Mastaa wanaotikisa Ligi ya Mabingwa Ulaya

Raundi ya pili ya mashindano Ligi ya Mabingwa Ulaya itaanza Novemba 5, mwaka huu.

Timu 16 zinatarajiwa kuingia vitani kuwania pointi ambazo zitatoa fursa kwao kufuzu hatua ya 16 bora kwenye mashindano hayo.

Kinachovutia katika mashindano hayo ni kuchomoza baadhi ya mastaa ambao awali hawakuwa na majina makubwa katika soka Ulaya.

Kitendo cha kucheza kwa ufanisi kimeanza kuwaweka mawindoni katika usajili wa dirisha dogo au majira ya kiangazi msimu ujao.

Mbali na klabu kutaka mafanikio katika mashindano haya, lakini nyingi zinatumia fursa ya kuona vipaji vipya ambavyo vitakuwa na tija.

Katika makala haya tumechambua wachezaji wazoefu na wale chipukizi ambao wameonyesha viwango bora.

Raheem Sterling wa Manchester City mwenye mabao manne alifunga matatu katika mchezo dhidi ya Atalanta na kutoa pasi ya bao kwa Sergio ‘Kun’ Aguero.

Winga wa Bayern Munich Serge Gnabry ana mabao manne aliyofunga katika ushindi wa 7-2 dhidi ya Totenham Hotspurs.

Mbali na Sterling, Gnabry, lipo kundi la wachezaji sita waliong’ara katika mashindano hayo wakiongozwa na mshambuliaji nguli wa Bayern Munich Robert Lewandowski.

Erling Haaland- Salzburg

Mshambuliaji huyo kinda mwenye miaka 19 wa Norway anaongoza kwa ufungaji bora mpaka sasa kwenye michuano hiyo akiwa na mabao sita nyuma ya Robert Lewandowski mwenye matano.

Licha kuwa na idadi ya mabao, Haaland anashika nafasi ya pili kupiga mashuti mengi golini kwa wapinzani wake amepiga mara nane chini ya Lewandowski aliyefanya hivyo mara tisa.

Katika msimamo wa Kundi E timu yake ipo nafasi ya tatu kwa pointi tatu ilizopata dhidi ya KRC Genk baada ya kuicharaza mabao 6-2 katika mchezo wa kwanza nchini Austria.

Robert Lewandowski-Bayern

Licha ya kushika nafasi ya pili ya ufungaji akiwa na mabao matano na kuibeba timu yake katika kila mchezo, nguli huyo wa zamani wa Borussia Dortmund amepiga mashuti tisa.

Nyota huyo wa Poland anapewa nafasi kutokana na uwezo wake ambao haujashuka muda mrefu na uwezekano wa timu yake kufika mbali kulinganisha na Haaland.

Roberto Firmino-Liverpool

Nyota huyo raia wa Brazil haonekani kwenye kufunga lakini kazi kubwa anayofanya uwanjani unaweza usiione kwa urahisi, lakini ni mtu hatari zaidi.

Katika michezo mitatu aliyocheza hajafunga hata bao lakini anaongoza kwa kutoa pasi nne za mabao nyuma ya Takumi Minamino wa Salzburg aliyetoa tatu.

Kylian Mbappe-PSG

Winga huyo wazamani wa Monaco ana mabao matatu na pasi moja ya bao, amezidiwa bao moja na Harry Kane na Mislav Orsic wa Dinamo Zagreb.

Mfaransa huyo amefunga mabao ndani ya dakika 67 tofauti na wawili hao waliocheza zaidi ya dakika 200 katika michezo yote mitatu. Mbappe hakucheza dhidi ya Real Madrid na Galatasaray ambayo PSG ilishinda yote na alirejea kuikabili Club Brugge akitokea benchi.

Harry Kane-Spurs

Nahodha huyo wa England amefunga mabao manne na kuiwezesha timu yake kushika nafasi ya pili ikiwa na pointi nne katika msimamo wa Kundi B nyuma ya Bayern Munich yenye tisa. Kane anashika nafasi ya tatu kwa kupiga kiki nyingi.

Mislav Orsic-Dinamo Zagreb

Kiungo huyo raia wa Croatia ana mabao manne. Ameingia katika vitabu vya historia baada ya kufunga matatu katika mchezo dhidi ya Atalanta.

Pamoja na wachezaji hao kufanya vizuri wapo wengine wameonyesha ubora lakini hawapo katika orodha.

Mastaa hao ni Dries Mertens (Napoli), Mohammed Salah (Liverpool) Mauro Icard (PSG), Memphis Depay na Heung Son (Spurs).

Cristiano Ronaldo na Lionel Messi hawajaonyesha makeke. Ronaldo ana bao moja alilofunga dhidi ya Bayer Levekusen na Messi alipoifunga Slavia Praha.