TUONGEE KIUME: Mkeo anatakiwa afahamu nini kuhusu wewe?

Kuna aina mbili za maisha. Maisha ya hadithi na halisi. Maisha ya hadithi ndio yale unayoambiwa na swahiba wako anayekuelezea jinsi kilimo cha matikiti kinavyolipa.

Anakwambia, ukiwa na milioni tu unalima ekari ya matikiti, ukivuna na kuuza unapata 24 milioni kwa hiyo ukitoa milioni yako ya mtaji, faida ni milioni 23 kwa ekari.

Anakwambia, shamba unapata la kukodi kwa laki tu ukienda kutafuta Kibaha. Kisha mbegu za kutosha kupanda ekari nzima unanunua kwa bei nafuu Kariakoo hata laki haifiki. Ukiajiri kibarua mmoja anakusafishia shamba lote na kukupandia kabisa kwa 2000 tu kwa siku, pesa inayobaki unakodi mashine ya kumwagilia, dawa ya kuulia wadudu, pesa ya mtu wa kukuangalizia shamba ukiwa mjini na kibarua wa kukusaidia kuvuna.

Ukimsikiliza ukaingia huko, ndiyo sasa unakuwa umekwenda kwenye maisha halisi. Sasa utafuata maelekezo yake halafu baada ya miezi sita ukisimama mbele ya shamba ulilokodi kwa laki, unagundua hakuna hata senti 10 yako inayoweza kurudi.

Maisha ya hadithi ni yale unayosikia watu wakisimulia kwamba mke na mume ni mwili mmoja, mke na mume ni muungano wa juu zaidi ya miungano yote, kwa hiyo mke na mume wanatakiwa kuchangia taarifa, siri, anachokijua mke na mume akijue na anachokijua mume ni cha mke pia. Hayo ndiyo maisha ya hadithi.

Katika maisha halisi unatakiwa kuwa muwazi kwa mkeo, unatakiwa kuwa mkweli, lakini kamwe hautakiwi kumuelezea mkeo kila taarifa kuhusu wewe.

Kwa lugha rahisi ni kwamba wewe ni binadamu, una mambo ambayo huenda hayapendezi mkeo kuyafahamu.

Inawezekana yanapendeza akiyajua, lakini itakusababishia kukosa amani sasa ili kuepusha yote inatakiwa uheshimu faragha yako.

Katika maisha halisi watu wengi wameingia kwenye matatizo kwa sababu ya kuchanganya kati ya kutokuwa wawazi na kutunza faragha. Kuheshimu na kulinda faragha yako haimaanishi kwamba wewe ni msiri bali inamaanisha unajali na kuheshimu uhusiano wenu na hauko tayari kumpoteza mwenza wako.

Fikiria kwa mfano labda kuna kosa uliwahi kumfanyia mke wako nyuma bila yeye kujua. Kosa hili linakunyima amani kila ukilifikiria, unatamani sana kumwambia lakini ukifanya hivyo utahatarisha mapenzi, labda utatengeneza roho ya kisasi kwa mwenzio au utamfanya ashindwe kuendelea kuhimili kuwa na wewe.

Kwa hiyo badala ya kuwa muwazi, unaweza ukatumia akili ya kulifanya hili kosa kuendelea kuwa siri, iwe faragha yako ili ulinde uhusiano.

Kuna taarifa nyingi tu kuhusu wewe mkeo hatakiwi kujua, unatakiwa uchague, kuchuja ya kumpa na utakayokufa nayo kifuani mwako. Mkeo hatakiwi kujua kila kitu kuhusu wewe na familia yako. Ikiwezekana asijue hata mshahara wako.

Ili ndoa zidumu wakati mwingine siyo mara zote wanaume wanapaswa kuishi maisha ya hadithi na faragha kwa pamoja.

Kusema sema kila jambo utakuja kuropoka ambalo kwa mwanamke ni kosa kubwa wakati kwako ni jambo la kawaida.

Ndoa itavunjika oohoo...