Mwakalikamo anavyozisubiri milioni 500 za miche ya michikichi

Jitihada zinalipa. Tangu aanze kilimo cha michikichi zaidi ya miongo miwili iliyopita, Jumapili Mwakalikamo hivi karibuni anaweza kuingia katika orodha ya mamilionea wa kilimo nchini.

Serikali kupitia Wizara ya Kilimo imempa kibarua cha kuandaa miche milioni moja ya michikichi na kwa bei waliyokubaliana, akifanikiwa anaweza kujiingizia kipato hicho kikubwa cha fedha kwa kila mwaka.

Mwakalikamo ambaye ni mkulima na mzalishaji wa zao hilo kutoka Kigoma, anasema safari yake ya uzalishaji mbegu na miche ya michikichi, ilianza mwaka 1995 kwa kupanda miche 200 katika eneo la robo ekari kwa mtaji wa Sh 500,000 , huku mtaji wake kwa sasa ukiongezeka na kufikia Sh40 milioni.

Anasema anazalisha miche ya michikichi katika vitalu vyake vilivyopo barabara ya Kagashe eneo la uwanja wa ndege, wilaya ya Kigoma mjini.

“ Kwa sasa nazalisha miche zaidi ya milioni moja kwa mwaka na niliamua kuanzisha uzalishaji wa mbegu na miche baada ya kuona kuwa hakukuwa na watu wanaofanya biashara hii” anafafanua

Kupitia uzalishaji huo, Mwakalikamo amefanikiwa kuingiza mkataba wa miaka minne na Wizara ya Kilimo, ambapo kila mwaka anatakiwa kuzalisha miche milioni moja

Anasema katika mkutaba huo mche mmoja wa michikichi atauza kwa bei ya Sh 500, hivyo miche milioni moja anayotakiwa kuzalisha na kuiuzia wizara anatarajia kupata Sh 500 milioni kwa mwaka.

Uzalishaji wa michikichi

Mkulima huyo mwenye elimu ya darasa la saba, anasema amebuni aina mpya ya uzalishaji wa mbegu za michikichi kwa kutumia pipa badala ya oveni.

“ Kwa kawaida ukizalisha mbegu ya michikichi kwa kutumia ovena inachukua siku 100, ili mbegu iweze kuota na kwenda kuipanda katika vitalu, ila ukitumia pipa, unachukua siku 72 tu” anasema.

Anasema kwa kutumia pipa, yeye hukata pipa na kulichimbia shimo chini na kuweka majani ya mabingobingo, mabaki ya mikaa na vipande vya mabati ambayo huhifadhi joto na kufikia nyuzi joto 40, ambapo hapo mbegu inakuwa tayari kuota na kwenda kupandwa katika vitalu ndani ya siku hizo 72.

Mkulima huyo anasema tangu kupanda hadi kuvuna zao hilo, huchukua muda wa miaka saba kama mbegu ni ya asili na huchukua miaka mitatu hadi mitano kwa mbegu ya kisasa.

Anasema kilimo hicho hustawi vizuri katika maeneo yenye udongo wa tifutifu na kichanga ambao huruhusu maji kupenya kwa urahisi na hivyo kuruhusu mizizi ya michikichi kutambaa.

Msimu mzuri wa kupanda mbegu kuanzia mwezi Novemba na Desemba na kwamba kama eneo la kilimo litakuwa na maji ya kutosha basi kilimo hicho kinaweza kufanywa muda wowote kwa sababu miche ya michikichi inahitaji maji ya kutosha. kwa wa wiki moja ndio akaanza kuikamua mafuta, kwa hali hii lazima Mafuta yawe na harufu” anaonya.

Mavuno yake

Mwakalikamo anabainisha kuwa katika kila ekari moja ya michikichi ya asili, mkulima ana uwezo wa kuvuna tani 1.5 ya michikichi, ambayo ni sawa na lita 1500 za mafuta ya mawese.

Kwa upande wa michikichi ya kisasa, mkulima anaweza kuvuna tani nne hadi tano za michikichi, ambayo ni sawa lita 4000 hadi 5000 za mafuta ya mawese kwa ekari moja.

Bei ya mafuta ya mawese

Anabainisha kuwa, lita 20 ya mafuta ya mawese inauzwa kwa Sh 28,000 hadi 30,000 lakini pia inategemea na msimu husika kwa kuwa kuna kipindi bei hupaa na kuwa zaidi ya hapo.

“Wanunuzi wengine wa miche hii ni taasisi na mashirika mbalimbali na wakulima wa kawaida” anasema.

Changamoto iliyopo:

Mkulima huyo anasema anakwazwa kwa kuwa na eneo dogo la kuotesha mbegu na kupanda miche, hivyo anaomba apewe ekari 100 alizoahidiwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, wakati alipotembele mkoa wa Kigoma na kuvutiwa na vitalu vya miche ya michikichi anayozalisha.

“ Zile ekari 100 bado sijapewa, nikipewa lazima uzalishaji utaongezeka, lakini pia nitatoa ajira kwa vijana na hivyo kukuza uchumi” anasema.

Mikakati yake

Aneleza kuwa mikakati yake kwa sasa ni kuwa na kilimo endelevu, kupata ekari 100 kws ajili ya shamba darasa, kuajiri vijana na wanawake, kufuga ng’ombe na samaki na kuchakata mafuta ya mawese kuwa grisi ya kulainishia mitambo.