Usafishaji upi wa njia ya uzazi ni salama?

Katika maisha ya kila siku si wanawake wote katika jamii wana ufahamu sahihi juu ya usafishaji salama wa njia ya uzazi utakaowakinga na magonjwa ya kina mama ikiwamo fangasi.

Wapo wanaobeba maelekezo potofu ya mtaani na kufanya usafi eneo hilo kwa kuingiza ukeni vitu kama sabuni, maji yenye kasi, manukato, dawa ya kuoshea na kuulia vimelea anticeptic, vilainishi na mitishamba.

Baadhi huamini kufanya hivi ndiyo usafi salama wa kujikinga na maradhi kama fangasi za ukeni, magonjwa yanayoenea kwa kujamiiana na vile vile kuondoa harufu mbaya.

Ukweli ni kwamba njia hizi si salama kwa afya ya uzazi kwani vikiingia ukeni vinasababisha mabadiliko ya njia na hatimaye kuharibu mfumo wake wa kujilinda.

Na haishauriwi kuweka manukato kukata harufu kwani harufu asili ya ukeni huongeza usisimkaji kwa mwenza wa kiume.

Sayansi ya kitabibu kwa magonjwa ya kina mama inathibitisha kuingiza vitu hivyo ukeni kunaharibu mfumo wa kinga ikiwamo tindikali ya ukeni na kuua vijidudu rafiki kwa eneo hilo la mwili.

Kwa kawaida ukeni huwapo vijidudu rafiki wakiwamo bakteria na fangasi ambao hudhibiti vijidudu visivyo rafiki.

Tindikali ya njia ya uzazi na vijidudu rafiki ni moja ya eneo hilo kujihami dhidi ya magonjwa mbalimbali ikiwamo fangasi za ukeni ambazo mara nyingine hutokea na kuwa sugu kwa wanawake wenye usafishaji wa kuingiza vitu.

Njia ya uzazi ina namna ya asili ya kujisafisha ambayo ni ute ute mweupe ulio na harufu ya kiasili unaoshuka kila siku kutokea katika shingo ya uzazi.

Ni kawaida ute huo unaweza kuwa kiasi cha kijiko cha chai kubadilika badilika ikiwamo pale kijiyai kinapopevushwa, ute huo huwa mzito na rangi ya kahawia iliyofifia.

Aidha wapo ambao kwa kukosa ufahamu wanaweza kudhani pengine kutoka ute huo ni tatizo la kiafya.

Endapo ute huo utakua na harufu mbaya kama kitu kilichooza au uvundo mzito kama shombo la samaki kuenda ni ishara ya magonjwa hivyo vizuri kufika kwa watoa huduma za afya kwa ushauri na matibabu.

Zipo namna salama kiafya ambazo zikitumika husaidia kuboresha mfumo wa ulinzi dhidi ya vimelea adui wanaovamia njia hiyo.

Kitabibu inashauriwa mwanamke asiingize kitu chochote, zaidi inatakiwa kuoga na kusafisha maeneo hayo kwa maji ambayo ni safi na salama tu.

Kila mara anapooga na kwenda haja ahakikishe hakuna unyevu nyevu unaobaki, vizuri kujifuta na kitambaa safi au taulo laini yenye kunyonya maji maji kwa ufanisi.

Unyevu unyevu wowote katika maeneo nje ya uzazi na katika mikunjo mikunjo ya maeneo hayo huweza kuwa ni mazalia ya vimelea kama fangasi na bakteria wasio rafiki.

Aina za nguo za ndani ambazo ni rafiki kwa afya ya njia ya uzazi ni zile zisizobana ambazo zimetengenezwa kwa malighafi za pamba ambazo hunyonya unyenyevu kwa ufanisi na ibadilishwe mara tu inapojaa unyevu nyevu.

Kwa usalama zaidi wa njia hizi wanawake wanapoogelea ufukweni au katika jakuzi wasikae muda mrefu kwani tafiti zinaonyesha kuwa huweza pia kuathiri mazingira ya tindikali ya ukeni ingawa si kwa kiwango kikubwa.