Hii hapa fursa kwa wabunifu katika sekta ya kilimo

Muktasari:

  • Kama una wazo la kuboresha sekta ya kilimo kupitia ubunifu wa kiteknolojia, unaweza kushindanisha wazo lake kupitia mradi wa e-Kilimo

Sekta ya kilimo ni moja ya vichocheo muhimu vya ukuaji wa uchumi wa taifa lolote duniani. Hapa nchini, zaidi ya asilimia 65 ya Watanzania wanategemea kilimo kuendesha maisha yao ya kila siku.

Hata hivyo, licha ya watu wengi kutegemea kilimo, sekta hiyo imekuwa na mchango mdogo katika pato la Taifa, licha ya ukweli kuwa kuna mazao mengi yanayoweza kuchangia uchumi wa nchi na kuongeza kipato kwa wananchi.

Matumizi ya teknolojia yanatajwa kuwa moja ya njia zinazoweza kutumika kuimarisha sekta ya kilimo. Na hii ni pale Watanzania watakapoamka na kubaini fursa za ubunifu wa teknolojia zilizopo kwenye sekta hiyo.

Kilimo kwa teknolojia

kilimo pekee bila teknolojia hakiwezi kuwa na tija. Hivi sasa kuna teknolojia ya kidigitali ambayo inatoa fursa muhimu kwa maendeleo ya kilimo nchini.

Wadau wa kilimo wameanzisha mradi wa e-Kilimo kwa ajili ya kuwawezesha watu wenye mawazo bora ya kilimo na kuyaboresha katika namna ambayo itayafanya yawe bora zaidi.

Programu hiyo iliyoandaliwa na kusimamiwa na shirika linalojihusisha na masuala ya teknolojia na ujasiriamali (Sahara ventures) itaambatana na mafunzo ya kilimo kwa vijana.

Mratibu wa mradi wa e-Kilimo, Abbas Sykes anasema mradi huo unalenga kutafuta wabunifu mbalimbali kwenye sekta ya kilimo. Anasema mradi huo unaangalia zaidi urahisi wa kutumia teknolojia katika kutatua matatizo yanayowakabili wakulima.

“Wabunifu wajue kwamba siyo lazima ushike jembe kwenda shambani ndiyo upate faida, lakini unaweza kuingiza faida kwa kutumia teknolojia tu, ukajipatia kipato na ukawa umewasaidia wakulima,” anasema Sykes.

Anasema kilimo kina fursa kubwa kwa sababu ndiyo kinaajiri watu wengi hapa nchini na moja ya maeneo yenye fursa ni ubunifu wa teknolojia ambazo zitawasaidia wakulima kuongeza mapato yao.

Mratibu huyo anabainisha kwamba mawazo ya wabunifu yanatakiwa kuwa na sifa kuu tatu ambazo ni pamoja na kuwa na teknolojia ndani yake, iwe ni teknolojia endelevu na iwe ni kitu kinachoonekana.

“Tumepokea mawazo karibu 300, lakini mwishowe tukachagua mawazo bora tisa na baadaye tutachagua washindi wanne. Tunachokifanya ni kuyaboresha mawazo ya wabunifu na kuyajengea business model (muundo wa biashara),” anasema.

Sykes anasema mradi huo ni wa miezi 12 na mawazo yanayoshindanishwa yapo tayari na yanafanya kazi.

Anasema jukumu lao ni kusimamia mawazo hayo ya kibunifu na kuyaboresha ili yawe rafiki kwa wakulima.

Baadhi ya mawazo ya kibunifu yaliyoshiriki kwenye mradi wa e-Kilimo ni Sky Gulio ambayo ni teknolojia inayorahisisha uuzaji na ununuaji wa chakula. Teknolojia hii itapunguza matumizi ya muda wa kwenda kwenye masoko na utaletewa pale ulipo. Shamba Faida ni wazo jingine la kibunifu ambalo linatoa fursa ya soko kwa wafanyabiashara wa mazao kukutana na wakulima walio tayari kulima kibiashara na wawekezaji walio tayari kufadhili kilimo hicho. Jukwaa hilo linapatikana kwa njia ya mtandao.

Doctor Kilimo ni ubunifu mwingine ambao unawawezesha wakulima kupata taarifa mbalimbali juu ya magonjwa ya mazao na namna ya kukabiliana nayo. Jukwaa hilo pia linapatikana kwa njia ya kidigitali.

Vilevile, Jamvi ni jukwaa jingine ambalo linawakutanisha vijana na wafanyakazi wa kada mbalimbali kuwekeza kwenye kilimo cha kibiashara na kugawana faida na wakulima. Jamvi ni kitovu cha biashara kati ya makundi hayo mawili.

Kilimo Guide ni jukwaa ambalo linawawezesha wakulima na kuwapatia fursa za uwekezaji kwenye kilimo.

Kupitia jukwaa hilo, wakulima wanapatiwa mbegu bora, pembejeo za kilimo, mafunzo ya kilimo cha kisasa na kuongeza thamani ya mazao yao.

Teknolojia zote hizo zinampatia fursa mkulima kupata taarifa mbalimbali juu ya kilimo anachofanya, namna ya kuongeza thamani ya mazao na kujua masoko yanakopatikana na kupanga bei ya mazao yake.

Maendeleo haya ya teknolojia yametoa nafasi kwa wakulima kukutana na wateja wao, washauri wao, madaktari wao na wafadhiri wao ambao wangependa kuona mkulima anapata mafanikio katika kilimo chake.

Ni wakati sasa wa wakulima nchini kubadilika na kuendesha kilimo kinachokwenda na wakati, kilimo chenye tija, kwa kuzingatia teknolojia ya kidigitali ambayo imerahisisha utendaji kazi kwa wakulima na wafanyabiashara popote nchini.

Kwa wenye mawazo ya kiubunifu na wangependa kushiriki katika mradi huu siku zijazo, wanaweza kuwaona wahusika katika ofisi ya Tume ya Sayansi na Teknolojia (Costech). ambayo makao makuu yake yapo jijini Dar es Salaam.