Breaking News

Umefikiria kufuga bata? anza leo

Saturday May 25 2019

 

By Flora Laanyuni, Mwananchi

Wafugaji wengi wadogo wa bata nchini wanafuga bata chotara ambao

wamechanganyika na aina mbalimbali za jamii ya bata.

Matumizi makubwa ya bata hawa ni kwa ajili ya kupata nyama, japokuwa wanaweza pia kutumika kwa ajili ya kupata mayai na mapambo ya nyumbani, sehemu za biashara, bustanini, maeneo ya kupumzikia au hotelini.

Aina za bata

Aina maarufu ya bata wa nyama ambao pia hufugwa kwa wingi kibiashara ni Pekin. Asili ya bata hawa ni kutoka bara la Asia hasa China.

Unaweza kuwatambua bata hawa kwa rangi ambayo ni nyeupe. Aina hii ya bata wana sifa zifuatazo:

Advertisement

• Hukua haraka na wana umbo refu.

• Wana vidari vilivyojaa na ngozi zao ni rangi ya njano.

• Vichwa na miguu ya bata hawa huwa na rangi nyekundu iliyochanganyika na njano.

• Dume wa Pekin huwa na wastani wa kilo 4.5 na majike kilo nne wakiwa hai.

Banda

Kama ilivyo kwa aina nyingine ya mifugo, bata pia wanahitaji kuwa na banda zuri kwa ajili ya kujisitiri na usalama wao.

Mfugaji anaweza kutengeneza banda kulingana na mazingira yake, mahitaji na malighafi zinazopatikana.

Paa la banda linaweza kuwa la nyasi, makuti, vigae au bati alimradi mvua, joto na baridi kali visiruhusiwe kuwamo ndani.

Kuta zinaweza kujengwa kwa kutumia miti, udongo, mbao, matofali au bati. Sakafu inaweza kuwa ya saruji, zege au udongo.

Unaweza kuweka matandazo ya pumba za mbao au maranda, huku sakafu ikiwa ya nyavu za chuma au fito kama kichanja.

Banda liwe kavu na mwanga wa kutosha lenye kuruhusu mzunguko wa hewa vizuri.

Kipimo kiwe ukubwa wa kuweka bata wakubwa watatu katika mita

moja ya mraba. Bata wanaokua wasizidi sita wenye umri wa wiki nne katika eneo la ukubwa huo.

Ni vizuri kuwa na kijibwawa kwenye eneo la kufugia, ili kuwa na maji safi ya kutosha maana huongeza urutubishaji wa mayai.

Pia, huongeza mazingira ya unyevunyevu unaohitajika kwa uhatamiaji wa mayai.

Uzalishaji

• Majike ya bata yachaguliwe kutoka kwenye majike mama yenye uwezo wa kutaga mayai mengi, kuhatamia vizuri na kutotoa vifaranga wengi (15 hadi 20).

Madume yawe na uwezo wa kupanda yakiwa na umri wa miezi sita na majike nayo huanza kutaga yakiwa katika umri huo huo.

• Inashauriwa kuwe na madume na majike ya ukoo mmoja katika upandishaji ili kuondoa kurithishwa kwa sifa mbaya katika kizazi kijacho.

Kwa mfano, uwezo mdogo katika utagaji, uanguaji wa mayai, ukuaji hafifu, kushambuliwa kirahisi na magonjwa na kadhalika.

• Dume moja la bata lina uwezo wa kupanda/kurutubisha majike manne hadi sita.

• Inashauriwa dume na majike wakae pamoja kipindi cha mwezi mmoja au zaidi kabla ya majike kutaga. Hii inasaidia mayai kupata muda wa kutosha wa kurutubishwa kabla ya kutagwa. Majike yana uwezo wa kutaga, kuhatamia na kuangua vifaranga 15 hadi 20.

• Uhatamiaji huchukua siku 28. Bata aina ya Muscovy kutoka Amerika ya Kusini wao huatamia kwa muda wa siku 35.

Makala hii ni kwa hisani ya mtandao wa mkulima.

wasiliana nao kupitia mbunifu.www.mkulimambunifu.c.tz au mfugaji Ombeni Urio 0756 641 810.

Advertisement