USHAURI WA DAKTARI: Sababu mwanamke kulewa haraka kuliko mwanaume...

Sunday July 7 2019

 

By Dr Chris

Miezi michache iliyopita, shirika la Afya Duniani, (WHO) lilifanya tafiti zake na kuja na hitimisho kuwa, kiwango chochote kile cha kilevi hata kikiwa kidogo kiasi gani, si salama kiafya. Hivyo ni vyema ikaeleweka kuwa unywaji pombe kwa ujumla wake ni hatari kwa afya hata kama ikitumika kwa kiwango kidogo.

WHO pia wamebainisha madhara ya pombe yanatofautiana kulingana na jinsia, yaani kwa kifupi, pombe inawaathiri zaidi wanawake kuliko wanaume.

Je? Matumizi ya pombe na ulevi kwa ujumla wake upoje baina ya jinsia hizi mbili?

Ukweli ni kwamba kwa tafiti yangu ndogo niliyoifanya kupitia idara ya afya ya akili, nimegundua kuwa, wanaume ndio wanaoongoza kuwa na idadi kubwa sana ya ulevi kwa ujumla tukiachana na pombe.

Linapokuja suala la unywaji wa pombe, japo pia wanaume wanaongoza takribani kwa asilimia 70 tofauti na wanawake, lakini kuna ishara kuwa idadi ya wanawake huenda ikalingana na wanaume katika unywaji wa pombe hapo miaka kadhaa ijayo kutokana na sababu mbalimbali za kijamii zinazowapelekea watu kuangukia kwenye ulevi wa pombe.

Takwimu za sasa zinaonyesha kuwa katika kila kundi la watu 10 wanaokunywa pombe, basi takribani watu watatu hadi wanne kati yao ni wanawake.

Advertisement

Takwimu zinaonyesha dhahiri kuwa bado wanaume ndio wanaoongoza kwa idadi ya ulevi wa pombe tofauti na wanawake, lakini kwa nini wanawake ndio wahanga wakubwa wa pombe kuliko wanaume?

Leo utapata kujua imekaaje hii kisayansi.

Kisayansi kuna sababu nyingi zinazosababisha pombe kumuathiri zaidi mwanamke kuliko mwanaume na baadhi ya sababu hizi ni kama ifuatavyo:

Kwanza kabisa ifahamike kuwa kisayansi, wanawake wana kiwango kidogo cha maji mwilini kuliko wanaume. Tofauti na kimo au uzito, wanawake wana sehemu kubwa ya mafuta (fat) katika miili yao wakati wanaume wana sehemu kubwa ya ujazo wa misuli kwenye miili yao. Mafuta yana mkusanyiko wa asilimia 25 tu ya maji wakati misuli ina mkusanyiko wa asilimia 75 ya maji. Kutokana na dhana hii, wanawake wana kiwango hafifu cha maji mwilini tofauti na wanaume.

Wakati pombe inaponywewa na kuingia mwilini, inachakatwa, na kile kiwango cha maji kinachobaki baada ya kuchujwa kwenye mfumo wa mkojo kinaingia kwenye mzunguko wa damu.

Sasa kwa sababu, wanawake wana kiwango hafifu cha maji cha kuweza kuzimua ile pombe, inaingia kwenye mikondo ya damu na hivyo kusababisha damu inayozunguka mwilini kuwa na uwepo wa kiwango kikubwa cha pombe na hata kusababisha pombe kudumu kwa muda mrefu mwilini tofauti na wanaume.

Lakini pia sababu nyingine, mwilini kwenye mfumo wa chakula, kuna kimeng’enya ambacho kitaalamu kinaitwa “Enzyme Alcohol Dehydrogenase”.

Kimeng’enya hiki ni maalumu kwa ajili ya kuvunja vunja vyakula vyote ambavyo vimeambatana na kiwango chochote kile cha pombe kabla pombe haijaingia kwenye mikondo ya damu.

Kisayansi kimeng’enya hiki ni hafifu na dhaifu zaidi kwa mwanamke kuliko mwanaume, hivyo kusababisha kuruhusu kwa kiwango kikubwa cha pombe kuingia kwenye mikondo ya damu kuliko ile ya mwanaume.

Advertisement