Mzee Sumaye hajanikomesha, hatanikomesha

Monday December 9 2019Julius Mtatiro

Julius Mtatiro 

By Julius Mtatiro

Uamuzi wa Waziri Mkuu Mstaafu Mzee Fredrick Sumaye kutangaza kuachana na Chadema na kutoeleza uelekeo wake wa moja kwa moja kisiasa haujanikomesha hata kidogo, ni uamuzi uliosaidia kuonesha kuwa yale ambayo niliyachambua yako karibu kutokea.

Awali katika uchambuzi wangu kwenye safu hii wiki iliyopita nilieleza kuwa Mzee Sumaye hatakuwa na chaguo lolote zaidi ya kuamua kule alikokulia na kukuzoea yaani CCM, tangazo lake la hivi karibuni kwamba anaondoka Chadema na hajiungi na chama kingine cha siasa bado halijabadilisha mtizamo wangu juu ya siasa za mbele za Mzee Sumaye.

Baada ya tangazo la Mzee Sumaye, baadhi ya wasomaji wangu waliniletea ujumbe mfupi kwa njia ya WhatsApp na kuniambia utabiri wangu haujatimia na haukuwa sahihi. Watu wa aina hiyo wanaamini kuwa Mzee Sumaye ameshahitimisha mipango yake ya kisiasa, jambo ambalo nalitizama kinyume chake.

Kisichojulikana kwa wengi kwa kawaida kimo kwenye uchambuzi siyo utabiri. Mambo yatokeayo mbeleni kwa uhakika hutegemea uchambuzi wa mambo mbalimbali uliofanywa kabla, mambo yatokeayo mbeleni hayawezi kuwa ubashiri kwa sababu ubashiri hauwezi kuwa uchambuzi, ubashiri ni mchezo wa pata potea wakati uchambuzi ni kitu kipana ambacho mara nyingi hujaribu kuweka mahaba pembeni.

Kwa kumbusho tu, uchambuzi wangu wa toleo lililopita kwenye safu hii ulizungumzia uzoefu na ugumu mkubwa uliomo ndani ya mifumo ya siasa za upinzani, mfumo na ugumu ambao hupelekea kukawa na misigano mingi ya kimadaraka ndani ya vyama hivyo. Na nilisisitiza kuwa, vyama vya upinzani vya Tanzania vina mapigano na mapambano makubwa ya ndani kuliko mpambano ambayo vinafanya nje dhidi ya chama tawala.

Uelekeo Mpya wa Sumaye ni upi?

Advertisement

Mzee Frederick Sumaye, pamoja na mambo mengine wakati akiiaga Chadema hivi majuzi, na kueleza kuwa hajiungi na chama chochote cha siasa, alisisitiza kuwa yuko tayari kuwa mshauri wa masuala ya kisiasa, lakini hakueleza katika kukwaa lipi la kisiasa.

Kwa kawaida, huwezi kuwa mshauri wa masuala ya kisiasa bila kuwa na mrengo au chama ambacho unakoshauri kuhusu sera na mwenendo wake, kwa sababu Mzee Sumaye anataka kuwa mshauri wa masuala ya kisiasa, kama hatajiunga na chama kingine ni vigumu kuifanya kazi hiyo, labda atapaswa kuwa mchambuzi wa masuala ya kisiasa, kazi ambayo haifungwi na ikiwa anayeifanya yumo kwenye chama cha siasa au la!

Kwa kawaida washauri wa masuala ya kisiasa huifanya kazi hiyo kitaaluma, ni watu waliokaa darasani na kusoma siasa kwa mapana yake na hutumia uzoefu huo wa darasani kujenga milinganisho na kutoa maelekezo kwenye siasa halisi ambazo vyama au wadau wengine wanashiriki.

Je, atakwenda ACT?

Ziko tetesi na mahitimisho mengi kuhusu kauli ya Mzee Sumaye kwamba hatajihusisha na siasa za chama chochote. Kwa kawaida katika maisha unapofanya maamuzi fulani bila kutoa mwelekeo uliokamilika ni rahisi kuwafanya watu waanzishe mahitimisho ya binafsi, watu hawa hawapaswi kuhukumiwa kwa sababu wanajaza ombwe lililoachwa.

Lakini tetesi hizi haziwezi kupuuzwa, haifahamiki kwa haraka mzee Sumaye anataka kufanya nini katika siasa za upinzani. Kabla hajaondoka Chadema alichukua fomu ya kugombea uenyekiti wa chama hicho na imeshaelezwa kuwa hiyo ndiyo sababu kubwa iliyofanya apigiwe kura za hapana katika uchaguzi mwingine wa ngazi ya chini ambapo Mzee Sumaye alikuwa akisaka uenyekiti wa kanda wa Chadema.

Ikiwa ni kweli mzee Sumaye atajiunga ACT Wazalendo, nadhani atafanya hivyo ili kuwezesha masuala kadhaa, kwanza labda itakuwa ni kutimiza azma yake ya siku moja kufanikiwa kuwa pia kiongozi wa upinzani nchini Tanzania, kama alivyojaribu kutafuta nafasi hiyo Chadema bila mafanikio.

Lakini wachambuzi wa mambo wanaeleza kuwa huenda Mzee Sumaye anataka kupata nafasi ya kugombea urais wa Tanzania kupitia chama chochote cha upinzani japokuwa yeye mwenyewe kwa kinywa chake amekuwa akirudia mara nyingi kuwa hahitaji kabisa kiti cha Urais.

Naamini, ikiwa ni kweli Mzee Sumaye ana nia ya kuendeleza harakati zake za kisiasa ndani ya ACT, labda kwa kuanza kama mshauri na baadaye kugombea wadhifa fulani, yale yale yaliyomkuta Chadema yatamkuta huko huko ACT.

Uzoefu wangu na siasa za upinzani nchini Tanzania unathibitisha kuwa kwenye upinzani kuna vyama ndani ya vyama, kuna chama cha nje na chama cha ndani, ndani ya chama kimoja kuna makundi mengi yanayofanya maamuzi mbalimbali kwa maslahi za kimakundi badala ya chama. Na kubwa zaidi, katika upinzani wa Tanzania, ziko nafasi ambazo hata uwe na sifa kumshinda kila mmoja ndani ya chama, hautokaa uzipate.

Julius Mtatiro ni Mkuu wa wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma. 0787536759. [email protected]

Advertisement