Bilionea Bloomberg chachu mpya kampeni za uchaguzi Marekani

Wednesday November 27 2019

 

By Reginald Miruko na Mashirika

Kujitosa kwa bilionea na mmiliki maarufu wa vyombo vya habari katika uchaguzi mkuu wa Marekani kwa vyovyote vile ni mtikisiko wa aina yake.

Michael Bloomberg, mmoja wa waanzilishi na ofisa mtendaji mkuu wa kampuni ya habari ambayo pia inakwenda kwa jina lake, Bloomberg News, ametangaza kujitosa katika kinyang’anyiro cha urais wa Marekani.

Alitangaza uamuzi huo Jumapili alipohutubia umati wa wafuasi wa Democrats na kueleza nia yake ya kurithi nafasi ya Donald Trump, huku akiahidi “kuijenga upya Marekani.”

Kufuatia uamuzi huo ambao umetikisa siasa za Marekani, Mtandao wa Bloomberg News Jumapili ulichapisha mabadiliko kadhaa katika safu ya uhariri, ikiwa ni maandalizi ya jinsi ya kuandika habari za bosi na mmiliki wa mtandao huo maarufu duniani, akiwa anawania nafasi ya juu kabisa ya nchi hiyo.

Meya huyo wa zamani wa New York alithibitisha kuingia katika kinyang’anyiro hicho cha kurithi nafasi ya bilionea mwenzake wa New York, Rais Trump, miezi mitatu tu kabla ya kura za maoni.

“Hakuna namna tunaweza kudai kuwa itakuwa rahisi kuandika habari za kampeni hizi za urais,” alisema John Micklethwait, mhariri mkuu wa shirika la habari la Bloomberg, katika barua pepe iliyotumwa kwa wafanyakazi.

Advertisement

Alinukuu sera ya uhariri ya kampuni hiyo kuhusu kutoandika habari zao wenyewe wala za washindani wao.

Micklethwait alieleza mabadiliko kadhaa yatakayofanyika katika bodi ya uhariri ya shirika hilo, lakini akisisitiza kuwa wataandika habari za kampeni kulingana na tukio husika, lakini si kwa kuwa kanuni ya jumlajumla.

“Katika eneo ambalo Mike (Bloomberg) alikuwa na fursa ya moja kwa moja na uhariri ni kona ya “maoni ya Bloomberg; maoni hayo yamekuwa yanaakisi mawazo yake,” amesema Micklethwait akifafanua kuwa kampuni itasisitiza sera ya kuchapisha maoni yasiyokuwa na jina la mwandishi.

Pia, wataisimamisha kazi bodi nzima ya uhariri kwa kuwa wajumbe wake wengi watachukua likizo za muda kujiunga na kampeni za Bloomberg.

Micklethwait amesema wanatarajia kuandika habari za kampeni hizo, kama vile ambavyo wamekuwa wakifanya kabla, isipokuwa tu watakuwa wanaeleza wazi kuwa mmiliki wa Mtandao wa Bloomberg News ni mgombea.

Katika ujumbe huo, Micklethwait aliongeza kuwa hawatachunguza familia ya Bloomberg au taasisi zake, vilevile hawatafanya hivyo kwa washindani wake wa Democrats; lakini watachapisha kwa ufupi uchunguzi huo kwa wagombea wote wa Democrats.

“Bloomberg News iliwahi kufanya shughuli kama hii hapo awali,” aliandika Micklethwait, akikumbushia kampeni za umeya pale shirika hilo lilipotumia sera kama hiyo.

Bilionea Bloomberg anajipanga kugombea akiwa na mlengo wa kati, na wachambuzi wanasema anaweza kubeba baadhi ya mashabiki wa Joe Biden ambaye pia ni wa mlengo huo.

Wachambuzi hao wanasema taswira aliyojijenga na msaada wake katika masuala ya mabadiliko ya tabia nchi yanamfanya kuwa mpinzani mkubwa wa Trump katika uchaguzi wa 2020.

Utajiri wake binafsi wa Dola50 bilioni za Marekani (Sh11.5 trilioni) unaweza kutikisa mchakato unaoendelea wa kinyang’anyiro cha rais kupitia Democrats, hasa baada ya kutangaza nia yake, ikiwa ni miezi mitatu tu kabla ya kura za maoni.

“Lazima tushinde uchaguzi huu. Na tunatakiwa kuanza kuijenga upya America,” alisema Bloomberg mwenye umri wa miaka 77 kwenye mtandao wake, huku matangazo ya kampeni ya Dola 30 milioni yakirushwa hewani.

Advertisement