KUTOKA LONDON: Neno ‘kuku wa kisasa’ linafundisha maana mbaya , kiafya

Wiki iiliyopita tuliangalia uharibifu wa lugha kupitia wanahabari na walimu. Kuna matumizi yanayobomoa thamani ya lugha kama kusema “fulani yuko katika nchi ya Uingereza” ...

Hapa ni marudio ya nchi na katika ....

Ukishasema Uingereza tayari ni “nchi” si mji. Hivyo “fulani aliye Uingereza” inatosha. Ukishatamka ‘yuko Uingereza’ hakuna haja ya neno katika.

Haya marudio ni mfano wa tatizo. Huonyesha ufinyu wetu wanahabari na watangazaji. ...Kutokana na ama kutoichimba lugha, kuisoma au tu uvivu. Ni pia tatizo la kibiashara. Wengi wetu hulipua kazi kunenepesha kipato.

Kwa vipi?

Baadhi ya wafanyabiashara hawatafurahishwa tukitamka kuwa twaweza kutengeneza fedha bila kuharibu maendeleo ya afya ya jamii.

Miaka kadhaa sasa Tanzania tuna nahau: ‘kuku wa kisasa’ na ‘kuku wa kienyeji’...misemo hii imejenga taswira iliyokuwepo baada ya ukoloni. Miaka ya sitini kuvaa suti za Kizungu ilionekana jambo la kisasa kuliko Kimasai, mathalan.

Wavaaji suti waliitwa Naizesheni (Kenya) au Mastafu (Tanzania).... Naizesheni tokana na “Nice” (Kiingereza) Safi, Zuri, Bora; ilhali, Stafu yaani “Staff member” - wafanyakazi ofisini...ambayo si maneno mabaya, ila yalitumika kunyanyapaa walala hoi.

Ndiyo uongozi wa Tanu na Mwalimu Nyerere ukabatilisha suti za Kizungu na kuunda zisizo na kola shingoni kama sehemu ya ukombozi wa kifikra.

Miaka ya sabini sisi vijana tulianza kuvaa mashati ya vitenge yaliyoitwa Dashiki. Leo Dashiki ni fahari ya mavazi ya Kiafrika. Si maastajabu kama 1970 au 1975.

Tukija 2020, suala la kuku wa kisasa na kuku wa kienyeji limepanda sana ngazi. Limeharibu kabisa vichwa vya vizazi vichanga visivyolinganisha na kuchanganua matukio duniani yanavyoathiri mazingira yetu Afrika.

Tukianza na mazingira. Afrika ni bara lenye vitu asilia, uzuri usiojulikana, imejaza madini na maumbile ya kupendeza. Bado Afrika ina wanyama na vyakula vitamu visivyopatikana kwingine.

Si ajabu yamezuka maradhi ya kutisha kama Ebola na corona. Wenyeji Afrika wanajua nyama gani yafaa au haifai kuliwa... ila walaji Ughaibuni hawajui.

Sasa Wazungu (walioongoza kwa teknolojia), wamegundua kumbe mashine na dawa huharibu afya. Miaka arobaini iliyopita wimbi Ulaya limeng’amua kuwa biashara imebadili sana chakula. Mifugo iliyofugwa kwa umeme na taa bandia haifikii nguvu za jua asilia.

Ndege na wanyama wanaoachwa kutembea huru, kula wadudu, nk wana furaha na ni watamu kuliko wanaodungwa sindano na kuishi vibandani saa 24 wakiteseka na tayari baada ya miezi miwili au pungufu. Matokeo nyama bandia imezua maradhi kem kem. Uzunguni, mathalan wanaume kupoteza mbegu za uzazi. Hata wanawake wanadhurika.

Msomaji kwanini wadhani vuguvugu la kutokula nyama kubwa sana Uzunguni? Ni kutokana na mateso ya wanyama. Vuguvugu jipya la kuwalea wanyama na ndege katika mazingira asilia (kama wanavyopaswa, yaani ‘Organic’ ) limeshadidi Ughaibuni kiasi biashara mpya ya kiafya inastawi.

Kuku, bata na wanyama wengine wanaokuzwa kwa furaha huitwa ‘free range’ na wanapendwa zaidi. Ni hawa ndege na wanyama wasiodhuru mwili, ndiyo tunaowaita ‘wa kienyeji’ na waliodungwa sindano na dawa ili wakue haraka (na kutuua upesi) ndiyo tumewabatiza jina la wa kisasa...

Asiye jua hudhani usasa ni maendeleo.Kumbe? Afya za kizazi kipya zinaathirika Afrika kama ilivyo Uzunguni.