TUONGEE KIUME: Mambo 5 ya kuzingatia kabla hujaingia baa

Monday September 23 2019

 

By Kelvin Kagambo

Inawezekana zaidi ya nusu ya wanaume wote duniani wanaokunywa pombe wanafurahia zaidi kunywea baa. Hivyo huenda ni muhimu pia kufahamu mambo ya kuzingatia kabla hujaanza safari ya kwenda huko ili usijutie pesa na muda wako. Anza kwa kuzingatia haya matano.

Sababu ya kwenda baa

Kila mtu huingia huko akiwa na sababu tofauti na mwenzake. Wapo wanaokwenda kupunguza msongo wa mawazo, wanaokwenda kujipumzisha baada ya mizunguko ya siku, wanaokwenda kupata fursa mpya za kibiashara, wanaokwenda kusubiri foleni ipungue na ambao wao ni ratiba yao ya kawaida ya kila siku.

Kwa hiyo kabla hujaanza safari jiulize kwa nini nakwenda baa, kisha fanya tathmini ya baa unayotaka kwenda kama inaweza kuwa sehemu nzuri ya kufuata unachokitafuta vinginevyo utajuta.

Daraja la baa

Siyo kwa sababu wewe ni mlevi basi unatosha vigezo kuingia kwenye kila baa, utafeli. Ifahamu baa unayoingia ni ya daraja gani? La juu, la chini au la kati, kisha jitathmini na wewe ni mlevi wa daraja gani.

Advertisement

Kuna baa zinauza bia moja Sh15,000, ukiingia hizo wakati wewe ni wa bia za Sh2,500 unaweza kuagiza, ukanywa kama komba, halafu ukaletewa bili ya ajabu usiamini. Usipokuwa makini unaweza kupewa kazi ya kupanga makreti stoo.

Umbali wa baa hadi nyumbani

Kiuhalisia hakuna mlevi aliyewahi kulewa hata akapasahau nyumbani kwake. Iwe isiwe, walevi wote hufika nyumbani hata baa iwe mbali kiasi gani. Yaani hata mtu anywe hadi azimie, atafika nyumbani hata kwa kubebwa. Kufika ni kufika.

Ila ni vyema zaidi kunywa karibu na nyumbani kwa sababu kadri baa inavyokuwa mbali na nyumbani ndivyo ambavyo mlevi hufika nyumbani na hali mbaya.

Ulishawahi kusikia mtu karudi nyumbani hana chochote, hata nguo. Hayo ni miongoni mwa madhara ya kulewea mbali na nyumbani.

Watu wanagawana kila ulichokuwa nacho huko huko njiani.

Pombe zinakugeuza kuwa nani?

Kila mtu anabadilishwa na pombe kuwa mtu fulani. Kuna wengine wakilewa wanakuwa wanamuziki, wataimbaa weeee mpaka mwisho. Wengine huwa waandishi wa habari, wengine huwa ‘usalama wa taifa’ na zaidi.

Wewe ukilewa unakuwa nani? Hili ni swali muhimu kujiuliza kabla hujaingia baa kwa sababu kwa mfano yawezekana ukilewa unakuwa Mike Tyson, unajisikia kupigana tu na kila mtu. Hii ni bora uende baa zenye ma bodyguard ili hata ukianzisha ugomvi, utatolewa nje na kama kupigwa utapigwa kistaarabu. Ila ukienda kwenye baa za kawaida, ukaanzisha ugomvi, hakutakuwa na kuamulia utapigwa mpaka watu wahakikishe wamekuchomoa meno yote ya barazani. Litafakari hili.

Wanao watakula kesho

Kama unaishi kwa kuamini kesho itajisumbukia hata usifikirie hili swali. Nenda katumbue fedha yote. Ila kama unafahamu kuwa wewe ndiyo nahodha wa familia yako ni muhimu kujiuliza ukiingia leo baa, utatoka na pesa ya kuwanunulia wanao chakula. Liweke kichwani hili.

Advertisement