KALAMU HURU: Kama hawajapikwa wasipewe vijana madaraka makubwa

Katibu mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally ametumbua jipu linalosumbua ndani ya chama hicho na serikalini akisema baadhi ya viongozi vijana hawakupikwa kiuongozi.

Maoni yake yameungwa mkono na baadhi ya viongozi wastaafu, wakieleza janga lililopo la uongozi tofauti na zamani ambapo vijana walipikwa vyuoni kuhusu maadili ya uongozi.

Jambo la kujiuliza, kama vijana wa siku hizi hawapikwi, kwa nini wanaaminiwa kupewa madaraka mazito hivi? Hivi mwenye kosa ni nani, ni hao wanaopewa madaraka au anayewapa madaraka hayo?

Maana hakuna mtu anayezaliwa akiwa anajua kuongoza. Ni lazima watu wafundishwe misingi ya uongozi na ikiwezekana wapelekwe vyuoni wapewe mafunzo ya muda mrefu.

Tatizo lilianza baada ya Tanzania kuingia kwenye mfumo wa vyama vingi. CCM iliyokuwa ikipika viongozi ikajikuta kwenye ushindani mkali na vyama vingine. Kwa hiyo ule muda wa kupika watu ukaonekana kama utakuwa unachelewesha mambo.

Ndani ya chama chenyewe kulikuwa na ushindani mkali wa makundi ya wasaka urais na kila kundi lilikuwa na wapambe na wapiga debe ambao wana matarajio ya kuteuliwa huku na kule. Mheshimiwa akishateuliwa na chama na hatimaye kushinda urais ndio wanateuliwa.

Hao wateuliwa si vijana tu, wengine ni watu wazima kabisa. Kazi yao ni moja tu, kumfurahisha aliyewateua. Hata watu wakilalamika kuwa hawakupikwa, hiyo si kitu kwao.

Rais anateua viongozi wa majeshi ya ulinzi na usalama, majaji, makatibu wakuu, katibu wa Bunge na wabunge 10, anateua hadi viongozi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi ambao humsimamia akiwa mgombea.

Angalau uteuzi wa waziri mkuu tu ndiyo hufikishwa bungeni kupigiwa kura, lakini viongozi wengine karibu wote anawateua bila ushauri wa mtu yoyote.

Ndiyo maana viongozi wa kuteuliwa wana nguvu kuliko hata waliochaguliwa na wananchi. Wananchi ambao ndiyo msingi wa madaraka ya Serikali hawana la kusema kwa wateule wa Rais.

Madaraka haya ya Rais ndiyo yanawalevya hata baadhi ya makada wa vyama vya upinzani, ndiyo maana utashangaa wakishahamia CCM wanateuliwa huku na kule, yaani wanakuwa na uhakika na kule wanakokwenda. Ni kama njia inayotumika kudhoofisha upinzani.

Hapo ndipo tunapoona umuhimu wa kuwa na mabadiliko ya Katiba yatakayompunguzia Rais madaraka yakiwemo ya kuteua viongozi. Viongozi wa kuteuliwa wapunguzwe na hao wanaoteuliwa majina yao yapitie kwenye mchujo ambao maoni ya wananchi yachukuliwe.

Tunaweza kuiga mfano mzuri wa Katiba ya Kenya ambapo baadhi ya wateuliwa wa Rais inabidi waombe kazi na wanapitia mchujo mkali, siyo kuteuliwa tu. Kwa nini Tanzania isiwezekane?