USHAURI WA DAKTARI: Wanaume wasitumie dawa za kuongeza nguvu za kiume kiholela

Zipo dawa zinazotangazwa kuongeza nguvu za kiume na baadhi ya waganga wa kienyeji na wa tiba mbadala ambao huweka namba zao katika mitandaoni, vipeperushi na mabango.

Pia zipo dawa za kitaalamu za mahospitalini zinazoandikwa au kutolewa na madaktari baada ya kutathimini usalama wake kwa mgonjwa.

Ikumbukwe kuwa si sahihi kutumia dawa yoyote kiholela bila kuandikiwa na daktari na ni kosa kwa mtu asiye mtaalamu wa afya kuandika au kutoa dawa.

Dawa ambazo zinatumika mahospitalini huwa ni zile ambazo zimethibitika kuwa ni salama na mamlaka husika.

Kwa mtaani dawa maarufu kama inavyoitwa vumbi la kongo ndiyo inayoonekana kutangazwa mitandaoni lakini hakuna taarifa za vyombo husika inayoeleza kuwa ni salama.

Kwa kawaida dawa za hospitalini zimewekewa utaratibu wa kutolewa kwa wagonjwa kwa kuandikiwa na daktari wa kawaida au bingwa wa magonjwa ya ndani.

Ndiyo maana baadhi ya maduka ya dawa muhimu na maduka ya dawa hugoma kuzitoa bila fomu maalum ya kuzichukulia inayotambulika.

Utaratibu huu unafanyika ili kuhakikisha kuwa mgonjwa anapata dawa ambazo ni salama na zinazomsaidia katika kiwango (dose) ambayo hakitamletea madhara.

Daktari hufanya uchunguzi wa maradhi mbalimbali ikiwamo magonjwa ya moyo na mishipa ya damu ndiyo hukuandikia dawa hizo.

Hii ni kwa sababu dawa hizo hazitolewi kwa wenye matatizo haya na zikitumika kiholela mgonjwa anaweza kupoteza maisha.

Vile vile lazima daktari ajiridhishe kama kweli mgonjwa ana uimara wa kuipokea dawa hiyo pasipo kupata tatizo lolote la kiafya.

Pia huchunguza chanzo kilichosababisha na hali ya kiafya kiujumla ndipo hufanya maamuzi ya kutoa dawa sahihi.

Moja ya dawa ambayo imeshika umaarufu nje na ndani ya nchi ni viagra ambayo kwa lugha ya kitabibu hujulikana kama sildenafil.

Ugunduzi wake kwa kiasi fulani ulileta mapinduzi hasa katika kukabiliana na tatizo la upungufu wa nguvu za kiume. Pia zipo dawa zingine ambazo utendaji wake unafanana na viagra zilizotumiwa miaka ya nyuma ikiwamo cialis, levitra, staxyn na strenda.

Dawa hizi hufanya kazi ya kusaidia mishipa damu kutanuka zaidi na kuruhusu damu nyingi kutiririka katika misuli ya uume na hatimaye kupata nguvu. Haishauriwi kutumiwa na mtu ambaye kwa kipindi cha miezi sita amekuwa akiugua magonjwa ikiwamo kiharusi, magonjwa ya moyo, shambulizi la moyo (heart attack) na tatizo la mapigo ya moyo.

Pia, wenye shinikizo la damu la kupanda au kushuka na mwenye kupata maumivu ya kifua wakati wa kujamiiana. Mjulishe daktari anayekutibu kama una matatizo haya ili aweze kukupa matibabu salama au kukubadilishia dawa ambayo itakuwa salama.

Unaweza ukashauriwa kutumia lakini vizuri kufahamu madhara madogo dogo unayoweza kuyapata ikiwamo kuumwa kichwa, kuhisi joto kupanda, kupata shida ya kuona kwa muda na kuishiwa nguvu.

Pia unaweza kuumwa tumbo, kupata mafua ya kukwama, maumivu ya mgongo na kutosikia vizuri.