Wanaolilia upinzani ufe Tanzania wafikiri upya

Juni mwaka jana, raia wa Marekani ambaye ni mchambuzi wa siasa na masuala ugaidi, Malcolm Nance alitoa kitabu chenye jina “The Plot to Destroy Democracy”, yaani mpango wa kuua demokrasia.

Katika kitabu hicho, Nance anasema Vladimir Putin, ndiye Rais wa kwanza wa Urusi kuwa Rais wa Marekani.

Anaeleza kuwa urais wa Putin katika nchi hiyo yenye nguvu kubwa kiuchumi upo kwa Donald Trump alipomsaidia kwa kudukua mchakato wa uchaguzi mwaka 2016.

Nance anaeleza kuwa baada ya Trump kushinda, Putin ndiye amekuwa Rais wa Marekani, maana anafuata matendo na nyendo za rais huyo wa Urusi.

Kwamba mpango wa Putin kumsaidia Trump ulikuwa wa kuvuruga demokrasia ya Marekani.

Ndani ya kitabu hicho, mwandishi anatoa maonyo mbalimbali kuhusu matendo ya kuua demokrasia akisema linaonekana ni jambo rahisi, lakini ni mchakato wa kuijenga upya ni mrefu na mgumu.

Mifano ipo mingi. Tanzania ilipoharamisha mfumo wa vyama vingi vya siasa mwaka 1962, iliichukua miaka 30 kuurejesha mwaka 1992.

Haikuwa kuamua mara moja tu kwamba vyama vingi viwepo, bali ilichukua mchakato mrefu. Harakati nyingi zilifanyika na Serikali ilitumia fedha nyingi kuigharamia Tume ya Jaji Francis Nyalali ili kupata maoni ya wananchi.

Tangazo la kupiga marufuku vyama vingi lilitolewa mara moja chini ya amri ya Rais na vyama vikatoweka, lakini kuvirejesha ulikuwa mchakato mrefu. Katiba ikafanyiwa marekebisho. Mfumo wa utawala ukageuzwa.

Zamani jeshi lilikuwa linafungamana na CCM baada ya Tanu, baadaye ilibidi mabadiliko yafanyike ndani ya jeshi. Kukawa na mchakato wa kutenganisha mali za chama na Serikali.

Hivyo, tukubaliane na Nance kuwa kuvuruga demokrasia ni rahisi mno kuliko kuijenga.

Maombi ya vyama kufutwa

Kumekuwa na maneno ya hapa na pale kuhusu kufuta vyama vingi vya siasa. Wasemaji wa maneno hayo, ama kwa ulevi wa kisiasa na kunogewa nafasi walizoshikilia au kutojua, hutamka kwamba hawaoni ulazima wa vyama vingi.

Watu hao husema kwamba Rais John Magufuli anatosha, vyama vingine vya nini? Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila ni miongoni mwao. Aliwahi kusema vyama vyote vifutwe, kiundwe kimoja kinachoitwa Magufuli Ruling Party (Chama tawala cha Magufuli).

Hata hivyo, Katibu mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally ameonya mara kadhaa kuhusu kauli hizo. Ni muhimu kukumbushana na kuelekezana kuliko kuonya. Inawezekana wasemao maneno hayo hawajui athari zake.

Pengine wanaolilia vyama vingi vife, wao ndiyo wanavihitaji, lakini wamepigwa na upofu wa fikra na kushindwa kutambua kesho itakuwaje.

Je, wanaolilia vyama vingi vife leo wana madaraka makubwa kuliko mawaziri wakuu wa zamani, Fredrick Sumaye na Edward Lowassa? Wangetamani vyama vife wakati wakitembea na misafara ya ulinzi barabarani, mwaka 2015 wangekuwa wageni wa nani baada ya kuona CCM si mahali salama kwao?

Mwalimu Nyerere aliyepiga marufuku vyama vingi, ni yeye aliyevipigania virejeshwe miongo mitatu baadaye. Wanadhani Mwalimu alikuwa mjinga?

Hivi karibuni, Rais mstaafu wa Botswana, Ian Khama alitupa kadi ya chama kilichomwingiza madarakani cha Botswana Democratic Party (BDP) na kusema anakihama, kwa kile alichodai Rais wa sasa, Mokgweetsi Masisi anaendesha nchi vibaya.

Unadhani Khama angetamani vyama vingi vya siasa vife Botswana akiwa rais, yeye angekuwa mgeni wa nani leo? Wanaotamani chama kimoja Tanzania, wameshajiuliza kesho yao ya kisiasa itakuwaje?

Maisha ya kisiasa ni majalala! Ndio maana leo makatibu wakuu wastaafu CCM, Yusuf Makamba na Abdulrahman Kinana, wanalalamika kuchafuliwa majina na kuchonganishwa na Rais Magufuli.

Uchonganishi huo unafanywa na mtu ambaye hajawahi kuwa hata mjumbe wa Halmashauri Kuu Taifa (NEC) CCM.

Wazee hawa wanalalamika kuwa wamekaa kimya kusubiri hatua ambazo zingechukuliwa na uongozi wa CCM dhidi ya huyo mchonganishi, lakini hakuna chochote kimefanyika ndiyo maana wameandika waraka.

Hao wazee walikuwa injini ya chama kwa nyakati zao. Hata hivyo, wakati wa sasa wanabaki kuwa walalamikaji. Wanaolilia vyama vifutwe, wajipime ubavu kama msuli wao unazidi waliokuwa nao Kinana na Makamba.

Vyama vya upinzani ni salama ya wanasiasa. Mfumo wa vyama vingi ungekuwapo mwaka 1967, Oscar Kambona asingekimbilia Uingereza baada ya kutofautiana kiitikadi na Nyerere. Angehamia chama kingine.

Na pengine Nyerere asingekubali Kambona aondoke Tanu, badala yake wangeketi naye kumaliza tofauti zao, maana kuhamia chama kingine kungehatarisha utawala wake. Tanu ingepasuka na kuna chama kingeimarika.

Kuanzia mwaka 2011, CCM walianzisha kampeni ya kujivua gamba. Shabaha ilikuwa kuwafuta uanachama waliokuwa na kashfa za ufisadi. Lowassa alitajwa sana.

Mbona hakufukuzwa na kampeni ya kujivua gamba ikajifia? Jibu ni kwamba, kulikuwa na hofu kuwa wangemtimua, angehamia chama kingine na kukiimarisha.

Hata sasa, pengine kuna wana CCM mamlaka za chama zinatamani kuwatimua, lakini wanahofia kuimarisha upinzani. Ukiyajua mengi ya siasa, hakuna mwana CCM atatamani vyama vingi vifutwe.