayowasaidia kupambana na changamoto zinazowazunguka.”

Anasema akaamua kumweleza mume wake, Amos Lugata juu ya ndoto yake ya kuwekeza kwenye elimu. “Nashukuru Mungu mume wangu alinipa sapoti kubwa kuliko nilivyodhani, nikagundua kama nisingeamua kusema ndoto yangu ningeendelea kuwa mama wa nyumbani tu,” anasema Joyce.

Anasema aliamua kuanzisha shule ya chekechea akaiita jina la Lusasaro lililounganisha herufi za awali za majina ya watoto wake wanne; Luis, Samweli, Salome na Rivival-Omega.

“Nilifanya hivyo ili nao wajue ni wamiliki na wanapaswa kuhakikisha ndoto za mama yao Mzinatimia,” anasema.

Anasema wanafunzi wa chekechea walipofika muda wa kuanza darasa la kwanza, alianzisha shule ya msingi.

“Nilishangaa mambo yanaenda kama yalivyopangwa, niliajiri walimu wazuri na madarasa yaliendelea kuongezeka,” anasema Joyce.

Mwaka 2015, shule yake ilipata usajili na kuwawafanya wazazi wengi waiamini hivyo kupokea idadi kubwa ya wanafunzi.

“Nilitamani watoto wapewe elimu bora, si elimu ya kukaririshwa tu darasani hapana, wajifunze maisha na mazingira.

Aliongeza kuwa anatamani kuona watoto wanapomaliza masomo wanakuwa na uwezo wa kujitegemea.

Mwaka 2017 shule hiyo ilishika nafasi ya pili kwa kundi la wanafunzi chini ya 40, katika mtihani wa darasa la saba. “Nilifurahi kuona taaluma ya shule inakua, mwaka 2018 tukawa watano mwaka huu tumekuwa wa kwanza kwa manispaa ya Ilala, najipa moyo, lengo langu linaendelea kufanikiwa,” anasema.

Kinachompatia nguvu

Joyce anasema kama asingeamua kusimama angebaki kuwa mama wa nyumbani jambo ambalo, wanawake wanapaswa kulikataa. “Ukishakuwa tegemezi, akili inalala, wanawake ni viongozi na wanaweza kuongoza na kuwekeza kwenye sekta nyingi kama afya, elimu, biashara na nyingine lakini kwanza utoke na usimame,” anasema mkurugenzi huyo wa Lusasaro.

Anasema kwa sasa akilala mawazo yanapanuka, hawazi watoto tu anawaza walimu na wafanyakazi wengine. Anafikiria afanye nini ili ainue zaidi kiwango cha elimu shuleni kwake.

Nidhamu

Anasema wapo wanawake wengi waliothubutu kusimama lakini wakaanguka tena baada ya kulewa mafanikio.

“Nidhamu ndio siri kubwa ya mafanikio ya mwanamke, ukiwaheshimu unaowaongoza ni rahisi kufika mbali, nawaheshimu sana wafanyakazi wenzangu hapa shuleni na naishi nao vizuri,” anasema.

Anasema amebaki kuwa mkurugenzi akisimamia mambo yote ya msingi kwenye shule yake hususani maendeleo ya kielimu.

Joyce anasema aliamua kuanzisha utoaji wa motisha kwa walimu wanaofanya kazi kwa bidii.

“Kwa mfano mwalimu anayetoa A nyingi kwenye mtihani wa kitaifa wa darasa la nne na saba anapewa Sh100,000 kwa kila A.

“Motisha hiyo imewaongezea ari ya kufanya kazi na wanashindana kufaulisha wanafunzi,” anasema.

Anasema pia wanatumia mbinu za kuwazoesha wanafunzi mitihani, hususani watakaofanya ya taifa hupewa mitihani iliyopita na kuifanya mara kwa mara.

Mafanikio ya wanawake

Mkurugenzi wa Shirika la Pamoja Foundation, Paul John anasema wanawake wakifanya kazi kwa bidii na kufanikiwa kimaisha, watapunguza ukatili wa kijinsia dhidi yao.

“Zamani kina mama walikaa nyumbani kwa sababu walionekana hawawezi lolote zaidi ya kuzaa na kulea watoto. Hapo wanaume waliwaendesha walivyotaka na wao walivumilia kwa sababu ya utegemezi,” anasema John.

Anasema mwanamke akiwa na kipato cha uhakika atakuwa na maamuzi kuhusu maisha na ataiongoza vizuri familia yake.

“Wanaume wanapenda wake zao wawasaidie kwenye maisha kutokana na ugumu uliopo, utegemezi hutengeneza hasira na mwisho ukatili kwenye nyumba nyingi,” anasema John.

Anasema kujitambua, kuamua, kujiamini na kuthubutu ni hatua muhimu kwa kila mwanamke kufikia ndoto za mafanikio yake.

Joyce anasema ndoto zake ni kuendelea kuwekeza kwenye elimu kwa kujenga shule ya sekondari kuanzia kidato cha kwanza mpaka cha sita.

“Bado ndoto yangu haijaisha naamini nitafika niendako, namshukuru sana Mungu kwa hatua hii na namuomba anisaidie nifike hatua kubwa zaidi,” anasema Joyce.

Wito wake kwa wanawake

“Wito wangu kwa wanawake wenzangu tuamke, tusimame, tukimbie na tufanye kazi kwa bidii ili tuondoe utegemezi kwenye jamii yetu,” anasema Joyce.

Anasema utu wa mwanamke kwenye jamii utaendelea kuheshimishwa na kuthaminiwa ikiwa hataogopa mazingira yanayomzunguka ikiwamo vikwazo vya asili, badala yake atayatumia kusonga mbele.