Wanawake hutamani ndoa mapema wakati wanaume wanahofu kupoteza uhuru wao

Muktasari:

  • Wanaume huanzisha familia kwa kushtukizwa, ilihali wanawake wengi wao hujipanga kufanya hivyo
  • Wanaume wanachelewa kuoa au kuanzisha familia mapema kwa sababu wanahitaji kujiandaa kuishi na mke au familia

Kila mmoja hufikiria la kwake anapoona mwanaume analia baada ya ndoa au wakati wanafungishwa ndoa, wengine wakiamini analia kwa furaha, ilimradi hakuna mwenye jibu sahihi zaidi ya mhusika mwenyewe.

Kitendo hicho kikifanywa na mwanaume huwashangaza wengi tofauti na kikifanywa na wanawake ambao mara kadhaa hufanya hivyo tangu enzi na enzi na kuonekana kama ni kitendo cha kawaida.

Huenda utafiti wa mwaka 2018 uliochapishwa kwenye Jarida la Psychology Today ukawa na jibu la swali hilo. Utafiti huo ulibaini kuwa asilimia kubwa ya wanaume wanaogopa kuwa na uhusiano wa kudumu au kufunga ndoa wakiamini wanapoteza uhuru wao.

Katika mahojiano ya utafiti huo yaliyohusisha watu 15,000 wenye wastani wa umri wa miaka 22, ulionyesha kuwa wanawake wanatamani kuolewa wakiwa na umri wa miaka 22 na kuendelea, ilhali wanaume wa kuanzia umri wa miaka 33 mara 10 ya umri wa wanawake hawana mpango wa kufanya hivyo kwa kuogopa kupoteza uhuru wao.

Utafiti huo ulifanywa na National Longitudinal Study of Adolescent Health (Add Health) ulibaini kati ya watu 15,000 wakiwamo wanawake vijana kati ya miaka 22 na wanaume wenye miaka 33 na kuendelea ilionyesha kuwa asilimia 31 ya wanawake walitamani kuanzisha uhusiano wa kuduma ikiwamo ndoa mapema iwezekanavyo huku wanaume waliokuwa na jibu kama hilo wakiwa ni asilimia 20.

Mbali na hilo utafiti huo pia ulibainisha wanawake hutamani kuanza familia mara tu wanapokuwa kwenye uhusiano wa kudumu, ilihali wanaume huwatokea kama dharura.

“Nilibaini wanawake wakihakikishiwa uhusiano wa kudumu hufikiria kuanzisha familia kwa maana ya kupata watoto, huku wanaume wachache wakilitamani hilo.

“Kwa kuwa mwanamke ndiyo mwamuzi wa kuzaa au kutozaa kutokana na sababu za kibaiolojia, wanaume wengi walijibu walianzisha familia kwa kushtukizwa...mpenzi nina mimba ya miezi miwili....” anasema Elizabeth Aura McClintock Ph.D aliyeendesha utafiti huo kwa miezi sita kwenye majimbo tofauti nchini Marekani.

Hata hivyo wataalamu wa saikolojia wanasema kuwa kuoa au kuolewa mapema kunategemea na malezi ya kijana, mila na tamaduni za eneo husika.

Elizabeth anaendelea kufafanua kuwa kwa mujibu wa utafiti huo, asilimia 4 ya wanawake walisema walikuwa tayari kuingia kwenye uhusiano wa kudumu au ndoa na wapenzi walio nao sasa lakini asilimia 23 ya wanaume wakisema hawako tayari kufanya hivyo. Anafafanua zaidi kuwa asilimia nne ya wanawake na tano ya wanaume waliosema kuwa hawaoni nafasi ya uhusiano walionao kuwa wa kudumu.

“Wanawake walitamani sana kubadili uhusiano wa kawaida walionao kuwa wa kudumu na ikiwezekana wafunge ndoa, huku wanaume wakilipinga hilo kwa nguvu zote,” anasema Elizabeth.

Kwa upande wa Zawadi Kambi msomi wa Shahada ya Uhusiano wa Kimataifa ambaye ni mama wa watoto watatu anasema kuwa alizaa mtoto wake wa kwanza na mwanaume ambaye hakuwa tayari kuanzisha familia.

“Iliniletea shida, mwanaume nilikutana naye chuoni nchini India, kwa kuwa anatoka katika nchi mojawapo za Afrika Mashariki sikuwa na shaka, nilijua tunaweza kuoana, hivyo nikabeba mimba.

“Nilipomwambia kuhusu hilo, uhusiano wetu uliishia hapo, alikuwa mkali, mwisho aliniambia wazi hajapanga kuanzisha familia wala kuzaa,” anasema Zawadi.

Zawadi anaeleza kuwa wakati huo alikuwa na miaka 34 na mwanaume aliyezaa naye ambaye sasa ni mumewe alikuwa na miaka 39. Anasema alisoma kwa taabu akilea mimba na hatimaye mtoto bila maelewano na baba yake na alilazimika kuhama eneo alilokuwa anaishi ili kuepuka kukutana naye mara kwa mara.

“Baada ya masomo tulirudi nyumbani, familia ya mume wangu ilimuweka sawa kijana wao, miaka mitano baadaye alinichumbia na sasa ni mume wangu na tuna watoto watatu, ”anasema.

Anasema haikuwa rahisi kufikia makubaliano hayo, lakini kwa msaada wa familia zote mbili walimaliza utata huo na kuoana.

“Nimejifunza, nina kaka zangu watatu karibu wote wameoa wakiwa wanakaribia miaka 40, huku wawili kati yao wakisita sita kukubali watoto waliozaa na wapenzi wao,” anasema Zawadi.

Lakini pia yapo madai kwamba kuna wanawake ‘wanaowategeshea’ wanaume baada ya kubaini siku nzuri ya kupata ujauzito, anakuwa na mpenzi na katika mkakati wa kuanzisha familia akiona mwanaume hana haraka hiyo yeye huweka mazingira ya kupatikana mtoto na hapo familia huanza na hatimaye ndoa.

Naye Moland Nelson anasema alianza kufikiria kuoa mara baada ya kumaliza kujenga. “Niliona nyumba kubwa kuishi peke yangu, lakini siyo kwamba sikuwa na mpenzi nilikuwa naye, ila sikuwa tayari kuoa.

“Nilikuwa naona waliooa wanapigiwa simu kila mara tukiwa tumekaa tunabadilishana mawazo, wengine wakifokeana kwenye simu na magomvi ya aina hiyo,” anasema.

Anafafanua kuwa aliamini kuoa ni kuingia kwenye migogoro ya kifamilia, jambo ambalo lilikuja kuwa tofauti baada ya kuoa.

Anaweza kuwa alichojifunza kila ndoa ina majaribu yake, huku zikiwamo chache zenye amani na kupishana kusiko na madhara.

Hata hivyo anasema habariki vijana kuoa wakiwa na umri wa miaka 25 hadi 30 kwa sababu kipindi hicho ujana unakuwa mwingi, ndiyo kwanza kwa waliosoma na kupata vibarua wanakuwa wameanza kushika fedha.

“Muhimu kusubiri kidogo wakue na wapanuke kifikra, kuoa mapema kwa mwanaume nako ni mtihani kwa sababu atachanganya ujana na familia, mwisho wa siku wanaweza kuachana,” anashauri Nelson.

Nelson anasema kwamba kitu alichokuwa nacho makini kwenye uhusiano kabla ya ndoa ni kupata mtoto, kwa sababu hakuwa anajua atakuja kumuoa nani.

Wataalamu wa afya wanashauri umri sahihi wa kuzaa ni miaka 20 hadi 35

Daktari kutoka Hospitali ya Sanitas na mratibu wa Hospitali Narayana ya India, Limbanga Fredie anasema umri sahihi wa kuzaa ni miaka 20 hadi 40.

Dk Limbanga aliyasema hayo wakati akitoa elimu ya afya katika mkutano wa Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (Tamwa) hivi karibuni.

Naye daktari bingwa wa magonjwa ya akili kutoka Hospitali ya Taifa ya akili ya Mirembe, Dk Damas Andrew anasema kwamba hajafanya utafiti kuhusu kutamani na kutotamani kuoa, kuolewa mapema, lakini kitaalamu wanawake wanawahi kupevuka kiakili.

Anasema suala hilo pia linaendana na jamii inayowazunguka, zipo ambazo wanaume wanatakiwa kuoa mapema na zile ambazo hupanga mwenyewe kufanya hivyo.

“Hizi ambazo kijana akibalehe anatakiwa kuoa au kuolewa, kisaikolojia wanakuwa tayari kufanya hivyo, tofauti na wale wanapanga wenyewe.

“Lakini tofauti ya kisayansi iliyopo kati ya mwanamke na mwanaume ambapo mwanamke akili yake huwa ya kiutu uzima mapema, hivyo humsukuma kuwaza maisha mapema kuliko mwanaume na hiyo inaweza kuchangia wao kutamani kuanzisha familia, kuolewa mapema,” anasema Dk Andrew.