KALAMU HURU: Vita ya kiuchumi au dhidi ya demokrasia

Nimemsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda alipokuwa akizungumza katika mkutano wa kimataifa wa uwekezaji wa sekta ya madini uliofanyika hivi karibuni jijini hapa.

Alikuwa akizungumza kabla ya kumkaribisha Waziri wa Madini, Dotto Biteko ambaye naye alimkaribisha Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliyekuwa mgeni rasmi wa mkutano huo.

Makonda alisema kuna vita kubwa ambayo ilishatajwa na Rais John Magufuli inayoitwa vita ya kiuchumi.

Akasema katika vita hiyo kuna silaha 11 zinazotumiwa (na maadui), lakini kwa sababu ya muda alitaja silaha mbili tu ambazo ni demokrasia na silaha za kibaiolojia (biological weapon).

Hata mimi kwa sababu ya nafasi na kwa sababu ya muktadha wa makala hii nitajikita kwenye hii ‘silaha’ inayoitwa demokrasia.

Makonda alisema demokrasia ni silaha mbaya sana iliyofanya nchi nyingi za Afrika zikaendelea kuwa na migogoro na kushindwa kutumia rasilimali za nchi husika kuwanufaisha wananchi wa ke.

Alisema hata watu wanoatetea demokrasia, ukifuatilia nchini zao hawana na hata wanaotwambia tudai Katiba mpya ya nchi kwao hawajawahi uandika Katiba na wengine wana Katiba zina miaka mingi hawajawahi hata kuzitengeneza.

Japo RC Makonda hakuiweka hoja yake kinagaubaga, lakini inatosha kuonyesha dhamira yake kuwa demokrasia ni adui kwenye hiyo anayoiita vita ya kiuchumi.

Demokrasia ni neno lililotafsiriwa na wasomi wengi, lakini kwa ufupi ni haki ya wananchi kuchagua viongozi au vyama vya siasa wanavyotaka. Ni sehemu ya utawala bora unaohusisha uhuru wa kujieleza, uhuru wa vyombo vya habari, ambayo pia yapo katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano. Demokrasia itambuliwa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano katika ibara ya 8 (1) inayoitambulisha Tanzania ikisema Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni Nchi inayofuata misingi ya demokrasia na haki ya kijamii. Pia katika ibara ya 3 (1) ya Katiba hiyo inasema Jamhuri ya Muungano ni nchi ya kidemokrasia na ya kijamaa, yenye kufuata mfumo wa vyama vingi vya siasa.

Sasa hii vita anayoitaja Makonda inahusiana na ujenzi wa demokrasia? Kwamba watu wakichagua viongozi wao wanahujumu uchumi? Au kwamba watu wasiwe huru kuendesha shughuli za kisiasa?

Ni kauli inayotakiwa kufafanuliwa kwa kina, kwa sababu ni hatari kwa kiongozi kama Makonda asijue kuwa demokrasia imeruhusiwa na Katiba, halafu yeye aje aseme ni kitu kibaya.

Maana yake Makonda hajui kwamba mwaka 1992 Serikali iliruhusu mfumo wa demokrasia ya vyama vingi baada ya kufutwa mwaka 1965?

Hata vyama vingi vilipofutwa, bado Serikali iliendeleza uchaguzi hata kama Mwalimu Julius Nyerere alikuwa akigombea urais peke yake, lakini angalau alipigiwa kura. Wananchi walikuwa huru hata kupiga kura ya hapana, hiyo ndiyo demokrasia.

Inawezekana Makonda anahofia kuwa ikiwa mazingira ya demokrasia yakijengwa vizuri na kuweka tume huru ya uchaguzi, huenda chama chake kikawa hatarini kufutika kwenye anga za siasa za Tanzania.

Hiyo vita ya kiuchumi ni kisingizio tu. Makonda pia anahofia mabadiliko ya Katiba akilaumu watu wanaochochea akisema hata katika nchi zao (hakuzitaja) Katiba hazijabadilishwa.

Huo wote ni woga wa mabadiliko, ni hofu ya kuwapa fursa wananchi kuchagua viongozi wanaowataka, kwa kisingizio cha vita ya uchumi.