Michikichi fursa inayoweza kuwatoa kimaisha wakulima wengi

Saturday April 20 2019

 

By Elias Msuya, Mwananchi [email protected]

Licha ya Tanzania kuwa na hali ya hewa inayoruhusu uzalishaji wa zao la michikichi, uzalishaji wake uko chini ukilinganishwa na nchi zianzozalisha kwa wingi kama vile Malaysia na Indonesia.

Ni kwa sababu hii Tanzania hujikuta ikiagiza karibu tani 400,000 za mafuta ya mawese ili kukidhi mahitaji ya mafuta yanayokaribia tani 600,000 kwa mwaka, huku pia ikizalisha tani 210,000 kutoka kwenye mazao mengine kama vile alizeti, karanga, ufuta, pamba na mawese.

Kuepuka matumizi makubwa ya fedha zinazotumika kuagiza mafuta haya, wakulima wanaweza kuchangamkia kilimo cha michikichi, ambacho ni aina ya kilimo kinachokubali katika maeneo mbalimbali nchini.

Hata ulimaji wake hauna ugumu sana ikiwa mkulima atafuata maelekezo kutoka kwa wataalamu wa kilimo. Kwa sasa zao la michikichi linaelezwa kufanya vizuri zaidi katika mkoa wa Kigoma ambapo asilimia 80 ya mafuta ya mawese yanazalishwa mkoani humo.

Hata hivyo, uzalishaji huu unakwazwa na matunzo na mauzo ya mafuta hayo kwa kuwa wakulima wengi hawafuati misingi ya biashara.

Mbali ya Kigoma, mikoa mingine inayoweza kustawisha zao hilo ni Pwani, Mbeya (hasa wilaya ya Kyela), Tanga, Tabora, mabonde ya mto Rufiji na Kilombero.

Advertisement

Fursa kwa wakulima

Kwa mujibu wa kitabu cha Hali ya Uchumi wa Taifa cha mwaka 2017, imeonekana kuwa uuzwaji wa mafuta hayo umekuwa ukipanda mwaka hadi mwaka na hivyo kutoa fursa mpya ya wakulima wa zao hilo kimasoko.

Ni kutokana na fursa hiyo, Serikali sasa imeamua kuwekeza kwenye zao hilo ili kuongeza uzalishaji na kuziba pengo la uagizwajii wa mafuta hayo kwa matumizi ya ndani.

Mapema mwama huu, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alitembelea Mkoa wa Kigoma na kuitaka Wizara ya Kilimo kusimamia mkakati wa kuendeleza kilimo cha michikichi mkoani Kigoma, ili zao hilo lilete mapinduzi ya kiuchumi nchini.

Alisema kuwa mkakati uliowekwa katika kusimamia zao hilo ukitekelezwa, una mchango mkubwa kwa zao hilo kuchangia kwa kiasi kikubwa mapato ya nchi.

Akikagua uzalishajii wa mbegu bora za michikichi, alipotembelea kituo cha utafiti wa michikichi Kihinga wilaya ya Kigoma, alisema kuwa ni lazima zao la michikichi lilete tija kwenye uchumi wa nchi na kuboresha maisha ya wakulima wa zao hilo.

Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (Tari), Dk Geofrey Mkamilo anasema baada ya Serikali kutoa kipaumbele kwa zao hilo, sasa wameanza kufanya utafiti wa mbegu bora. Alikitaja kituo cha utafiti wa michikichi cha Kihinga kilichoanzishwa kwa ajili hiyo kuwa kitazalisha mbegu zitakazozalisha chikichi tani tano hadi nane kutoka tani 1.5 za sasa kwa hekta moja.

Baadhi ya kampuni zimejitokeza kuwekeza kwenye zao hilo ikiwa pamoja na African Green Oil iliyoripotiwa kuwa na mpango wa kuendeleza hekta 20,000 ifikapo mwaka 2020. Hadi mwaka 2009, kampuni hiyo ilikuwa imepewa hekta 5,000 na ilipanda hekta 435 kwa ajili ya majaribio.

Katika Wilaya ya Bagamoyo iliyopo mkoani Pwani, kampuni ya Tanzania Biodiesel Plant ilikuwa na hekta 16,000 kwa ajili ya kilimo hicho wakati kampuni ya Infenergy ilikuwa imepewa zaidi ya hekta 5,000 katika wilaya ya Kilombero kwa ajili ya lengo hilohilo.

Maeneo mengine yanayotajwa kufaa kwa kilimo hicho na kuifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zinazozalisha mawese kwa wingi ni pamoja na mabonde ya Mto Rufiji na Kilombero.

Hali ilivyo kwa sasa

Wakulima wa Tanzania wamekuwa wakilima zao hilo kwa mazoea na siyo kibiashara. Kwanza mbegu wanazotumia hazina uwezo wa kuzaa matunda mengi na pia matunda hayo hayana kiasi kikubwa cha mafuta.

Mbegu za asili zinazotumika huzalisha tani moja hadi tatu kwa hekta moja na mafuta chini ya asilimia 8, wakati mti wa kisasa wa mchikichi huweza kuzalisha tani 12 hadi 40 za matunda kwa hekta moja ikwa pia na kiasi cha asilimia 25 hadi 30 za mafuta.

Kama wakulima watalima aina hiyo watapata masoko haraka kwani mazao hayo ndiyo yanayotakiwa na wawekezaji.

Nchi zinazozalisha mafuta mawese kwa wingi huzalisha kwenye mashamba makubwa yanayomilikiwa na vikundi vya wakulima. Lakini kwa Tanzania na hasa Kigoma, hakuna mashamba makubwa wala hakuna vyama vya wakulima wa michikichi. Wakulima wenyewe hawana taarifa za kutosha kuhusu masoko na hivyo kulifanya zao hilo kukosa mwelekeo wa kimasoko.

Kwa mfano nchi ya Malaysia ilizalisha tani milioni 20 za mafuta ya mawese katika mwaka 2015, ambazo zilikuwa asilimia 32 ya jumla ya uzalishaji wa kimataifa ambao ni tani milioni 62.8 kwa mujibu wa Bodi ya Mafuta ya Mawese ya Malaysia (MPOB).

Kwa mujibu wa Ripoti ya mwaka ya utafiti wa sekta ya kilimo (AASS 2016/17) iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) inaeleza kuwa eneo lililopandwa miti ya michikichi mwaka 2016/2017 lilikuwa hekta 9,742 lakini ni asilimia 79.2 tu ya miti hiyo ilivunwa.

Hii inadhihirisha kuwa licha ya jitihada za wakulima kulima zao hilo bado hawafaidiki inavyotakiwa na zao hilo kutokana na kukosa mbinu bora za kulima na masoko ya uhakika hapa nchini.

Hata hivyo, mabonde ya Rufiji mkoani Pwani na Kilombero (Morogoro) yanatajwa kuwa maeneo mapya ya kuendelezwa kwa ajili ya kwa kilimo cha michikichi, jambo litakalosaidia kuongeza uzalishaji wa mafuta ya kula nchini.

Mafuta ya mawese pia yanafungua fursa ya uanzishwaji wa viwanda vidogo vidogo vya kutengeneza sabuni na kutoa ushindani kwa wajasiriamali wanaozalisha bidhaa hiyo nchini.

Wilayani Kyela, tayari wajasiriamali kama Nuru Njumbo ameanza kutengeneza sabuni hizo lakini ameileza Nukta kuwa changamoto inayowakabili ni upatikanaji wa mawese kwa wakati kutokana na uzalishaji mdogo wa zao hilo.

Nyongeza kwa hisani ya mtandao wa www.nukta.co.tz

Advertisement