Warioba: Nyerere aliendeleza vitu vinavyoleta maendeleo ya watu

Monday October 19 2020
warioba pic

“Wakati huu wa uchaguzi kila mmoja anapotaka kujenga hoja yake anarejea kwenye mawazo ya Mwalimu,” anasema Waziri Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba alipozungumza na baadhi ya waandishi wa habari jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki.

“Mwalimu Nyerere alisema kuna vipimo vingi vya maendeleo. Lakini watalaamu kwa kawaida wanataka kuleta vipimo ambavyo vinaonyesha Pato la Taifa limekua. Yeye alisema hicho siyo kipimo pekee kwa sababu unaweza kuona Pato la Taifa limekua kumbe watu wanaomiliki uchumi ni wachache, yaani matajiri, huku wananchi wengi wako katika dimbwi la umasikini,” anasema Jaji Warioba na kuongeza kwamba, “Kwa hiyo mwalimu alisema kipimo kizuri ni kwamba maendeleo lazima yahusishe watu.”

Alisema kwa mujibu wa Mwalimu Nyerere, ni lazima kuyapima maendeleo hayo kwa kutathmini na kuona wananchi wengi wanaishi vipi; je, wanapata chakula bora? Wana makazi mazuri? Wana mavazi mazuri? Je, elimu yao ikoje? Na pia kuangalia upatikanaji wa huduma yao ya afya.

“Lakini ili uweze kupata maendeleo hayo, lazima uweke mazingira wezeshi, ikiwa ni pamoja na vitu vinavyochochea maendeleo. Vitu hivyo ni pamoja na huduma ya usafiri ambayo inahitaji barabara pamoja na madaraja. Kwa hiyo Mwalimu alikuwa anasema kitu ambacho ni cha msingi kabisa ni kupima maendeleo kwa kuangalia maendeleo na huduma zinazowafikia watu,” alisema.

Akifafanua falsafa na msimamo wa Mwalimu kuhusu maendeleo ya watu na vitu, Jaji Warioba alisema katika jitihada zake, Mwalimu Nyerere aliendeleza vitu vilivyokuwa vinasaidia kuleta maendeleo ya watu.

Alitolea mfano ujenzi wa shule, hospitali, zahanati, barabara, na viwanda.

Advertisement

Alisema alifanya hivyo kwa sababu hayo ndio mazingira ambayo yanaleta maendeleo ya watu. Bila mazingira hayo kwa mfano elimu nzuri, huwezi kuwa na maendeleo mazuri,” anasisitiza huku akilinganisha mtazamo huo na hoja zinazotolewa na baadhi ya wagombea kwamba awamu ya tano imejikita zaidi katika maendeleo ya vitu na kusahau maendeleo ya watu.

Aidha, alisema ingawa anaridhishwa na mwenendo wa kampeni zinazoendelea, ametoa wito Watanzania wawe macho muda wote hasa wakati huu wa kipindi cha uchaguzi mkuu. “Lazima tuwe macho kwa kulinda amani yetu. Wananchi waende kusikiliza hoja na sera za wagombea ili wapige kura kwa kujiamini.”

Kwa mtazamo wake, anasema kampeni zinaendelea vizuri katika mazingira ya amani.

“Ukiangalia vurugu nyingi zinazotokea katika bara letu la Afrika zinatokana na shughuli za uchaguzi. Uchaguzi tutafanya utapitam maisha yataendelea. Na sisi Watanzania tangu tupate uhuru tumeishi katika mazingira ya amani. Hiki ndicho kitu kikubwa kwetu kwa sababu hatutaweza kufanya chochote cha maana kama hatuna amani. Kwa hiyo katika kipindi hiki ambacho mahala pengi huwa kuna hatari ya kuleta vurugu kwa njia ya hoja zinazoweka sumu, lazima tuvumiliane, wote tulinde amani yetu. Tumalize shughuli za uchaguzi kwa amani,” ameshauri Jaji Warioba.

Hata hivyo, akizungumzia tatizo la rushwa nchini, alisema vita dhidi ya rushwa na ufisadi inayoendelea nchini, imempatia faraja kwa sababu ni mambo yaliyolisumbua taifa kwa muda mrefu.

Alisema mwaka 2015 wakati CCM inazindua kampeni zake Jangwani, jijini Dar es Salaam, alikuwa miongoni mwa watu waliomwombea kura Dk John Magufuli.

Anasema alichokisema wakati ule kuwa nchi ilikuwa inahitaji kiongozi mzalendo, mwadilifu mwenye kuchukia rushwa, mpenda maendeleo na mchapa kazi, ndicho kilichotokea.

Jaji Warioba ambaye mwaka 1996 aliongoza Tume ya kuchunguza kero za rushwa nchini, anasema alitumia nafasi hiyo kuwashawishi Watanzania kumchagua mgombea wa CCM kwa sababu aliamini anazo sifa hizo.

Kwa kile kinachoonekana kuridhishwa na utendaji kazi wa mtu aliyempigia debe kuingia ikulu, Jaji Warioba anatathmini utendaji wake.

“Tukizungumzia rushwa, ni moja ya mambo ambayo yamenivutia sana katika kazi za awamu hii ya tano.”

Anakiri kwamba mwelekeo wa Serikali na msimamo wake kupambana na rushwa, kurejesha uadilifu katika utumishi wa umma na kudhibiti dawa za kulevya umemvutia.

Anasema rushwa ilileta athari na kuharibu mwenendo wa maisha ya watu miaka ya nyuma hasa baada ya Mwalimu Nyerere kung’atuka madarakani.

“Viongozi wengi walishughulikia rushwa na hasa mwasisi wa taifa hili. Mwalimu alikuwa havumilii vitendo vya rushwa. Alikuwa havumilii watu wanaojihusisha na rushwa. Nakumbuka siku za mwisho bado alikuwa anazungumza kwa nguvu sana kuhusu rushwa. Mwaka 1995 alipozungumzia nyufa, moja ya nyufa alizozungumzia ni rushwa,” anaeleza Warioba.

Alipoulizwa ni vigezo gani alivyotumia kutathmini na kuridhishwa na jitihada za vita dhidi ya rushwa nchini, Jaji Warioba anasema Rais Magufuli amejibu hoja na kero za wananchi ambazo walizitoa wakati wa kupokea maoni ya kuandika katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

“Mimi nilibahatika kuongoza Tume ya mabadiliko ya katiba. Tulizunguka nchi nzima na kati ya masuala makubwa ambayo wananchi walizungumzia ilikuwa ni kuporomoka kwa maadili,” anasema na kuendelea, “Wakati huo viongozi na wananchi wengi hawakuwa na nidhamu, kulikuwa na rushwa na ufisadi ambao sasa hivi umepungua kwa kiwango kikubwa.”

“Na katika mkutano wake wa mwisho kwenye mkutano mkuu wa CCM wa uteuzi mwaka huohuo (1995) alisema kiongozi tunayemhitaji lazima aonekane ana sifa za kupambana na rushwa. Kwa hiyo kazi iliyofanyika na Serikali ya awamu ya tano ni nzuri lakini tatizo bado lipo. Na hatua tunazochukua kwa sasa lazima ziendelezwe; na Rais Magufuli ametuthibitishia anastahili kuendeleza jitihada hizi,” Warioba.

Makala haya yameandaliwa na timu ya kampeni za Chama cha Mapinduzi.

Kulingana na sera yetu ya uandishi wa habari za uchaguzi, wagombea wa vyama vyote au timu zao za kampeni wanakaribishwa kuandika makala na maoni, ilimradi ziwe katika lugha ya staha na zisizoshambulia washindani wao.


Advertisement