MAKALA YA MALOTO: Uhuru na Raila wanajenga daraja Kenya, kama lililovunjwa Zanzibar

Wednesday December 4 2019

 

By Luqman Maloto

Yapo mambo mengi yenye matumaini ya kuijenga Kenya mpya kupitia shabaha yao ya mabadiliko ya Katiba, yaliyopewa jina la Building Bridge Initiative (BBI), yaani mpango wa kujenga daraja.

Machi mwaka jana, Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta na mpinzani wake mkuu, Raila Odinga walishikana mikono na kukubaliana kuanza mwanzo mpya wa kuijenga nchi yao bila migawanyiko ya kisiasa, ukabila wala matabaka.

Machafuko au migogoro yenye kuibuka mara kwa mara vipindi vya uchaguzi ni sababu ya Uhuru na Raila kuketi kama Wakenya, wenye kuipenda Kenya na kuitakia kesho njema, wakazungumza na kuzika tofauti zao, kisha kupata mawazo yaliyofanikisha ripoti ya BBI.

Baada ya mazungumzo ya Uhuru na Raila, kiliundwa kikosi kazi cha wajumbe 14, kikapewa agenda tisa. Kikazunguka majimbo 47 ya Kenya ili kupata mawazo ya namna ambavyo Wakenya wangependa nchi yao iwe.

Agenda tisa ni kumaliza mgawanyiko wa kikabila, ushirikishwaji wa vyama vya upinzani katika muundo wa Serikali, jinsi ya kutatua misuguano ya uchaguzi, ulinzi na usalama na namna ya kupambana na rushwa.

Pia ni jinsi ya kushughulikia ukosefu wa moyo wa utaifa kwa wananchi, haki na uwajibikaji, mgawanyo sawa wa matunda ya nchi na kutanua nguvu ya mamlaka kwa wananchi na uwakilishi.

Advertisement

Ni agenda hizo zilisababisha kikosi kazi cha BBI kije na mapendekezo ya mabadiliko ya vifungu vya Katiba ya Kenya ya mwaka 2010, vipo vinapendekezwa kufutwa na vingine kubadilishwa.

Rais atachaguliwa kwa kura za majimbo kama Marekani. Hiyo itasaidia kuondokana na hulka za kufanya kampeni za kikabila na kugawa watu. Mpinzani mkuu wa kiti cha urais anaposhindwa, moja kwa moja anakuwa mbunge ili aitumikie nchi yake.

Daraja la Zanzibar

Walichokitengeneza Raila na Uhuru Kenya kilishafanywa Zanzibar mwaka 2010. Katiba iliandikwa na kuhalalisha Serikali ya Umoja wa Kitaifa. Miaka mitano ilipita salama, Uchaguzi Mkuu 2015 uliharibu jasho lililovuja na maarifa yaliyotumika kujenga Zanzibar ya maridhiano.

Rais wa Tatu wa Tanzania, Benjamin Mkapa, katika kitabu chake “My Life My Purpose”, anaeleza majuto yake kuhusu Zanzibar, kwamba tukio la ghasia na mauaji ya Zanzibar Januari 26 na 27, 2001, ni kovu lisilofutika kwenye uongozi wake.

Ni kumbukumbu hiyo ya Zanzibar, ghasia za kila uchaguzi, huku mgawanyiko wa wazi ukiwa kati ya CCM na CUF, pia kisiwa cha Unguja kikionekana kumezwa na CCM, halafu Pemba CUF, ndio mwanzo wa mawazo ya kuunda utawala wenye maridhiano.

Desemba 2005, Rais wa Nne wa Tanzania, Jakaya Kikwete, alipolihutubia Bunge, alisema ilikuwa vigumu kuitawala Pemba kupitia CCM kwa sababu kisiwa kizima kilichagua CUF. Hekima hizo ndizo zilijenga mawazo ya Zanzibar kuongozwa na Serikali ya Kitaifa.

Mwaka 2010 Serikali ya Umoja wa Kitaifa iliundwa na maisha yalikuwa salama kuliko wakati wowote ule tangu kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa mwaka 1992. Mwaka 2015 mambo yalibadilika. Hakuna aliyetaka kuwa msaidizi.

Pengine Kenya walijifunza kutoka Zanzibar jinsi daraja lililojengwa mwaka 2010 lilivyovunjwa mwaka 2015 kwa sababu ya uchaguzi, ndio maana wameibuka na mpango wa Rais akae madarakani miaka saba na asiongeze. Kwani anapotaka kuongeza hutaka ashinde kwa lazima, hivyo kuchafua nchi.

Pamoja na yote, Tanzania ina mengi ya kujifunza kutoka Kenya. Wapinzani Raila na Uhuru wanavyotazamana kwa tabasamu kila wanapoifikiria Kenya yao. Wanajenga daraja la kisiasa, kimakabila na majimbo ili kuunda Taifa lenye amani na maridhiano.

Waziri wa Mambo ya Nje, Palamagamba Kabudi, alikuwepo Boma, Nairobi, Uhuru alipopokea ripoti ya BBI. Kabudi aliwapongeza Uhuru na Raila, kisha akawaapiza Wakenya kuifia nchi yao kwa umoja. Kabudi ana wajibu wa kurudi nyumbani na mawazo ya kujenga daraja kama Wakenya.

Ni kwa sababu Tanzania inarudi nyuma kiushirikiano wa makundi ya kisiasa. Daraja limeshavunjwa, ukuta unajengwa na unaongezeka kimo. Si Zanzibar, si Tanzania Bara.

Advertisement