Breaking News

Ujasiriamali wa mtama ulivyomtoa Agatha

Saturday May 18 2019

Agatha Laizer akionyesha bidhaa anazotengeneza

Agatha Laizer akionyesha bidhaa anazotengeneza kutokana na mtama.Na mpiga picha wetu 

By Mwandishi wetu, Mwananchi

Shauku ya kufanya mambo ni kiungo muhimu katika mafanikio. Hivyo ndivyo ilivyo kwa Agatha Laizer, mkazi wa jiji la Arusha aliyefanikiwa kuwa mjasiriamali wa kusindika mtama na kusaga na kuuza unga wake.

Agatha ni miongoni mwa wasindikaji wachache nchini Tanzania wanaotumia mtama kutengeneza bidhaa mbalimbali. Mtama ni zao la nafaka linalostawi hata katika maeneo yenye ukame. Hutumika kama chakula cha familia lakini linaweza kuwa bidhaa ya biashara kwa wajasiriamali.

Licha ya virutubisho muhimu vilivyomo kwenye mtama, matumizi na mahitaji ya mtama yanakabiliwa na vikwazo kama uwekezaji mdogo na mwendelezo hafifu wa mnyororo wa thamani. Hii ni pamoja na uhaba wa aina mbalimbali za vyakula vilivyoongezwa thamani kwa ajili ya matumizi ya kaya na wingi wa masoko.

Hata hivyo, kwa Agatha, habari ni tofauti kwani ameonyesha kufanikisha azma yake kupitia zao hilo. Ameonyesha kudhamiria kulifanya zao la mtama kuwa kichocheo cha maendeleo yake.

“Mimi huchoma nafaka mwenyewe,” anasema huku , akionyesha sufuria kubwa. “Mimi na wasaidizi wangu hutumia vijaruba, maandiko na vifungashio vya masanduku ambayo huwa tunatuma kwa maduka mbalimbali.”

Hata hivyo, haikuwa rahisi kufikia mafanikio ya usindikaji wa mtama, kwani kazi hiyo pia inahitaji mashine maalum ambayo haipatikani Tanzania. Ni vigumu kusimamia uagizaji na pia ni gharama kubwa kwa mfanya biashara mdogo.

Advertisement

“Serikali imekua na msaada mkubwa, ninasubiri baadhi ya mashine nilizoagiza kuingia nchini. Naweza pia kuhamasisha wakulima kuwa na hamu ya kulima mtama zaidi na kukuza zao hili binafsi ili kufanya upatikanaji rahisi wa kupata malighafi. Kikubwa kinachohitajika ni mitaji ya kulipia vyombo vya kazi,” anasema Agatha.

Tayari, Idara ya mambo ya nje na biashara ya Australia na miradi inayofadhiliwa na IFAD Smart Food na SOMNI wameweka lengo kuu la kufahamu mahitaji ya walaji, kufanya kazi na wasindikaji ili kuendeleza bidhaa za kisasa zinazopatikana kwa urahisi. Wafadhili hawa walishirikiana na wahamasishaji kama Agatha kufanya mabadiliko hayo.

Mradi wa Avisa

Mradi wa Avisa, uliozinduliwa Februari mwaka wa 2019 na unaofadhiliwa na taasisi ya Bill na Melinda Gates imelenga kusaidia wajasiriamali kama Agatha katika hatua mbalimbali ikiwa pamoja na uzalishaji wa mbegu na upatikanaji wa masoko ya bidhaa zake.

Agatha alishiriki katika mkutano wa uzinduzi wa mradi wa Avisa uliohudhuriwa na wanasayansi, wataalamu wa mifumo ya utafiti wa kilimo wa kitaifa na wawakilishi wa kampuni binafsi za mbegu na huko ndiko alikopata ujuzi wa kusindika unga wa mtama na kutengeneza bidhaa.

Mradi huo una lengo la kujaza pengo katika uzalishaji na utafiti wa nafaka maalum na mikunde, kwa kupitia aina ya masoko yanayotokana na mazao matano, mtama likiwa ni zao mojawapo linalolimwa katika nchi saba za Afrika.

Ofisa wa taasisi ya Bill na Melinda Gates, Jeff Ehlers anasema: “Moja ya malengo ya msingi ya mradi wa Avisa ni kuhakikisha uhusiano mkubwa na sekta binafsi, zikiwamo kampuni za mbegu na wasindikaji, ili kuweza kujenga mzunguko wa thamani.’’

Advertisement