Mwanajeshi wa Uganda aua afande wake

Wednesday May 15 2019

 

Kampala. Uongozi wa Jeshi la Uganda, wakishirikiana na uongozi wa kikosi cha wanajeshi wa Muungano wa Afrika wanaolinda amani nchini Somalia (Amisom), wanachunguza tukio la mwanajeshi wa Uganda, aliyemuua kiongozi wake na wanajeshi wenzake wawili kabla ya kujiua.

Uganda inasema mwanajeshi huyo alifyatua risasi kiholela na kuua wenzake wote waliokuwa katika sehemu ya tukio, kikiwa kisa cha kwanza kwa mwanajeshi wa Uganda kuua wenzake wakiwa kazini, nje ya nchi.

Tukio hilo la Jumamosi, kwenye makao makuu ya Jeshi la Amisom nchini Somalia limetajwa na maofisa wa Jeshi la Uganda kuwa la kushtukiza, bila kutoa sababu kamili wala kutaja majina ya wahusika, wakisema uchunguzi wa kina unaendelea.

Japo kuna taarifa kwamba ofisa huyo wa jeshi alikuwa ameudhiwa na mkubwa wake, na kulikuwapo uhusiano mbaya wa kikazi kati yao, naibu msemaji wa Jeshi la Uganda (UPDF), Luteni Kanali Deo Akiiki amesema wachunguzi kutoka Uganda wamekwisha wasili na wameanza uchunguzi kwa kushirikiana na uongozi wa Amisom.

Hili ni tukio la kwanza kwa mwanajeshi wa Uganda kuua kiongozi wake. Ni mara ya kwanza pia kwa mwanajeshi wa Uganda kushambulia wenzake na kuwaua wakiwa nje ya nchi kazini.

Matukio ya wanajeshi wa Uganda kuua raia au wenzao kufuatia mzozo wa kifamilia, mapenzi, umiliki wa mali, sababu zisizojulikana ni kawaida nchini Uganda.

Mwaka 2018, mwanajeshi Isaac Okello alihukumiwa kifungo cha miaka 80 kwa kumuua mama mjamzito, mumewe na mtoto wao wa kiume katika wilaya ya Alebtong, kaskazini mwa Uganda.

Mwaka 2016, Sagenti Isaac Obua, aliua wanajeshi wenzake saba katika kambi ya Makindye jijini Kampala.

Advertisement