Catherine Nyakao Ruge, jicho la Chadema katika masuala ya fedha

Miongoni mwa wabunge ambao michango yao hutikisa bungeni ni Catherine Nyakao Ruge.

Huyu ni mbunge wa Viti Maalumu kupitia Chadema, msomi aliyebobea katika masuala ya biashara na uchumi na anayetumia elimu yake katika michango yake bungeni na kuiinua kambi ya upinzani.

Lakini mara nyingine michango hiyo humweka matatani na pengine hilo humfanya pia ajulikane yeye ni nani.

Hivi karibuni aliingia matatani baada ya mchango wake ulionukuu ripoti ya Shirika la Uhifadhi Duniani (WWF) iliyoandaliwa na mtafiti George Hartmann, ikieleza kuwa “kiuhalisia gharama za ujenzi wa mradi wa umeme wa Stiegler ni Sh21 trilioni”.

Mbunge huyo alitakiwa na Naibu Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson awasilishe vielelezo kwenye Kamati ya Maadili, Haki na Madaraka ya Bunge, jambo ambalo anasema alilitekeleza.

Si hilo tu, katika Bunge la Februari iliamuliwa mchango wake kuhusu ukaguzi wa Mkaguzi na Mdhibiti mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) katika mfuko mkuu wa Serikali ufutwe kwenye kumbukumbu za Bunge kwa sababu za kikanuni.

Ukisikiliza michango hiyo na mingine ya mbunge huyo huwezi kuacha kujiuliza huyu nini nani?

Michango yake

Kuhusu michango yake bungeni, anasema yeye na mbunge wa Moshi Vijijini, Anthony Komu ndiyo wachambuzi wa masuala ya fedha na ukaguzi ndani ya kambi ya upinzani.

Anasema tangu amekuwa mbunge amekuwa akitoa mchango mkubwa kwa wabunge wa upinzani katika kitengo cha fedha na hajawahi kutetereka.

Hoja zake

Akijibu kuhusu baadhi ya hoja zake ambazo husababisha atiwe msukosuko na kutakiwa ushahidi, mbunge huyo anasema kila anachozungumza kimekuwa cha kweli na chenye ushahidi.

“Pale wamekuwa wakitafuta kupotosha ukweli kupitia miongozo, taarifa na mara ushahidi, lakini kila nikipeleka ushahidi wanakaa kimya bila kueleza kilichomo na wala sijaitwa kwenye kamati,” anasema.

Ruge anasema yeye amesimama katika taaluma zaidi kuliko vitu

vingine na anakesha akisoma na kuandaa nyaraka kwa ajili ya kambi ya upinzani.

Alivyoteuliwa

Akivuta kumbukumbu hadi siku ya uteuzi wake, Nyakao anasema “Nilijifinya mara tatu nisiamini kama nimekuwa mbunge. Maana ilikuwa yangu ndoto kuingia jengo lile. Hata hivyo, namshukuru Mungu na wananchi wa Serengeti.”

Nyakao aliteuliwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi Mei 4, 2017 kuwa mbunge baada ya kifo cha aliyekuwa mbunge wa Viti Maalumu, Dk Elly Macha.

Katika mahojiano na Mwananchi hivi karibuni, mbunge huyo anasema ndoto ya ubunge alikuwa nayo lakini uhalisia ilikuwa vigumu kuifikia licha ya kuungwa mkono kila pande.

Anasema safari ya maisha yake ilikuwa ndefu na amepita milima na mabonde hadi na anaona bado anahitaji kwenda mbele zaidi.

Mwanamama huyu ambaye anabebwa na maneno mawili, ‘siogopi, najiamini’ , anasema siku moja kabla ya uteuzi, aliitwa na viongozi wa Chadema akitakiwa kujaza fomu na kuandika wasifu wake (CV) lakini hakuambiwa kitu hadi siku iliyofuata aliposikia jina lake linatangazwa.

Maisha yake

Mbunge huyo anasema anatoka katika familia ya wafugaji na alikulia katika tabaka la chini, ingawa baba yake alikuwa ni hakimu.

Safari yake kielimu ilianzia mkoani Mara 1990 alikoanzia darasa la kwanza kabla ya kuhamishiwa jijini Dar es Salaam baada ya kifo cha baba yake, yeye akiwa na umri wa miaka sita.

Kabla ya kifo hicho, baba alitaka kumsomesha kuwa daktari, lakini ndoto ilifutika na maisha yaliishia kuwa chini ya dada yake, ambaye ni fundi cherehani.

Nyota yake iling’ara alipomaliza darasa la saba akichaguliwa kujiunga kidato cha kwanza (1997) katika Shule ya Wasichana Msalato ambayo huchukua wenye ufaulu wa juu na baadaye kidato cha tano katika Shule ya Jangwani, Dar es Salaam, kisha Chuo kikuu Dar es Salaam alikosomea biashara na mahesabu.

Maisha ya siasa

Nyakao alijiunga na Chadema mwaka 2010. Akiwa UDSM mwaka 2005, anasema alikuwa miongoni mwa vijana walioshiriki harakati katika Jimbo la Ubungo wakimsaidia John Mnyika kuwa mbunge.

“Katika familia yetu asilimia 90 ni wanachama wa CCM, lakini niliona kijana mwenzangu Mnyika (John) ametoa ushindani mkali jimbo la Ubungo, nikaanza kujiingiza kwenye siasa kidogo kidogo, mwisho nikaamua kujiunga na chama hicho,” anasimulia.

Mbali na Mnyika (mbunge wa Kibamba), anamtaja Zitto Kabwe ambaye alimfuata hadi nyumbani kwa mama yake akitaka kujua mbinu za kutumia awe mwanasiasa mzuri. Pia anamtaja Habibu Mchange kwamba alimtia moyo kabla ya kujiunga na kundi la Hynes Kiwia (aliyekuwa mbunge wa Ilemela).

Barabara ndefu haikosi kona, Nyakao anasema alikutana na misukosuko mingi ndani ya siasa, lakini alipasua mawimbi hata kufikia kutambulika maeneo mengi.

Kugombea ubunge

Awali, Ruge anasema kugombea ubunge halikuwa wazo la kipaumbele, lakini alitaka kuwa mtu wa kupanda majukwaani na kuzungumza kutokana na taasisi iliyokuwa ikifanya kazi za kijamii kutetea wasichana mkoani Mara.

“Lakini mwaka 2014 mjomba wangu aliniita kutoka Dar es Salaam, nilipofika Musoma akaniambia watu wanakutaka ugombee Ubunge Serengeti. Niliwaza sikupata jibu la moja kwa moja lakini nikakubali.

Pamoja na kukubali, hakugombea kwa sababu alikuta chama kina nguvu na kulikuwa na wenzake waliokuwa wamekijenga, hivyo akaheshimu taratibu za chama na kumpisha Marwa Chacha (alishinda, sasa amerudi CCM), na yeye akapitia kundi la wanawake akashika nafasi ya 38 lakini uteuzi wa viti maalumu ukaishia nafasi ya 37. Yeye akabaki kando hadi alipopata fursa baada ya kifo cha Macha.

Baada ya kuingia mjengoni alichokiona anasema kilikuwa nje ya matarajio.

“Nilipokalia kiti kwa mara ya kwanza niliona shida. Watu wanaoitwa wabunge wanapiga kelele hadi Spika anaingilia kati lakini tunashindwa kuzungumzia mambo ya msingi badala tunazomeana na kupiga kelele huku ushabiki wa vyama ukitawala, inaniuma,” anasema Ruge

Anasema hali hiyo imekuwa ikimuumiza na kufanya aone ndoto ya kuwasaidia Watanzania katika Bunge la 11 bado hajaipata zaidi ya kushuhudia wabunge kwa pande zote wakiwa kwenye zomeazomea.

Nafasi ya upinzani

Pamoja na hali iliyopo, Nyakao bado anaamini upinzani unayo nafasi kubwa katika uchaguzi mkuu wa mwakani wakibebwa na kura tatu, yeye akitamba kulichukua jimbo la Serengeti.

Akifafanua kuhusu kura hizo, anasema watabebwa na huruma, pili, wasiounga mkono serikali kwa yaliyofanyika na tatu ni uwezo wa vyama vya upinzani kwa namna walivyopita na kuhimili misukosuko.

Bado anaamini umoja wa upinzani utawavusha kwenye uchaguzi 2020 na kuwa kimya kingi cha Watanzania mshindo wake utakuwa mkubwa kwenye kura.

Wabunge wa kuigwa

Ruge anatamani kufanya kazi na Mbunge wa Nzega , Hussein Bashe na mbunge wa viti maalumu, Zawadi Koshuma, wote wa CCM, kwamba wanasimama kutetea hoja badala ya vyama na wanafanya uchambuzi wa hoja zao.