Simba, Yanga zawarudisha uwanjani Mziba, Kibadeni

Tuesday August 6 2019

 

By Imani Makongoro, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Yanga kwa mara ya kwanza imekata kiu ya muda mrefu ya mashabiki wake, baada ya kuwaweka hadharani nyota wake wapya wakiwemo wa kigeni.

Yanga jana iliwatambulisha rasmi mastaa wake wapya katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa waliocheza dhidi ya Kariobang Sharks ya Kenya uliokuwa maalumu kwa ajili ya kuadhimisha Siku ya Wananchi.

Yanga imesajili wachezaji 10 wa kigeni. Pia Simba imenasa saini za mastaa 10 wa kigeni.

Usajili wa Simba na Yanga umewaibua nyota wa zamani wa klabu hizo kongwe ambao wamevichambua vikosi hivyo na kueleza matarajio yao kwa timu hizo katika Ligi Kuu Tanzania Bara na Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao.

Kauli za wadau

Mpachika mabao wa zamani wa Yanga, Abeid Mziba ‘Tekelo’ anasema msimu uliopita timu hiyo ilikuwa na udhaifu katika safu zote kuanzia kwa kipa.

Advertisement

“Kero kubwa katika kikosi chetu ilikuwa safu ya ushambuliaji. Lakini kwa usajili huu naamini tutakuwa tumemaliza kasoro hiyo baada ya ujio wa Molinga David. Mchezaji huyo ambaye usajili wake umemuweka njiapanda kipa Klause Kindoki ambaye anaweza kutupiwa virago ili Yanga itimize idadi ya wachezaji 10 wa kwa mujibu wa kanuni.

“Nafikiri Ndama atakidhi kiu ya mashabiki Yanga kwa kufunga mabao, nimemtazama umbo lake ni ya aina ya washambuliaji wazuri, ngoja tumpe muda,”anasema Mziba. Mziba aliyekuwa mkali wa mabao ya kichwa, anasema Yanga imefanya mabadiliko makubwa ya kikosi chao ambayo kila shabiki ana matumaini yatakuwa na tija msimu ujao.

Nyota mwingine wa timu hiyo, Peter Tino anasema usajili umebadili fikra za mashabiki wengi ambao msimu uliopita walishuhudia timu yao ikishinda kwa bahati.

“Pamoja na kwamba tulikuwa tunashinda, lakini kwa bahati. Msimu huu hata tutakapokutana Simba na Yanga mbona patakuwa hapatoshi,”anasema Tino.

Kiungo wa zamani wa Simba, Mtemi Ramadhani anasema pamoja na kwamba mashabiki wengi wa Simba hawajapata fursa ya kuwaona wachezaji wapya, lakini kwa usajili wa majina inatosha kuthibitisha umefanyika kwa kiwango bora.

Abdallah Kibadeni aliyewahi kuwa mchezaji na kocha wa timu hiyo kwa nyakati tofauti alisema hana shaka ubingwa wa Ligi Kuu msimu ujao utaendelea kubaki Simba kwa mara ya tatu mfululizo.

Kambi

Mbali na kusifu ubora wa vikosi vyao, nguli hao wamezichambua kambi hizo huku Yanga ikipewa pongezi kwa kambi ya Morogoro na wameitaja ilikuwa ni bora kulinganisha na ile ya Simba iliyoweka Afrika Kusini.

Mtemi licha ya kuwa shabiki wa Simba anasema kambi ya Yanga Morogoro ilikuwa nzuri kulinganisha na klabu yake. “Ni kweli wenzetu Afrika Kusini wako vizuri katika vifaa vya mazoezi na Simba ilipata fursa ya kucheza na Orlando Parates na kutoka sare ambayo ni matokeo mazuri ambayo yanasababisha mashabiki kuwa na shauku ya kutaka kuona Simba imeongeza kitu gani huko.

“Lakini kwa mchezaji kisaikolojia unapokwenda kuweka kambi nje ya nchi utahitaji kutembea kidogo kuangalia mazingira ya nchi uliyokwenda hivyo umakini kidogo unapungua,”anasema.

“Tutajua uwanjani timu ipi ni bora zaidi ya mwenzake, sisi tumeweka kambi Morogoro sawa, tumecheza na Friends Rangers mechi ya kirafiki pia ni sawa lakini naamini Yanga kuna kitu tulikuwa tunajifunza,”anasema Mziba.

Kibadeni anasema aliyekuzidi kakuzidi tu, kwani huwezi kulinganisha ubora wa kambi ya Afrika Kusini na ile ya Morogoro kwa watani wao. Wakati Tino yeye anasema kuweka kambi Afrika Kusini si ajabu na jambo la msingi ni kuona timu inafanya nini uwanjani, hivyo wakutane katika ligi.

Ushindani

Nyota hao kwa nyakati tofauti wanasema pamoja na kwamba ushindani wa timu hizo mbili zinapokutana hautabiriki, lakini msimu ujao itakuwa ni vita.

“Msimu uliomalizika Yanga tulikuwa na wakati mgumu, lakini Simba walitufunga mabao ya bahati tu, msimu huu tumekamilika sijui nini kitatokea ni vyema tusubiri,”anasema Mziba.

Tino anasema zitakapokutana timu hizo wala hana presha ya ushindi kwani akiutazama usajili waliofanya anahesabu mabao tu.

Wakati Mtemi akisisitiza kuwa kwa kikosi cha Simba, kinatosha kuthibitisha kuendeleza ubabe kwa watani wao Yanga msimu ujao licha ya kudai hata usajili wa Yanga unampapresha kwani sio Yanga dhaifu waliyoibeza msimu uliopita.

Kibadeni yeye anaamini Yanga itaendeleza ‘uteja’ kwa Simba akisisitiza kuwa kwa maandalizi ya timu hiyo, maisha wanayoishi na kikosi walichonacho hakuna cha kuwanyima ubingwa kwa mara nyingine katika mashindano ya Ligi Kuu Tanzania Bara.

Advertisement