Nyota Yanga afunguka maisha ya Ukraine

Monday May 6 2019

 

By Thomas Ng’itu, Mwanachi tng’[email protected]

Ndoto ya Tanzania kuwa na idadi kubwa ya wachezaji wanaocheza soka la kulipwa nje ya nchi imeanza kutimia baada ya mshambuliaji kinda wa Yanga, Yohana Mkomala kufuata nyayo za kaka zake.

Safari ni zamu ya Mkomola kutoka nje ya mipaka ya Tanzania baada ya kufaulu majaribio ya kujiunga na klabu ya Arsenal Kiev.

Hii ni neema kwa soka la Bongo kwasababu Tanzania inazidi kujitangaza kadri siku zinavyozidi kwenda, baada ya mshambuliaji wa Tanzania, Mbwana Samatta kung’ara na kikosi cha KRC Genk ya Ubelgiji.

Wiki iliyopita Mkomola aliyekuwa anakicheza kwa mkopo African Lyon akitokea Yanga, alipata ‘dili’ la kwenda Ukraine na kutia saini mkataba wa miaka mitatu kuitumikia Arsenal Kiev.

Mkomola alisajiliwa na Yanga mwaka 2017 baada ya kung’ara na timu ya Taifa chini ya miaka 17 ‘Serengeti Boys’ iliyoshiriki Fainali za Afcon 2017.

Usajili wa Mkomola ulishitua wadau wengi kutokana na timu ambayo Mkomola amekwenda kujiunga nayo. Samatta alianza kucheza soka la kulipwa DR Congo akiwa na TP Mazembe kabla ya kutimkia Ulaya.

Spoti Mikiki ilizungumza na Mkomola kwa simu akiokea Ukraine ambapo alieleza mambo mengi kuhusu maisha yake mapya.

Tunisia

Hii si mara ya kwanza Mkomola kupata fursa ya kwenda kufanya majaribio kwani aliwahi kupata ofa Tunisia katika klabu ya Etoile Du Sahel lakini hakufanikiwa na alirejea Yanga.

Baadhi ya wadau walimbeza wakimuona ameshapotea hasa pale ambapo alikuwa hachezi na baadaye kutolewa kwa mkopo kwenda African Lyon kabla ya kupata mkataba wa kwenda Ukraine.

Mkomola alisema baada ya kupitia magumu mengi, hivi sasa ndio kwanza safari yake imeanza katika kutafuta maisha ya kucheza soka la kulipwa kwa upande wake.

“Haya ni maisha yangu ambayo nilikuwa natamani siku moja nifike, sitakubali hata kidogo kukubali nipotee, nahitaji kufika mbali zaidi ya hapa.

“Nimetia saini miaka mitatu lakini ninaamini sitaweza kukaa hapa miaka mitatu, najua nitaonekana na kuzidi kupiga hatua. Kwangu hii ni fursa nataka nicheze kwa bidii nipate klabu kubwa za Ulaya”.

Lugha

Mkomola anasema lugha ya Ukraine inampa taabu kwa kuwa anazungumza kwa ufasaha lugha ya Kiingereza na Kiswahili.

“Lugha ni changamoto kwasababu wanachozungumza sifahamu kabisa inafika hatua wakiongeza sipati kitu. Lakini jambo la kufurahisha ni watu wa utani zaidi na wamenipokea vizuri,” anasema Mkomala.

Kinda huyo anasema hana tatizo na lugha ya kufundishia soka uwanjani kwa kuwa inafanana kwa wanamichezo wote duniani.

Changamoto

Ni ngumu mchezaji kwenda moja kwa moja na kupata nafasi ya kuanza katika kikosi cha kwanza, hiyo imeonekana kwa wachezaji wengi wa kitanzania wanapotoka nchini kwenda nje.

Ilimchukua miezi kadhaa Samatta kupata nafasi ya kuanza moja kwa moja katika kikosi cha Genk, hivyo hata kwa Mkomola pia tayari ameanza kujipanga mapema kuhakikisha anapata nafasi ya kuanza katika kikosi hicho msimu ujao.

“Si jambo rahisi kupata namba katika kikosi cha kwanza, inabidi nipambane vya kutosha ili kuweza kuingia katika kikosi, hakuna kulala ni kazi juu ya kazi nimekuja sehemu ambayo wametuzidi kila kitu kwahiyo kujituma kwangu ndio kutanifanya nipate nafasi ya kuanza katika kikosi cha kwanza,” anasema.

Mkomola alifunguka zaidi na kusema amekuwa katika wakati mgumu na wachezaji baadhi kwani hawampi ushirikiano wa kutosha lakini hilo halijamkatisha tamaa.

“Mazoezini ukikosea kidogo au ukifanya vizuri unakuta mtu ambaye unacheza naye namba moja anaonyesha sura fulani ya kutofurahishwa, lakini mwalimu anakuelekeza polepole hivyo mimi imani ya kuzidi kupambana inazidi kuwepo,” anasema kinda huyo.

Malengo

“Unajua ndugu yangu hii ni hatua kubwa ambayo nimepiga, sihitaji kurejea nyuma badala yake ni kusogea mbele zaidi, naamini nitatimiza ndoto zangu”.

Anasema hataki kukumbuka magumu aliyopitia wakati alipokuwa nje ya uwanja kabla ya kupata dili la kwenda Ukraine kufanya majaribio.

“Nilifanya majaribio kwa hasira sana nilikumbuka jinsi nilivyosota mtaani, lakini nashukuru Mungu nimefanikiwa, sitaki kukumbuka maisha ya nyuma,” anasema Mkomola.

Kauli ya Meneja

Meneja wa mchezaji huyo DK Alfred Amede akishirikiana na Johnson Pallangyo, anasema haikuwa kazi rahisi mchezaji huyo kupata timu Ulaya.

“Nimesoma Ulaya kwahiyo nilitengeneza mtandao na marafiki wengi, nimekuwa nikiwatibu watu wengi kwahiyo nilipotuma video kwa mmoja wa watu wangu wa karibu na kuvutiwa naye ndio wakampa nafasi ya kufanya majaribio,” anasema Amede.

Meneja huyo anasema kucheza kwake Serengeti Boys na Yanga kulimuongezea fursa ya kukubalika na benchi la ufundi la Arsenal Kiev.

Advertisement