Wapinzani wajitoe wakijua wanalo deni la matumaini kwa Watanzania

Chadema na ACT-Wazalendo wamejitoa kushiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika mwezi huu. Nani wa kuwalaumu kutokana na mazingira ya sasa? Hata hivyo wanalo deni la matumaini ambalo wana wajibu wa kulilipa kwa Watanzania.

Deni ambalo wapinzani wanadaiwa limo ndani ya nukuu ya Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally kuhusu nidhamu ya Watanzania kujiandikisha na kupiga kura. Nukuu hiyo ipo kwenye video inayosambaa mitandaoni.

Bashiru anasema “kuna wale ambao naweza kuwaita ni wajanja, wapigakura wa Tanzania, ambao wamefikia hatua ya kudharau uchaguzi, wanakaa nyumbani kwa sababu wanaona uchaguzi ni kituko, wanaona ni mchezo wa kuigiza, na ndiyo maana leo kupata watu kuhudhuria kwenye kupiga kura imekuwa shida. Kote tunaposhinda ni chini ya asilimia 30, chini ya asilimia 40.”

Nukuu hii inaundwa na mantiki kuwa Watanzania zaidi ya asilimia 60 hawana matumaini na uchaguzi. Hivyo, huwa hawaoni umuhimu wa kujiandikisha wala kupiga kura. Siku ya uchaguzi ikifika wao wanajishughulisha na mambo mengine au wanakaa nyumbani.

Turejee kwenye vyama kujitoa uchaguzi Serikali za Mitaa. Nauliza tena, nani wa kuwalaumu wapinzani? Dk Bashiru anasema Watanzania wanaona uchaguzi ni kituko. Nchi nzima imeshuhudia mambo ya kustaajabisha kuwahi kutokea.

Watanzania wengi hawakuwa na mwamko wa kujitokeza kujiandikisha. Vilitolewa mpaka vitisho kwa viongozi wa mikoa na wilaya kuhamasisha au kulazimisha watu wajiandikishe, wakatishia kuwafuata wananchi baa na hata kukagua watumishi wa umma maofisini.

Kwa nini ilitokea hivyo? Jibu ni lilelile la Dk Bashiru, kwamba Watanzania wanaona uchaguzi ni kituko. Wanaona kujiandikisha na kupiga kura ni kujisumbua, kwao uchaguzi ni mchezo wa kuigiza.

Awamu ya mivutano kuhusu kujiandikisha ilipita, ikawadia ya wagombea kujitokeza kuchukua fomu. Yakaibuka malalamiko chungu nzima, kwamba maofisa watendaji wa kata walijificha ili wasiwape fomu wagombea wa upinzani.

Awamu hiyo nayo ikapita, ikafuata ya kurejesha fomu, wapinzani sehemu nyingi walidai kukuta ofisi za watendaji wa kata zimefungwa mpaka muda wa kurejesha fomu ulipopita.

Hayakuishia hapo, ikafuata awamu ya ubatilishaji wa ushiriki. Ripoti zikatolewa kuwa vyama vya upinzani vimekosa sifa ya kushiriki uchaguzi kwa asilimia 90, kwani wagombea wake walikosea kujaza fomu.

Ikiwa vyama vimekosa ushiriki kwa asilimia zaidi ya 90 nchi nzima, vikijitoa nani wa kuvilaumu? Vyama vyote vya upinzani vyenye uwakilishi bungeni vinalia kuchezewa rafu. Profesa Ibrahim Lipimba (CUF), analia kilio kimoja na James Mbatia (NCCR-Mageuzi), Freeman Mbowe (Chadema) na Zitto Kabwe (ACT-Wazalendo). Vyama vingine ambavyo pengine hata wagombea havina vimetangaza kushiriki.

Uhuni na kituko

Profesa Lipumba amesema hajawahi kuona uchaguzi wa kihuni kama huu. Lipumba ni mzoefu wa siasa za vyama vingi. Aligombea urais wa kwanza wa vyama vingi mwaka 1995, kisha 2000, 2005 na 2010. Mwaka 2015 pekee ndio hakugombea.

Mwaka 2000 na 2005, Lipumba alitoka mshindi wa pili wa urais. 1995 na 2010 alikuwa wa tatu. Lipumba anaongoza CUF ambacho ni chama kilichoongoza upinzani kwa miaka 15.

Bila shaka, Lipumba ni mtu wa kusikilizwa sana anapotoa maoni au tathmini kuhusu uchaguzi. Ameshiriki na kuhusika moja kwa moja. Yeye anasema hajawahi kuona uchaguzi wa kihuni kama huu wa Serikali za Mitaa.

Januari 26 na 27, 2001, CUF walifanya maandamano Zanzibar na Dar es Salaam, kupinga matokeo ya Uchaguzi Mkuu 2000 yaliyompa ushindi wa urais Zanzibar, Aman Karume, dhidi ya Seif Sharif Hamad.

Lipumba aliongoza maandamano hayo yaliyosababisha athari kubwa, vifo, majeruhi, upotevu wa watu na Watanzania wengi walikimbia nchi.

Lipumba anasema uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka huu kwa tathmini yake, ni wa kihuni kuwahi kushuhudia. Kwa maana hiyo anaona unazidi ule wa mwaka 2000 Zanzibar ambao uliacha historia chafu isiyofutika kwa Watanzania.

Kuna tatizo kubwa

CCM wanafurahia kushinda bila uchaguzi kwa lugha ya kupita bila kupingwa. Wapinzani wanasusia uchaguzi. Wananchi wanagoma kujiandikisha wala kupiga kura kwa sababu wanaona uchaguzi ni kituko.

Nchi inaumwa “upagani wa uchaguzi”. Waingereza wanaita “election nihilism”. Kwamba hakuna aliye na imani na uchaguzi. CCM wanaona bora ushindi bila uchaguzi. Wapinzani na wapigakura wanaona uchaguzi umejaa mazingaombwe.

Tanzania tangu mfumo wa vyama vingi urejeshwe mwaka 1992, nchi haijawahi kushuhudia makosa ya CCM ili mpinzani apite bila kupingwa. Wapinzani ndio hufanya makosa na CCM kushinda bila uchaguzi.

Mwaka huu, imeonekana wapinzani asilimia 90 walikosea taratibu za kushiriki uchaguzi na kujaza fomu, lakini CCM nchi nzima wamepatia. Hiki ndio kituko kama alichosema Dk Bashiru.

Tanzania ambayo inakua, watu wanaelimika, teknolojia imetanuka, eti ndio watu wakosee kujaza fomu kuliko wakati mwingine wowote katika historia. Huu ni mchezo wa kuigiza kama aliousema Dk Bashiru.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tamisemi, Selemani Jafo, ambaye wizara yake ndiyo inaendesha uchaguzi, anataka wapinzani wakate rufaa ili waruhusiwe kushiriki uchaguzi. Rufaa nazo zilikataliwa.

Kwa maana hiyo, hata waziri ambaye ndiye hasa msimamizi mkuu wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa, hasikilizwi. Au alitamka kwenye vyombo vya habari halafu chini kwa chini akasisitiza waondolewe?

Deni la matumaini

Upagani wa uchaguzi unapokuwepo kwenye nchi, maana yake upande mmoja watu wanaona hakuna matumaini, wakati huohuo kundi lingine linaona uchaguzi hauna maana, muhimu ni kukaa madarakani.

Hivyo, wapinzani wanapitia misukosuko. Wanapitishwa kwenye chungu cha moto kila unapowadia uchaguzi. Wanajiona wapo katikati ya mamlaka isiyoona umuhimu wa uchaguzi na wananchi waliokata tamaa.

Wanaamua kususia uchaguzi. Si kosa lao. Hata hivyo, wajue hii si mara ya kwanza kususa na wawe na uhakika wa nini watakipata. Mfano, Maalim Seif alisusia uchaguzi wa marudio Machi 20, 2016, akidai alidhulumiwa ushindi katika Uchaguzi Mkuu 2015, nini alipata? Dk Ali Mohamed Shein anakwenda kumaliza muhula wa uongozi.

Wapinzani walisusia mara nyingi uchaguzi mdogo wa ubunge na udiwani kati ya mwishoni mwa mwaka 2016 mpaka mwaka huu, nini walipata? CCM wanatangazwa washindi na kuongoza ofisi. Wakati huohuo wananchi wanazidi kuona uchaguzi hauna maana.

Kwa msingi huo, tamko la wapinzani kujitoa halitoshi, walipaswa kwenda mbele na kusema ambacho hawajawahi kusema ili kuonyesha safari hii ni tofauti na nyakati zilizopita.

Wapinzani wakisema ambacho hawajakisema, pengine kitarejesha matumaini ya wananchi katika uchaguzi na mamlaka zitaona umuhimu wa kuheshimu uchaguzi.

Nini ambacho wanataka kufanya zaidi ya kujitoa? Hilo ndilo deni la wapinzani ili kuwapa matumaini waliokata tamaa.