TUONGEE KIUME: Tuoe tabia nzuri au wazuri?

Wanaosema tuoe tabia nzuri, wanadai uzuri ni kitu cha muda, mwanamke mzuri huwa hivyo katika umri fulani pekee, hasa ujana. Kwa hiyo kadri umri unavyosonga ulimbwende nao unapukutika. Hii maana yake ni kwamba kama utaoa kwa sababu ya uzuri, kuna uwezekano mkubwa wa kuichoka ndoa uzuri ukimuisha mwenzio. Lakini tabia, weee! Hizo hata akizeeka zitabaki palepale.

Tena wanakwambia wanawake wazuri hawajui maisha. Kwamba kwa sababu wanafahamu wanavutia macho ya wanaume wengi, basi wanakuwa na kujiamini kulikopitiliza. Maana yake ni anaweza kuwa hata hakusikilizi kwa sababu anaamini hata mkishindwana dakika hii, akitoka nje hatembei hatua tano anapata mwingine.

Na unaambiwa ukioa mwanamke mzuri pia inabidi uwe na nguvu sana ya kulinda ndoa yako kwa sababu wanaume wote duniani tunapenda vitu vizuri, kwa hiyo tutamsumbua sana — atatongozwa kazini, kwenye daladala, sokoni, dereva wa bodaboda na karibu na kila mwanaume atakayepata ukaribu wake. Swali ni Je, ataweza kukwepa mishale yote hiyo? Ukizingatia mingine inatoka kwa watu waliouzidi kila kitu? Wanawake wanaopendwa na wengi mtihani.

Wanaosema tuoe uzuri

Wanakwambia kabla ya kuoa fikiria vitu vingi. Fikiria jinsi utakavyokuwa unamtambulisha mkeo kwa rafiki na ndugu zako. Ukiwa na mwanamke mzuri, wala huhitaji kuongeza sifa wakati wa kumtambulisha, ukisema ‘huyu ndo mke wangu mtarajiwa.’ inatosha. Lakini ikiwa hawa wengine, inabidi uchombeze na sifa zisizoonekana kwa macho kama ‘huyu ndo mke wangu mtarajiwa. Usimuone hivi, anafahamiana na viongozi wengi huyu.”

Pia fikiria jinsi picha zenu za harusi zitakayoonekana. Fikiria watoto mtakaopata watakavyokuwa. Vyote hivi haviwezi kukuumiza kichwa ukiona mwanamke mzuri, utakuwa na amani.

Na ukitoka kibaruani, umeshagombana na bosi, umegombana na wateja, umegombana na konda kwenye daladala, ukirudi nyumbani unatakiwa upate kitulizo. Yaani ukute mwanamke mzuri anakusubiri. Mwanamke ambaye ukimuangalia tu, unasahau magumu yote uliyopitia mchana. Sio unarudi unakutana na kitu yenye ‘sura ya mjomba wake’. Ukiangalia, badala ya kupoza machungu ya siku unajikuta unapandwa na hasira upya hii inaweza kukupa magonjwa ya uzeeni ukiwa bado na umri mdogo sana.

Pia wanauliza kama tabia mbaya ni tatizo, hata wewe una tabia zako mbaya lakini amekubali kuolewa na wewe. Hii maana yake ni kwamba, hakuna mtu mwenye tabia zote nzuri. Kwa hiyo unaweza kuvumilia tabia zake mbaya ukadumu.

Tuoe yupi?

Inawezekana lengo la Mungu kutupa kila mtu roho yake ni kwamba kila mtu aishi maisha anayotaka. Wewe unataka nini? Uzuri wa sura au tabia? Fanya unachoona kinakufaa.

Mwisho wa siku fahamu kwamba uzuri sio kitu halisi, ni fununu tu. Hakuna kipimo cha aidha uzuri wa sura au tabia. Ni mitazamo pekee ndiyo inayoamua kwamba tabia hii au mwonekano huu ni mzuri au mbaya.