Mastaa watano Ligi Kuu Bara waliozipa mgongo fani tofauti walizosomea

Kama ilivyo kwa wachezaji wa ligi za wenzetu kama vile Ligi Kuu England (EPL), basi na Ligi Kuu Bara (TPL) inao wasomi ambao waliamua kuachana na fani walizosomea na kujikita katika soka.

Miongoni mwa wachezaji wasomi wa EPL walioweka kando taaluma zao ni pamoja na kiungo wa Manchester United, Juan Mata ambaye alianza kuwa na shahada ya uandishi wa habari ambayo aliipata huko Madrid nchini kwao Hispania.

Licha ya kutokuwa na nafasi ya kucheza mara kwa mara katika kikosi cha United, akiwa nchini England ambako alianza kuichezea Chelsea alisomea shahada mbili zaidi - ya Sayansi ya Michezo (Sports Science) na Masoko (Marketing).

Huo ni mfano wa wenzetu, lakini kwa Tanzania kuna baadhi ya wachezaji ni wasomi, hivyo tuwaangalie wachezaji watano hapa nchini akiwemo mshambuliaji wa Namungo, Reliants Lusajo anayeuwasha moto katika Ligi Kuu Bara akiwa miongoni mwa washambuliaji wenye mabao mengi.

Reliants Lusajo

Anaweza kuwa miongoni mwa wachezaji wasomi Ligi Kuu Bara akiwa na shahada ya Manunuzi na Ugavi ambayo aliipata katika Chuo cha Ushirika kilichopo mjini Moshi na hapa anaelezea umuhimu wa elimu aliyopata katika soka lake.

“Nashukuru Mungu kwa elimu niliyonayo, nimekuwa na uwezo wa kusimamia mambo yangu mengine nje ya soka, kwa ambacho nimekuwa nikikipata najitahidi kuwekeza, pia naitumia kushauri watu kulingana na ufahamu nilionao katika eneo langu nililosomea,” anasema nyota huyo.

Kwa nini Lusajo ambaye aliwahi kuichezea Yanga hakutafuta kazi katika ofisi kubwa na kufanya kazi aliyosomea.

“Mpira ni sehemu ambayo niliona naweza kufanikiwa zaidi kimaisha tofauti na kazi za ofisini, sisemi kuwa sitafanya, naweza kuhamia upande huo kama ukifika muda wa kustaafu soka.”

Salmin Hoza

Alitikisa Ligi Kuu Bara akiwa na Mbao FC iliyokuwa chini ya Etienne Ndayiragije ambaye kwa sasa ni kocha wa timu ya taifa ya Tanzania, wakati Hoza akiwa mchezaji wa Azam walikuwa wote hapo kabla ya kocha huyo Mrundi kupata nafasi ya kulitumikia taifa.

Hoza ambaye ni kiungo mkabaji ana stashahada ya Manunuzi na Ugavi ambayo aliipata katika Chuo cha Biashara (CBE) mjini Mwanza mwaka 2016.

Mchezaji huyo anasema ilikuwa rahisi kwake kuhamia katika soka kutokana na kupata kwake nafasi ya kusajiliwa na klabu ya Mbao FC baada ya kumaliza chuo.

“Nilikuwa nikisoma huku nikicheza soka, nilivyosajiliwa sikuona umuhimu wa kuendelea na shule,” anasema mchezaji huyo.

Ayubu Semtawa

Semtawa mwenye stashahada ya Tiba ndiye mchezaji msomi zaidi katika kikosi cha Coastal Union ya Tanga kilicho chini ya Juma Mgunda.

Mchezaji huyo anasema inawezekana kutenga muda wa shule na ukacheza soka.

“Kwa wenzetu unakuta mchezaji anasoma huku anacheza mpira, hivyo wito wangu kwa wachezaji wenzagu ni kwamba zikipatikana nafasi tujiendeleze,” anasema.

Paul Nonga

Nonga ambaye aliwahi kuichezea Yanga na Mbeya City, amekuwa mmoja wa wachezaji muhimu kwenye kikosi cha Lipuli ya Iringa.

Mshambuliaji huyo hatari ana stashahada ya Ulipuaji Miamba.

“Siku zote nimekuwa nikifanya kile ambacho kina masilahi kwangu, mbali na kupenda soka ni sehemu ambayo inaendesha maisha bila ya kusuasua kufanyia kazi nilichosomea labda baadaye sana,” anasema.

Roland Msonjo

Nyota wa Mbeya City, Roland Msonjo anatajwa kwenye orodha ya wasomi Ligi Kuu Bara na inaelezwa kuwa mchezaji huyo ana stashahada ya Biashara.

Huenda wachezaji hawa kama isingekuwa soka basi wangejikita kufanya kazi za kitaaluma ambazo wamezisomea miaka ya nyuma.