Mkataba wa uchaguzi wa demokrasia ulivyo mfupa mgumu kwa Tanzania

Wakati Tanzania ikielekea kwenye Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 2020 utata umebaki kuhusu kutosainiwa kwa mkataba wa Umoja wa Afrika unaohusu uchaguzi, demokrasia na utawala bora (ACDEC).

Mkataba huo uliopitishwa na nchi wanachama wa Umoja wa Afrika mwaka 2007 mjini Addis Ababa, Ethiopia unaweka miiko, kanuni na viwango vilivyokubaliwa na nchi za Afrika vikiwamo vya demokrasia na kuheshimu haki za binadamu, utawala wa sheria, Katiba na kufanya chaguzi za kidemokrasia zenye haki.

Vigezo vingine vilivyopo katika mkataba huo ni kukataza mabadiliko ya serikali kinyume na Katiba, utetezi na ulinzi wa mahakama, maendeleo endelevu na ulinzi wa binadamu, kuongeza ushiriki wa wananchi, uwazi na uwajibikaji katika masuala ya umma.

Kwa mujibu wa tovuti ya Umoja wa Afrika, tangu mkataba huo ulipopitishwa, nchi 30 zimeshatia saini na kuridhia ambazo. Nchi hizo ni Algeria, Benin, Burkina Faso, Cameroon, Chad, Comoros, Côte d’Ivoire, Djibouti, Ethiopia, Ghana, Guinea, Guinea Bissau, Lesotho na Liberia.

Nyingine ni Madagascar, Malawi, Mali, Mauritania, Namibia, Niger, Nigeria, Rwanda, Jamhuri ya Sahrawi, Seychelles, Sierra Leone, Africa Kusini, Sudan Kusini, Sudan, Togo na Zambia.

Mbali na nchi zilizoridhia mkataba huo, nyingine 19 zilizasaini lakini hazijaridhia ambako ni pamoja na Angola, Burundi, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Cape Verde, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Equatorial Guinea, Gabon, Gambia, Kenya, Msumbiji, Mauritius, Senegal, Somalia, Sao Tome & Principe, Eswatini Tunisia, Uganda na Zimbabwe.

Tanzania inabaki miongoni mwa nchi sita ambazo hazijasaini wala kuridhia mkataba huo mpaka sasa ikiwa pamoja na Botswana, Misri, Eritrea, Libya na Moroco.

Ni bahati mbaya kuwa wakati mkataba huo haujasainiwa, madai ya ukandamizaji wa demokrasia na utawala bora nchini yameendelea kutolewa na vyama vya upinzani, asasi za kiraia na vyombo vya habari.

Miongoni mwa malalamiko ya wadau hao ni kupigwa kwa marufuku kwa mikutano ya hadhara na maandamano, kutungwa kwa sheria zinazodaiwa kuminya haki za kidemokrasia na uhuru wa maoni kama ile ya huduma za habari ya mwaka 2016, Sheria ya Makosa ya Mitandao ya mwaka 2015 na Kanuni za maudhui ya mitandao (Epoca).

Kauli ya Serikali

Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Augustine Mahiga anasema suala la kusainiwa mkataba huo linasimamiwa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na kama ni kuridhiwa ni suala la mchakato wa kiserikali.

“Ukizungumza na watu wa Mambo ya nje wanaweza kukueleza. Hii ratification (kuridhia) nadhani ni procedural (mchakato) tu.

“Tuna process ambayo kisheria ni nzuri, wizara inayohusika inatayarisha andiko inapeleka kwa katibu mkuu kiongozi, anaitisha kikao cha makatibu wakuu wezake, wanajadili, baada ya hapo linapita kwenye cabnet, basi linakuja bungeni,” anasema Dk Mahiga.

Anaendelea kusema, “Labda priorities (vipaumbele) za mikataba na mambo mengine ya kiserikali yana chukua nafasi, lakini sidhani kama kuna sababu za kisiasa kutokusaini.”

Anasema kuna mikataba mingi ambayo Serikali imeitia saini lakini haijaridhiwa.

“Sasa hivi tuna mchakato wa makusudi kabisa kujaribu kuharakisha ratification ya mikataba mbalimbali ambayo tumesaini. Nadhani hivi karibuni utakuwa umeona tume-ratify huu na huu,” amesema.

Kwa upande wake Waziri wa Nchi Katika Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, George Mkuchika anasema licha ya mkataba huo kutosainiwa, Serikali imekuwa ikitekeleza vigezo vya utawala bora.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Mtumba jijini Dodoma hivi karibuni, waziri Mkuchika amehusisha utekelezaji huo na mpango wa kujitathmini kiutawalabora (APRM).

“Ukiangalia ACDEG ni suala la utawala bora ambalo linafanana na APRM, ndiyo kujitathmini kwenyewe. Pamoja na mpango wa Afrika wa kujitathmini, Tanzania ilikuwa mwanachama wa Mpango wa kuedensha Serikali kwa uwazi (OGP) ulioasisiwa na Rais mstaafu wa Marekani,

Barrack Obama,” anasema Mkuchika.

“Tanzania ilijitoa na kubaki kwenye APRM kwa vile taasisi zote zina malengo yanayofanana. Vyombo hivyo ni vingi na Taifa linapoingiza kuna gharama zake mnawajibika kulipa ada ya kila mwaka japo kazi zinazofanyika zinafafana,’ ameongeza Waziri Mkuchika.

Hata hivyo, Waziri Kivuli wa Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala bora, Ruth Mollel anasema suala la kuridhia au kutoridhia ni sawa na kazi bure kwa sababu hata Katiba ya Jamhuri ya Muungano haiheshimiwi.

“Hivi Katiba inazingatiwa? Tuanzie hapo, kanuni zinazingatiwa? Kama sisi wenyewe hatuwezi kuzingatia, Katiba tuliyoandika, tutakwenda kuhangaika na protocol tusizoandika? Charity begins at home (ukarimu huanzia nyumbani),” anasema Mollel.

Anaongeza, “Sasa kama Katiba hatuangalii, uhuru wa maoni, wa kuzungumza hakuna, ndiyo tutakwenda kuzungumza hayo? Mimi sioni. Nasema charity begins at home.”

Mollel ambaye ni mbunge wa viti maalum (Chadema), anasema ameshauri kwanza kupigania haki za kidemokrasia na utawala bora kabla ya kwenda kupigania mkataba huo.

Hata hivyo, anasema kama mkataba huo utatakiwa uletwe na wizara husika na ukifika bungeni Kambi Rasmi ya upinzani bungeni itatoa maoni yake.

“Kuridhia lazima wizara inayohusika wailete na sisi turidhie. Wakiuleta upinzani tunatoa maoni yetu, kamati inayohusika ya mambo ya nje wanatopa maoni yao halafu kama kuna vipengele ambayo hatukubaliani navyo au kama tunakubali ndiyo tunaridhia,” anasema.

Madai ya tume huru ya uchaguzi

Licha ya Serikali kusisitiza kuwa uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba, mwaka huu utakuwa huru na wa haki, utata uliobaki ni uhuru wa Tume ya Taifa ya uchaguzi (NEC) ambayo uongozi wake wote umeteuliwa na Rais ambaye pia ni mwenyekiti wa CCM.

Akisisitiza madai hayo bungeni jijini Dodoma Februari 6, Kiongozi wa Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe alimuuliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kuhusu kupatikana kwa Tume huru ya uchaguzi na hatua ya vyama vya siasa kuzuiwa kufanya mikutano ya hadhara na maandamano.

Akijibu swali hilo, Waziri Mkuu Majaliwa aliitetea Tume huru ya uchaguzi akisema imeundwa kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano na haiwezi kuingiliwa na mamlaka yoyote.

“Tume hii imeundwa kwa mujibu wa Katiba kipengele 74(7,11, 12) inaeleza kuwa hiki ni chombo huru.

“Imeeleza kwenye Katiba pale kinaundwaje na chombo hiki hakipaswi kuingiliwa na chombo chochote, iwe Rais, chama chochote cha kisiasa au mamlaka nyingine haipaswi kuingilia. Kama ni chombo huru kwa mujibu wa Katiba ndiyo tume huru,” alisema waziri Mkuu Majaliwa.

Ahadi ya kufanyika kwa uchaguzi ulio huru na wa haki, imerudiwa Februari 26 na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Profesa Palamagamba Kabudi wakati akihutubia kikao cha 43 cha Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa linaloendelea jijini Geneva, Uswisi likiwakutanisha wadau kutoka sehemu mbalimbali duniani.

“Mwaka huu Tanzania itafanya uchaguzi mkuu wa sita tangu kuanzishwa kwa vyama vingi vya siasa utakaokuwa wa uwazi, huru na wa haki,” alisema Profesa Kabudi

Lakini akizungumzia suala la ‘uhuru wa uchaguzi’ kama ilivyogakikishwa na Rais John Magufuli wakati akizungumza na mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao nchini Januari 21, Mwenyekiti wa zamani wa Jukwaa la Katiba, Deus Kibamba amesema, “Nadhani Rais Magufuli alikuwa anafanya siasa tu.”

Huku akirejea matukio ya kisiasa yaliyotokea nchini, Kibamba alisema “juhudi zinazofanyika kwa sasa ni kuelekea gizani kabisa.

“Kuna mifano mingi inayoonyesha kwa sababu tumeua michakato yote ya uwazi kwa mfano Open Governance Partnership (OGP), tumeua APRM (Mpango wa Afrika wa kutathjmini kiutawala bora), kulikuwa na African Charter on ACDEG Mkataba wa Afrika wa demokrasia, uchaguzi na utawala bora).

“Sasa kama mtu mkataba wa Afrika wa mambo ya uchaguzi demokrasia na utawala nchi imegomea kuutekeleza, halafu kiongozi aseme uchaguzi utakuwa huru na wa haki? Tutaupima kwa vigezo gani?” alihoji.