KULIKONI: Wanawake wanapotelea wapi kwenye elimu ya juu?

Dar es Salaam. “Sikufikiria kama ipo siku nitatamani kujiunga chuo kikuu, kwa sababu nilikuwa ninafanya vizuri kwenye mitihani yangu kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha tatu na nikiwa naamini nitaendelea hivyo hadi chuo kikuu.

“Wazazi wangu walipofariki nikalazimika kwenda kijijini kwa shangazi, huko ndiko ndoto zangu zilipopotea hadi leo nalazimika kuunganisha unganisha ili nisome chuo kikuu na huu mwaka wa nane sijafanikiwa, lakini sijakata tamaa,” anasema Mariam Elituwaha.

Mariamu anasema wazazi wake walipofariki (kwa nyakati tofauti) akiwa kidato cha tatu, alikwenda kuishi na shangazi yake Moshi maeneo ya Uchira.

“Maisha yalibadilika, nilikuwa zaidi ya mfanyakazi sina muda wa kusoma, maneno makali ya fedheha na maudhi ndiyo yalikuwa chakula changu.

“Kibaya zaidi licha ya kulipiwa ada na wajomba zangu, shangazi aliniamuru niache shule nikiwa kidato cha nne, niliacha kwa sababu nilikuwa nimeshapoteza mwelekeo sikuwa naongoza shuleni wala darasani hali hiyo ilinikatisha tamaa ya kusoma, ”anasema.

Anasema kwa sababu ya mateso alifunga ndoa kwa shangazi yake alivyokuwa akipenda na sasa ana watoto watatu, anasoma elimu maalumu apate cheti cha kidato cha nne ili aendelee mbele.

Anasema amekuwa akijaribu na kuishia njiani kwa miaka minane sasa kutokana na masomo kuingiliana na maisha kama kuzaa na majukumu mengine.

Huu ni mfano mdogo wa kile kinachowakwamisha wasichana kuendelea na masomo hasa ya elimu ya juu licha ya ukweli kwamba wanapoanza elimu ya msingi kuwa sawa kati ya mwanamke na mwanaume, wanaoendelea elimu ya juu katika kila vijana watano watatu ni wanaume huku wawili pekee wakiwa wanawake.

Mabadiliko huanza wanapofika kidato cha tano na sita, wanaume wanakua wengi zaidi ya wanawake.

Takwimu zinaonyesha wanaume wanaoendelea na elimu katika hatua hiyo ni asilimia 57.9 wakati wanawake hubaki asilimia 42.1 pekee.

Swali ni je wanawake wanapotelea wapi kwenye elimu ya juu?

Swali hilo linatokana na kupungua uwiano kadri wanavyosonga mbele ukilinganisha na wanaume.

Licha ya takwimu za idadi ya watu nchini zinazotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kuonyesha makadirio ya idadi ya wanawake kuwa ni wengi ukilinganisha na wanaume, lakini kwenye elimu ni tofauti, hususani ya juu.

Hii ikiwa na maana kwamba wanawake wengi wamekua wakiishia elimu ya chini.

Kwa mujibu wa takwimu za Ofisi ya Rais Tamisemi za “Takwimu za Elimu Msingi” (Best) pamoja na zile zinazotolewa na Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) zilibainisha kuwa katika ngazi ya elimu ya shule za msingi mwaka 2018 wanawake walikua asilimia 50.1 ukilinganisha na asilimia 49.9 za wanaume.

Uwiano huo unaonyesha kukiwa na takribani hali ya usawa kwa jinsia zote. Kwa elimu ya sekondari (Kidato cha kwanza hadi cha nne) mwaka huo wanawake walikua wengi zaidi wakiwa asilimia 51.5 ukilinganisha na asilimia 48.9 za wanaume.

Hali inaanza kuwa tofauti kidato cha tano na sita, wanaume wanakua wengi zaidi ya wanawake, wakiwa asilimia 57.9 wakati wanawake wakiwa asilimia 42.1 pekee.

Katika ngazi ya chuo hali ni mbaya zaidi kwani zaidi ya asilimia 60 ni wanaume. Hii ina maana kuwa katika kila wanafunzi watano waliochaguliwa kujiunga na vyuo vikuu mwaka 2017/18 watatu au zaidi ni wanaume wakati wanawake ni wawili pekee.

Takwimu hizo za mwaka 2018 hazina tofauti sana na mwaka 2017. Kwani uwiano wa wanawake na wanaume katika ngazi za chini za elimu ulikua kama unalingana (asilimia 50 kwa 50) na kupungua elimu inavyozidi kupanda.

Wanawake wanapotea wapi?

Mkurugenzi Mtendaji wa Msichana Initiative, Rebeca Gyumi aliliambia Mwananchi kuwa ni kweli kwenye elimu ya chini yaani ngazi ya shule za msingi kuna uwiano unaolingana wa wanaume na wanawake ukilinganisha na kiwango cha juu cha elimu kwa sababu wanawake wanapata changamoto nyingi katika upataji wa elimu.

Anasema jambo la kwanza ni umbali kutoka shule licha ya kuwa wanafunzi wa jinsia zote wanaweza wakawa wanatoka mbali lakini wanawake wanapata changamoto nyingi wawapo njiani.

“Unyanyasaji kingono kutoka kwa vijana ikiwemo bodaboda na bajaji ambao wanawaahidi kuwapa usafiri,” anafafanua Rebeca.

Akieleza sababu nyingine alisema ni jinsi jamii inavyowachukulia wanawake, “katika baadhi ya jamii mtoto wa kike anapomaliza darasa la saba inatosha, wanamuozesha na sehemu nyingine wazazi wanawarubuni watoto wajifelishe mitihani yao ili wasiendelee”.

Akichangia hilo Ofisa Programu mwandamizi kutoka Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Deogratius Temba anasema hali hii husababishwa na mazingira yasiyo rafiki kwa watoto wa kike hivyo kuwafanya wafanye vibaya lakini pia kuacha shule kwa sababu mbalimbali ikiwemo suala la mimba, ndoa au ajira za utotoni.

Aliongeza kuwa, “watoto wengine wa kike hususan vijijini ni walezi wa familia hivyo wanakabiliwa na majukumu mengi sababu inayowafanya waache shule.

Naye ofisa programu wa Taasisi ya Twaweza- Uwezo, Richard Temu anasema sababu ya kuacha shule kwa wanafunzi kwa sasa ipo kwa jinsia zote, “Katika kipindi hiki wanaume wanaoacha shule idadi yao pia inaongezeka kwa sababu mbalimbali ikiwemo wazazi kutokutilia maanani suala la elimu na kutokuwepo mikakati ya kuzuia watoto kuacha shule kama ilivyo ya kuhamasisha waende shule.

Naye mwalimu mkuu wa Shule ya Sekondari Lushoto, Mwanga Wetundwa anasema sababu zilizokua zinachangia wanawake kuacha shule kipindi cha nyuma mojawapo ilikua ni ada pamoja na wanafunzi kukosa elimu ya saikolojia kwa maumbile na jinsia ambapo alisema suala hilo limepungua.

Nini kifanyike?

Mushi wa TGNP anapendekeza kuwa ipo haja kwa jamii na Serikali kushirikiana kuboresha mazingira ya shule ili yawe rafiki kwa watoto wa kike sababu itakayowafanya wasiache shule na wafanye vizuri.

“Kuna haja ya kujenga mabweni kwa wanaokaa mbali lakini miundombinu kama vyoo na maji kwa watoto wa kike hata wanapokua kwenye kipindi cha hedhi waweze kujihudumia,” alisema na kuongeza kuwa Serikali kupitia Wizara ya Elimu na halmashauri zina haja ya kutenga bajeti na kusimamia mambo haya.

Naye Temu wa Twaweza alisema ipo haja sasa kwa Serikali kufuatilia kwa karibu na kutilia mkazo suala la watoto wanaoacha shule kama inavyofanywa wenye kuhakikisha wanaoandikishwa kila mwaka.

“Inatakiwa mikakati ya kuwabakiza watoto shule. Serikali inapokea takwimu za kila mwaka, inahitajika taarifa za wanaoacha shule kila mwaka zifuatiliwe na kufanyiwa kazi ili kupunguza au kuondoa tatizo,” alifafanua.

Rebeka anashauri kwa mikakati ya muda mrefu kusimamia utekelezaji wa sera ya elimu ya mwaka 2014 inayosema kiwango cha chini cha elimu kiwe angalau elimu msingi (hadi kidato cha nne). “Ikisimamiwa sera hii basi wanawake wanaoacha shule wanaweza kudhibitiwa, lakini pia wanaopata mimba waweze kurudi shuleni.” aliongeza.

Mwalimu Wetundwa alisema kuna umuhimu wa wadau yakiwamo mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs) kutembelea shule mbalimbali na kutoa mafunzo kwa wanafunzi juu ya mabadiliko ya kimaumbile na umuhimu wa elimu.

Kwa upande wa Mariamu anasema kuwa kuna umuhimu wa jamii kuwasaidia watoto wa kike kufikia malengo yao, bila kujali wanatoka kwenye familia gani.

“Nilikuwa nateseka na majirani wanaona hakuna aliyechukua hatua kunisaidia, jamii pia haikwepi lawama hii,” anasema.